CCM BIHARAMULO YASHTUSHWA NA UUZWAJI WA CHAKULA
Na Daniel Limbe, Biharamulo
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, kimewatahadhalisha wakulima kuacha kuuza mazao ya chakula pasipo kuwa na tahadhali ya baadaye ili kujiepusha na utegemezi wa kuomba chakula cha msaada kutoka serikalini.
Imeelezwa kuwa katika msimu huu wa 2023/24 wakulima wamevuna mahindi na maharage ambapo kumeibuka wimbi la wafanyabiashara kununua mazao hayo kutoka kwa wakulima hali inayotia hofu ya utoshelevu wa chakula kwa miezi michache ijayo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Biharamulo, Robert Malulu,ameyasema hayo leo,machi 7 kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo huku akiwasihi viongozi kuwaelimisha wananchi.
"Ndugu zangu madiwani niwasihi sana muendelee kuwaelimisha wananchi wenu kuacha kuuza mazao ya chakula holela, ipo hatari ya kukosa chakula siku zijazo na ikishafikia hatua hiyo bado watakuja kuomba chakula cha msaada wa serikali jambo ambalo siyo zuri" amesema Malulu.
Kadhalika amewataka wakulima hao kuuza mazao kwa malengo yenye manufaa kwa familia, sambamba na kuendelea na kilimo cha mazao mengine kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo.
Katika hatua nyingine, Malulu amewataka madiwani hao kujenga umoja kati yao na watendaji wa kata na vijiji badala ya kuendekeza mivutano inayoweza kukwamisha utekelezaji wa maendeleo huku akiwasihi kutumia vikao halali kujadili na kutatua changamoto za watumishi wasiofaa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Leo Rushau,ametumia fursa hiyo kukipongeza CCM wilayani humo kwa kuendelea kusimamia vyema Ilani ya chama hicho katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na maendeleo yanayo kusudiwa na serikali.
Post a Comment