WANAWAKE WATAKIWA KUTOWABAGUA WATOTO WA KIUME
Na Dinna Maningo, Musoma
AFISA Maendeleo Msaidizi Kata ya Mukendo Katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Janeth Peter Mafipa amewaomba Wanawake kutowabagua watoto wa kiume kwani wapo hatarini kutokana na kuwepo kwa vitendo vya ulawiti.
Ameyasema hayo Machi, 04, 2023 Katika kongamano lililoandaliwa na Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists ) mkoani Mara, lililohudhuliwa na wajasiriamali wanawake na wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi lililofanyika viwanja vya Mukendo mjini Musoma.
Wanawake Wajasiriamali mjini Musoma wakiburudika na Afisa maendeleo Kata ya Mukendo, Janeth Peter Mafipa ( wa kwanza kulia) kwenye Kongamano la Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono mkoani Mara katika kuelekea siku ya Wanawake duniani inayoadhimishwa Machi, 8 ya kila mwaka.
Amesema kuwa familia nyingi zimekuwa hazimjali mtoto wa kiume na badala yake humwangalia mtoto wa kike pekee, hivyo amewaomba wanawake kuwalea watoto ipasavyo.
"Akina mama kila mtu asimamie familia ipasavyo, kuna mtindo mmoja nimeuona kuna familia nyingi hazimwangalii mtoto wa kiume wanaangalia mtoto wa kike.
"Unakuta nyumba imejengwa chumba cha mtoto wa kike kipo karibu na chumba cha wazazi lakini mtoto wa kiume chumba kimejengwa nje, mzazi hajui mtoto kaingia saa ngapi au ameondoka saa ngapi, tusiwabague watoto wetu" amesema.
Amewasisitiza wazazi kuwalea na kuwaangalia watoto wa kiume kwakuwa wapo hatarini wanawindwa na kufanyiwa vitendo vibaya vikiwemo vya ulawiti.
Pia amewaomba Wanawake kujiunga Katika vikundi ili kupata mikopo isiyo na riba inayotolewa na serikali kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Walemavu.
Aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo Joyce Sokombi, amewaomba wanawake kutenga muda wa kukaa na watoto na sio muda wote kuutumia kwenye biashara.
"Mwanamke unakuwa bize unasahau mtoto wako, mtoto anaenda shule huwezi kuona utofauti wa mwenendo wake, anarudi nyumbani hujui maendeleo yake, anaenda shule hujui kaenda saa ngapi"amesema Joyce.
Ameongeza kuwa mwanamke asiyejali familia yake na kukaa kuangalia biashara yake anajipa laana mwenyewe ambayo inaweza kusababisha biashara yake isifanikiwe.
Katibu wa Jukwaa la Wanawake Manispaa ya Musoma Mwamvua Ukwaju amesema kuwa ukatili wa kijinsia umekuwa ni tatizo kubwa ambalo linawakumba watoto wa kiume hasahasa la ulawiti.
Amesema vitendo vya ulawiti kwa watoto wa kiume limekuwa likitendeka hadi shuleni hivyo amewaomba wanawake kuhakikisha wanawalinda watoto wa kiume na sio kuegemea tu kwa watoto wa kike pekee.
Post a Comment