HAKIMU ARISTIDA : WANAWAKE HAKIKISHA MNAJUA MALI ZILIZOPATIKANA WAKATI WA NDOA
Na Dinna Maningo, Musoma
IMEELEZWA kuwa baadhi ya wanawake hupoteza haki ya kumiliki mali walizochuma wakati wa ndoa pindi wanapoachana au mme anapofariki, kutokana na baadhi ya wanaume kutowashirikisha wanawake na kuwa wasiri katika mali wanazozitafuta.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya ya Musoma, Aristida Tarimo amesema wanawake wana haki ya kujua mali walizochuma wakati wa ndoa na wana haki ya kumiliki mali.
Ameyasema hayo wakati akitoa mada juu ya mirathi na wosia katika kongamano la hivi karibuni lililoandaliwa na Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists ) mkoani Mara, lililofanyika Viwanja vya Mukendo Mjini Musoma.
" Wanawake wanapoteza haki zao kwasababu ya kutojua mali walizochuma kwenye ndoa, anafungua kesi inapofika kwenye suala la kugawa mali mwanamke anakuja anasema tuna viwanja vitatu ukimuuliza viko wapi na eneo gani hajui.
" Mwanaume anamficha mali anasema hii nyumba siyo yangu nimemjengea baba yangu mwisho wa siku mwanaume anaoa mke mwingine unashindwa kupata haki zako kwasababu umeshindwa kuthibitisha kile unachostahili kwasababu ya kutokuwepo kwa uwazi.
"Sasa mahakama itagawaje kiwanja ambacho hakijulikani kipo wapi, mwisho wa siku unajikuta unaambulia sifuri. Kwahiyo cha muhimu kila kinachopatikana jitahidi kujua mali zenu za ndoa kuwa ipo sehemu fulani na ushiriki wako uonekane."amesema Aristida.
Hakimu huyo amesema wanawake wana haki ya kumiliki mali hata kama walikuwa ni wamama wa nyumbani hivyo wanaume wasiwanyime haki ya kumiliki mali.
"Wanawake wanahaki ya kumiliki mali iwe shamba au nini, hata kama ulikuwa mama wa nyumbani unamchango mkubwa ulikuwa unafua nguo, unampikia hata kama hukuwa na kazi mahakama inatambua. Kwa kutojua haki hizo watu wanapoteza haki zao " amesema Hakimu huyo.
Amesema wanaume wengine wamekuwa na tabia ya kuwadhurumu wanawake mali kupitia ulaghai wa kuandikisha mali kwa majina ya Wanawake kisha kuziombea mikopo na kutokomea na fedha bila kurejesha mikopo.
"Kuna akina baba unakuta anataka kuchukua mkopo, anaenda kuchukua mkopo ile mali iliyoandikwa kwa jina lako, kwasababu amepata mwanamke mwingine hata mali ikiuzwa hana shida anajua mkopo fedha kaishachukua benki.
"Anakwenda ananunua nyumba kwa siri bila kukushirikisha anamjengea mwanamke mwingine mnaachana na nyumba ina deni huna pesa za kulipa mkopo, nyumba inapigwa mnada unakosa pakuishi, unamwambia kwamba andika jina langu kumbe mwenzio ana maslahi yake."amesema Aristida.
Amewasisitiza wanawake kuhakikisha wanazifahamu mali ikiwa ni pamoja na kuambatana na wenza wao kununua mali na sio kuwaacha wanaume kwenda kuzinunua peke yao.
"Nilichogundua akina mama wengi kwa kutojua au kwa makusudi kwa sababu tumekuwa na utamaduni kuwa wanaume wengi ndio watafutaji unakuta mwanaume anaondoka kwenda kununua uwanja peke yake.
"Saa zingine pesa umempa wewe ataenda atanunua uwanja ataweka jina lake, wakati mpo kwenye ndoa anaweza nunua vitu vingi hasemi, kwenye ndoa kuna siri nyingi, anaweza kuwa na mchepuko huko au anazongwa na ndugu akafanya mambo mengine kwa siri hakwambii.
"Ndiyo maana tunaambiwa tuishi na wanaume kwa akili ili hata akinunua kitu akwambie,mme au mke ana haki ya kumiliki mali kwa majina yao, mmenunua mali mkiwa kwenye ndoa mnaweza kuandika majina yenu kwa pamoja au jina moja"amesema Aristida.
Wajasiriamali akiwemo Agnes Warioba Marwa wamekipongeza kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake kwa kuungana nao katika kongamano.
Wamesema kupitia kongamano wamepata elimu katika maswala mbalimbali iliyotolewa na wawezeshaji kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi na kusema kuwa sasa wamepata ufahamu wa mambo mengi na yatawasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Katibu wa Kikundi hicho cha Wanawake wenye maono Ghati Msamba amesema wameamua kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo ili kupata maarifa yatakayowasaidia wanapokuwa kwenye shughuli za uzalishaji na katika familia zao.
Katibu wa Kikundi cha Wanawake wenye maono Ghati Msamba
Post a Comment