HEADER AD

HEADER AD

ZAIDI YA WANAFUNZI 20 SIMIYU NI WAJAWAZITO


 Na Annastazia Paul, Simiyu.

>>>RC Simiyu amwagiza RPC, OCD kuwakamata waliowapa mimba wanafunzi.

MKUU wa mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda amemuagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu ACP Blasius Chatanda na Wakuu wa Polisi Wilaya kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote waliowapa mimba wanafunzi.

Akizungumza wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Itilima, mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa hadi sasa zaidi ya wanafunzi 20 mkoani humo wamegundulika kuwa wajawazito.


"Nimetoa agizo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, na ma-OCD wote kuhakikisha kwamba wale wote waliowapa mimba wanafunzi wanakamatwa na wachukuliwe hatua kali za kisheria, na hata waliowaozesha watoto wa shule nao wakamatwe pia.

"Haiwezekani Rais ametoa pesa nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa halafu wanafunzi wasisome, ni lazima watoto wangu muwalete shule." Amesema Dkt. Nawanda.

Diwani wa Kata ya Nhobora Mbuke Mlyandingu ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule ya sekondari katika Kata hiyo huku akiomba wapelekwe walimu wa kutosha shuleni hapo kwani kuna upungufu wa walimu.


"Tunaishukuru sana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule yetu ya sekondari ya Nhobora, uwepo wa shule hii utawasidia wanafunzi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu.

"Walikuwa wanatembea kilomita zaidi ya 10 kwenda shuleni lakini sasa watakuwa wakisoma hapa karibu, niombe tu Serikali ituletee walimu wa kutosha, kwa sasa shule hii ina walimu watano pekee hawatoshi Serikali ituongezee walimu hapa." Amesema Mlyandingu.

Nao baadhi ya wananchi wa Kata hiyo wamesema kuwa ujenzi wa shule katika maeneo yao umesaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shuleni jambo lililokuwa likiwafanya wengine kushindwa kumaliza masomo yao.

       Wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

"Kipindi cha nyuma wanafunzi walikuwa wanahangaika sana walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda shule mpaka wengine walikuwa hawamalizi masomo yao walikuwa wanaacha shule." Amesema Jesca.

Joshua Mabula ambaye pia mkazi wa kata ya Nhobora ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule na madarasa katika Kata hiyo.

"Watoto wetu walikuwa wanatembea umbali mrefu sana kwenda shule lakini kwa sasa wanapata elimu hapa hapa katika maeneo ya karibu hakuna tena shida kutembea kilomita zaidi ya 12 kwenda shule, tunaishukuru sana Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan." Amesema Joshua.
   




No comments