HEADER AD

HEADER AD

MADIWANI BIHARAMULO WAOMBA VISHIKWAMBI


Na Daniel Limbe, Biharamulo

KATIKA kile kinachoonekana ni hitaji muhimu kwa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia nchini,Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoni Kagera,wamelalamikia utaratibu wa uwasilishaji wa taarifa za maendeleo ya Kata zao kwa njia ya Kabrasha badala yake wameomba kupewa vishikwambi.

Ombi hilo maalumu limewasilishwa na Diwani wa Kata ya Nyamigogo,Mathias Nongejiwa, muda mfupi baada ya kumaliza kuwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake, kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichoketi Machi, 06,2023.

     Diwani wa Kata ya Nyamigogo, Mathias Nongejiwa,atoa ombi maalumu la madiwani kipewa vishikwambi.

Diwani huyo amesema ipo haja ya Madiwani hao kupewa vishikwambi na kuachana na uwasilishaji wa hoja kwa kutumia karatasi kwa madai jambo ambalo linaonekana kupitwa na wakati.

Kauli hiyo ikaungwa mkono na diwani wa kata ya Nyakahura, Apornal Mgalula, ambaye aliomba mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufanya mchanganuo wa gharama zinazotumika kuchapa kwenye makaratasi taarifa za maendeleo ya kila kata ikilinganishwa na iwapo wangelikuwa wakitumia vishikwambi.

" Nadhani ipo haja kwa mkurugenzi wetu kulitazama hili, ukifanya mchanganuo wa makaratasi yanayotumika kila kikao tunachokaa waheshimiwa ni gharama kubwa, bora tuwe na vishikwambi kwa wepesi wa kusoma na kujadili hoja kwa njia rahisi" amesema Mgalula.

Hoja hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita,nao kuomba kupewa vishikwambi badala ya makabrasha ambayo yamekuwa mzigo mzito wakati wa kuyasoma na kuyajadili.

Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mihayo Lutambi,akamsihi Mkurugenzi kulipa kipaumbele suala hilo kupitia fedha za makusanyo ya ndani ili madiwani hao waendane na sayansi na teknolojia.

"Niombe suala hili lipewe kipaumbele kwa sababu lina manufaa makubwa kwa halmashauri yetu, tuone namna yoyote kupitia mapato ya ndani ili ikiwezekana kabla ya mwaka 2024 tuwe na vishikwambi" amesema Lutambi.

         Mwenyekiti wa Baraza la madiwani,Leo Rushau, akifungua kikao cha Baraza hilo. 

No comments