HEADER AD

HEADER AD

RC KAGERA AMWAGIZA MKANDARASI KUBADILI TAA VINGINEVYO ACHUNGUZWE

 

Alodia Babara, Bukoba 

MKUU wa mkoa wa Kagera Albert Chalamila amemtaka Mkandarasi wa Otonde Construction and General Supplies Limited aliyeweka taa za umeme wa jua (Solar) katika kituo cha Malori kilichopo Ibura Kata ya Ijuganyondo Manisipaa ya Bukoba kubadili taa hizo.

Amesema vinginevyo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ianze kumchunguza mkandarasi huyo ili kuona ni kwa nini ziliwekwa taa za kiwango cha chini.

Mkuu huyo ametoa maagizo hayo Machi 13,2023 katika uzinduzi wa kituo cha Malori kilichojengwa katika kata ya Ijuganyondo wakati alipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa katika Manispaa hiyo ambapo taa 20 za wats 150 ndizo zimeonekana kuwa chini ya kiwango.



"Ukipita hapa usiku taa hizi zinawaka kama vibatari mwanga wake ni hafifu sana nitoe agizo kwa mkandarasi aliyeweka taa hizi kuzibadilisha haraka na kuweka taa zinazostahili.

"Kama akishindwa kuweka nyingine nawaagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU kuanza kumchunguza mkandarasi huyu na shughuli nzima ya ujenzi wa kituo hiki" Amesema Chalamila.

Awali Chalamila ameonyesha wasiwasi wa eneo hilo kuwa dogo ikilinganishwa na ukubwa wa heka mbili uliotajwa na Mkurugenzi wa manispaa hiyo Hamid Njovu na kumwamuru ofisa mipango miji wa manispaa hiyo kuanza kupima kona hadi kona ili mkuu huyo ajihakikishie kama eneo hilo linafika ukubwa uliotajwa na baada ya vipimo hivyo pameonekana ni ukubwa huo uliotajwa.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho cha maroli mkuu wa idara ya viwanda, biashara na uwekezaji, Philbert Gozbert amesema kituo hicho kimejengwa kwa gharama  zaidi ya sh. 475.5 milioni na mkandarasi wa mradi huo ni Otonde Construction and General Supplies Limited.

 Gozbert ametaja miundombinu iliyojengwa kwenye kituo hicho kuwa ni choo chenye matundu manne, bafu mbili, uzio wenye milango miwili wa kuingi na kutoka, jengo la mlinzi na mtoza  ushuru

Amesema malori 30 yatakuwa yanatumia kituo hicho na kila roli litakaloingia humo litakuwa linalipia sh. 5,000 na kwenda kushusha mizigo kwenye stoo kisha kurudi kwenye kituo.

Diwani wa Kata ya Ijuganyondo Ally Mohamed Ally amemuomba mkuu wa mkoa kuruhusu shughuli za kufanya usafi na kutoza ushuru zifanywe na jamii ya kata hiyo ili waweze kujiongezea kipato.

No comments