KATIBU SHIVYAWATA AISHUKURU SERIKALI KUIPATIA SHULE VITABU VYA NUKTA NUNDU
Na Dinna Maningo, Tarime
SERIKALI imetoa vitabu vya Nukta Nundu vya masomo yote ya darasa la awali katika shule ya msingi Magufuli ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum iliyopo Kata ya Nyamisangura, katika Halmashauri ya Mji Tarime Mkoani Mara.
Ukosefu wa vitabu vya Nukta Nundu Walimu ulazimika kubadili maandishi kutoka kwenye vitabu vya kawaida na kuyachapa kuwa maandishi ya nukta nundu kwenye karatasi maalum na kudurufu kwa ajili ya kujifunzia wanafunzi wenye ulemavu wa kuona.
KATIBU wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania ( SHIVYAWATA) Halmashauri ya Mji Tarime, Mwal Mekaus Maingu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuipatia vitabu vya Nukta Nundu shule ya msingi Magufuli.
Katibu huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya watu wenye ulemavu katika halmashauri hiyo na Mwalimu anayefundisha wanafunzi wasioona darasa la nne katika shule hiyo amesema vitabu hivyo vitawasaidia wanafunzi wa awali kujifunza na kuelewa kwa urahisi.
KATIBU wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania ( SHIVYAWATA) Halmashauri ya Mji Tarime, Mwal Mekaus Maingu
"Tunaishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kutupatia vitabu kwa wanafunzi wa awali, darasa la awali ndo msingi wa elimu akijua huyu wa chekechea anakuwa na mwanga, kwahiyo serikali imefanya vizuri kuanza na hawa wa chini.
" Ni mwanzo mzuri tunaomba Serikali yetu sikivu itusaidie na madarasa mengine maana yote hayana kitabu chochote cha nukta nundu" amesema Mwl. Mekaus.
Rejea
Awali Februari, 04, 2023 DIMA Online iliripoti habari mbalimbali katika shule hiyo za mafanikio na changamoto ambapo Katibu huyo Mwl Mekaus alisema wanalazimika kubadili maandishi ya kawaida kuwa maandishi ya nukta nundu kwakuwa hawana vitabu maalum vya nukta nundu kwa ajili ya wanafunzi wasioona kujifunzia.
Kitabu cha Nukta Nundu
Alisema kutokuwepo vitabu vya nukta nundu hujikuta hawaendi na muda unaotakiwa wa ufundishaji kwakuwa muda ambao wangetumia kufundisha wanafunzi wanautumia kunakili maandishi kutoka kwenye vitabu mbalimbali vya kufundishia na kubadili katika maandishi ya nukta nundu.
" Tunafundisha masomo mbalimbali kutoka kwenye vitabu vya Hisabati, Kingereza, Maarifa ya Jamii, Uraia na Maadili, Stadi za Kazi, Afya na Mazingira, Kusoma, Kuhesabu na kuandika ambavyo ni vitabu vinavyotumika pia kwa wanafunzi wasio na mahitaji maalum.
"Muda wa kubadili na kuchapa maandishi yote ya vitabu vyote vya kufundishia kuwa maandishi ya nukta nundu alafu ufundishe hautoshi, unafanya kazi mbili kwa wakati mmoja na unashindwa kukamilisha vipindi kwa wakati, tunajikuta hatuendi na muda unaotakiwa wa kufundisha". alisema Mwl. Mekaus".
Katibu huyo wa Shiriisho la Walemavu na Mwalimu wa shule hiyo aliongeza kusema " Shule ilianza kupokea wanafunzi wasioona mwaka 2019 hadi sasa hatujawahi kupata kitabu chochote cha nukta nundu zaidi ya kubadili maandishi kutoka kwenye vitabu vya kawaida kuwa ya nukta nundu unayachapa kwenye mashine, unafanya kazi mbili kwa wakati mmoja" alisema.
Mwalimu huyo alisema kuwa vitabu vya nukta nundu ni muhimu kwa wanafunzi wasioona kujifunzia kwani vinapokuwepo vinawasaidia wanafunzi kujisomea wawapo darasani na wawapo nyumbani.
"Faida ya vitabu cha nukta nundu ukishafundisha mwanafunzi ana uwezo wa kujisomea, kutokuwepo kwa vitabu kunakwamisha ufundishaji mzuri kwa wanafunzi."alisema Mekaus.
Post a Comment