RC MARA AKEMEA VITENDO VYA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO
Na Jovina Massano, Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee ameiasa jamii kuachana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto vikiwemo vya ubakaji, ukeketaji na ulawiti.
Ameyasema hayo hivi karibuni Machi, 8, 2023 katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mukendo Manispaa ya Musoma.
Amesema kuwa hivi sasa limeshamili wimbi kubwa la ulawiti wa watoto mashuleni na kwenye mialo ambapo amekemea na kupinga vikali vitendo hivyo.
Sambamba na hilo Meja Jenerali Suleiman amewataka wazazi kushirikiana kupinga ukatili kwa dhati na kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto ili kupunguza mmomonyoko wa maadili.
Ameitaka jamii kukumbuka kuwa watoto ndiyo Taifa la kesho na wanawake ndio nguzo kuu ya nyumba na jamii na ni mhimili mkuu wa uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
"Ukatili unaweza kuisha kwa kutoa elimu kwa jamii yetu lakini pia ni muhimu uwajibikaji wa wazazi na walezi uwe na nguvu kwa kujali malezi bora ya watoto kutokana na mabadiliko yaliyopo katika jamii.
"Mkoa wetu tatizo la ukatili ni kubwa na jamii haioni kama ni tatizo, hii inachangiwa na mila na tamaduni zetu, hatuzipingi ila ziwe zenye kulinda utu wa mtu na hakuna anaezaliwa akiwa katili, malezi tunayotoa kwa watoto wetu ndio yanachangia ukatili, amesema Meja Jenerali Suleiman.
Amezikumbusha mamlaka husika kuhakikisha zinapambana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na kutoa wito kwa wanawake kutoa taarifa za ukatili na unyanyaji unaofanyika kwenye jamii zetu.
Amewahamasisha wajasiliamali walio kwenye vikundi kuomba mikopo katika Halmashauri zao isiyo na riba kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa Musoma William Gumbo amempongeza mkuu wa mkoa kwa kusimamia haki za akina mama,vijana,wanaume na watoto na kupambana na ukatili unaoendelea ndani ya jamii.
Kwa upande wake Harriet Tagatta Afisa wa kitengo cha Dawati la jinsia wilaya ya Musoma,amewataka wazazi na walezi kuwafatilia watoto wao kwani hivi sasa wimbi la ulawiti kwa watoto ni kubwa.
Amesema katika kamati alioiunda Mkuu wa wilaya ya Musoma, Halfan Haule ambayo ilifanikiwa kutembelea shule sita ilibaini jumla ya watoto 57 wamelawitiana wenyewe kwa wenyewe kuanzia darasa la tano kushuka chini, na wazazi wao hawana taarifa ya vitendo hivyo jambo ambalo linachangia kuharibu ndoto za watoto hao.
"Sisi wakina mama ndio tunachangia ukatili ndani ya familia zetu kwa kuwajibika zaidi katika shughuli zetu za kibiashara na ofisini huku watoto wanajilea wenyewe na mkiacha watoto wakijiandaa wenyewe na wala hatuna muda wa kuwakagua na jukumu hilo wanaachiwa wadada wa majumbani ambao sio wazazi hawawezi kuwakagua", amesema Harriet.
Ameongeza kuwa ushiriki wa wazazi na walezi katika kutoa elimu kwa watoto hakuna ndiyo maana mmomonyoko wa maadili unazidi kuongezeka.
Post a Comment