HEADER AD

HEADER AD

AFISA KAZI : WAAJIRI MSIWATELEKEZE WAFANYAKAZI WANAOPATA AJALI KAZINI

Na Dinna Maningo, Musoma

MWAKILISHI wa Idara ya Kazi mkoani Mara Raphael Mauna amewataka waajiri kutenda haki na kuwalipa shahiki zao wafanyakazi wanaopata ajali pindi wawapo kazini na siyo kuwatelekeza.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la mwalimu mstaafu ambaye ni mjasiriamali Doto Magera aliyeuliza kutaka kufahamu iwapo kama alistafu kazi na kulipwa stahiki zake zote na akapata kazi sehemu nyingine kwa mkataba wa kazi je atakapopata ajali kazini ana haki ya kulipwa fidia?.

         Wajasiriamali mjini Musoma

Mwalimu huyo aliuliza swali wakati afisa huyo akitoa mada juu ya masuala ya ajira na kazi katika kongamano lililoandaliwa na Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists ) mkoani Mara,

Kongamano hilo lilihudhuliwa na Wajasiriamali na wawezeshaji wa mada kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, lililofanyika Viwanja vya Mukendo Mjini Musoma.

"Kwasababu ulikuwa mwajiriwa haijalishi ulikuwa na umri gani ajali uliyoipata inatokana na kazi uliyokuwa unaifanya, unastahili kulipwa fidia na wengi hawajui hizi fidia unazifidiwa vipi.

"Utakapokuwa umepata changamoto ukifika sisi tutakusaidia, tunafahamu wazi kwamba kuna ndugu zetu wengi wamekufa kutokana na kazi walizokuwa wanafanya na pia kuna wengine wameugua kutokana na kazi walizofanya, watu wamepata ulemavu na waajiri wakawaondoa kazini bila kuwalipa stahiki zao.

Raphael amesema iwapo mtu kapata changamoto akiwa kazini anapaswa kutafuta suluhu mapema kujua changamoto iliyomkumba imesababishwa na nini na kama imetokana na kazi aliyokuwa akiifanya anapaswa kufika ofisi ya kazi kueleza matatizo yake.
  Afisa Kazi mkoani Mara Raphael Mauna

"Njoo ofisini mwajiri wako ataitwa ataelezwa kama kuna uwezekano wa kutoa tiba atatoa tiba kama itashindikana tutaangalia kama alikuwa anachangia kwenye mfuko, na kama alikuwa hachangii kwenye mfuko atawajibishwa kisheria.

Amesema kuwa watu wengi wanapoteza haki zao kwa kuchelewa kufikisha madai yao ofisi ya kazi kwani sheria ya mfuko kwa wafanyakazi inataka mtu kufikisha malalamiko yake ndani ya mwaka mmoja tu.

"Changamoto kubwa ni kwamba wengi wanapopata hizi changamoto wanaamua kukaa kimya, baada ya miaka 9 anakuja ofisini kuhitaji msaada, sheria inakutaka ulete malalamiko ndani ya mwaka mmoja na kama itakuwa nje ya hapo basi kuwe na sababu ya msingi.

"Lakini pia unatakiwa ulete malalamiko ya kufukuzwa kazi ndani ya siku 30 tu nje ya hapo uwe na sababu ya msingi , madai mengine yote ya mshahara, posho na vitu vingine vyote yaletwe ndani ya siku 60.

Amesema mtu anapochelewa kupeleka madai yake anajinyima mwenyewe haki zake na kwamba akipata tatizo kazini asisubiri tatizo kuwa kubwa kwani mwajiri humpenda mfanyakazi pale anapokuwa na nguvu akipata ugonjwa au ulemavu hakuhitaji tena.


"Ukipata changamoto nenda pia kwa mwanasheria, mahakamani utapata elimu, usisubiri tatizo likiwa kubwa ambalo sasa huwezi kupata suluhu, yawezekana hata mwajiri wako alishafirisika hana cha kukusaidia tena au alishafariki.

Ameongeza kuwa mfanyakazi anakuwa na thamani kwa Mwajiri pale anapokuwa mzima kiafya lakini akipata shida ya kiafya anakuwa adui kwa mwajiri hamtambui tena.


















































































No comments