HEADER AD

HEADER AD

MSAJILI : MTOTO WA NJE YA NDOA ANAHAKI YA KURITHI MALI

Na Dinna Maningo, Musoma

BAADHI ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa hawezi kurithishwa mali ya baba aliyemzaa kwakuwa sio mtoto halali wa ndoa.

Hali hiyo imepelekea baadhi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa kutengwa na familia ya baba aliyemzaa lakini pia kukosa haki ya kumiliki mali jambo ambalo baadhi ya watoto wamejikuta wakiishi maisha magumu licha ya baba waliowazaa kumiliki mali.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Kanda ya Musoma, anayetekeleza majukumu yake ya kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma, Eugenia Gerald Rujwahuka amewatoa hofu wanawake waliozaa na wanaume walioko kwenye ndoa zao na kusema kuwa mtoto wa nje ya ndoa ana haki ya kutunzwa na kurithi mali za baba aliyemzaa.

       Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Kanda ya Musoma, anayetekeleza majukumu yake ya kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma, Eugenia Gerald Rujwahuka.

Eugenia amesema mtoto wa nje ya ndoa akiwa ametambuliwa na kufahamika kwa wanafamilia ana haki ya kurithishwa sehemu ya mali ya baba yake sawa na watoto waliozaliwa ndani ya ndoa.

Naibu Msajili huyo ameyasema hayo wakati akitoa mada juu ya Mirathi na Wosia katika kongamano lililoandaliwa na Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists ) mkoani Mara na kufanyika Viwanja vya Mukendo Mjini Musoma.

        Wajasiriamali wakisikiliza mada mbalimbali

Kongamano lililofanyika Machi, 04, 2023 lililowakutanisha waandishi wa habari wanawake, wajasiriamali wanawake pamoja na wadau kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi.

Mjasiriamali ambaye ni mwalimu mstaafu Doto Magera, wakati wa usasilishwaji wa mada hiyo aliuliza swali kutaka kufahamu je watoto waliozaliwa nje ya ndoa wana haki ya kurithishwa mali ambazo amechuma na mmewe ambaye ni mwanandoa halali?.

        Wajasiriamali na Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono wakiwa kwenye maandamano kusherekea siku ya Wanawake duniani

"Nawashukuru wawezeshaji wote akina mama tumejua mengi kupitia mada zenu hasa mambo ya sheria, akina mama tumewezeshwa na akina mama wenzetu tuache uoga tutasaidiwa na wanasheria wanawake wenzetu, nimepambana na mengi nashukuru wanasheria mmeniongezea vitu kichwani.

"Swali langu, kuna watoto wanaozaliwa nje ya ndoa mtoa mada umesema hao watoto watambulishwe mapema kwenye familia ili watambulike tuweze kuwafahamu kabla mzazi wa kiume hajafa, je huyo mtoto aliyetambulishwa ambaye yupo nje ya ndoa ana haki ya kupata mali niliyoichuma mimi na mme wangu?.

Naibu Msajili Eugenia akajibu " Mtoto wa nje ya ndoa anatambuliwa kwenye mirathi ana haki ya kurithi mali ya baba aliyemzaa, wewe mama kama hutaki kumpa mali zako mtoto atapata shea ya mme wako aliyemzaa.

"Mtoto wa nje ya ndoa akishafahamika kwenye familia nae ana haki kama wale watoto wako wa marehemu mmeo lazima arithi mali ya baba yake" amesema.

        Wajasiriamali wakisikiliza mada mbalimbali

Akizungumzia kuhusu watoto wa nje ya ndoa ambao marehemu baba zao walikufa wakiwa hawajawatambulisha katika familia amesema ;

"Watoto wa nje ya ndoa wanatambulika kwenye mirathi kama hakutambulishwa wakati wa uhai wa baba, huwa tunaomba vyeti vyao vya kuzaliwa tunaangalia majina yaliyoandikishwa, sio kwamba unaenda kubumbabumba vyeti vya kuzaliwa.

"Unasema huyo ni mtoto wa marehemu kisa umeona alikuwa na mali, na ikibidi tunaomba na kadi ya kliniki, kwahiyo wote wana haki sawa hata kama atakuwa amezaa nje ya ndoa watoto sita wote watapata mgao wa mali ya baba yao" amesema Eugenia.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists ) mkoani Mara, Jovina Massano amesema sababu ya kuwashirikisha wajasiriamali kwenye kongamano hilo ni kuwapa elimu ya ujasiriamali na maswala mbalimbali ya kijamii kupitia wawezeshaji mbalimbali.

        Mwenyekiti wa Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists ) mkoani Mara, Jovina Massano 

No comments