HEADER AD

HEADER AD

CCM YAELEZA SABABU YA MWENYEKITI WA KIJIJI KUSIMAMISHWA UONGOZI

Na Dinna Maningo, Butiama 

KIJIJI cha Magunga kata ya Mirwa wilaya ya Butiama mkoani Mara, kimekuwa na sintofahamu ya Wenyeviti wanaochaguliwa na wananchi kuongoza Serikali ya Kijiji kutomaliza muda wa miaka mitano ya uongozi.

Jambo hilo limeibua sura mpya katika Kijiji kwa kile kinachoelezwa ni hujuma za kiuongozi, ubinafsi, chuki na matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kijiji na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Magunga ni Kijiji ambacho kwa awamu tatu mfululizo za uongozi, wenyeviti watatu wamesimamishwa uongozi kabla ya kumaliza muda wa miaka mitano ya uongozi huku tuhuma zao zikiwa na utata zingine zikidaiwa ni chuki za madaraka.

          Senta ya Magunga

Wenyeviti watatu walisimamishwa uenyekiti na kutoendelea na uongozi na kisha nafasi zao kukaimishwa kwa wajumbe wa Serikali ya Kijiji ambapo chanzo ni kutofuatwa taatibu sahihi za uvuaji madaraka.

James Zabron kutoka Chama hicho alidumu kwa miaka mitatu na kusimamishwa uenyekiti kwa tuhuma za kuuza shamba la Kijiji ekali 65 na ofisi kukaimishwa Mwandika Omari aliyekuwa mjumbe wa Serikali ya Kijiji na kudumu nafasi hiyo hadi uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mwingine ni Togoro Juma kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyedumu kwa miaka miwili na kusimamishwa uongozi kwa tuhuma za kushindwa kusimamia upotevu wa Tsh Milioni 5.

Fedha hizo zilizotolewa Benk na aliyekuwa Mtendaji wa kijiji Simon Mgendi Magebo aliyedaiwa kughushi na kutoa fedha,na ofisi kukaimishwa uenyekiti kwa Rafael Kubira aliyedumu katika nafasi hiyo hadi uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Magige Mahera Msyomi (CCM) aliyesimamishwa Novemba, 2022 kwa tuhuma saba zikiwemo za kutosoma mapato na matumizi ambaye nafasi yake imekaimishwa kwa mjumbe wa halmashauri ya Kijiji  Daud Sarurya.

Unapopita maeneo mbalimbali ya kijiji hicho cha Magunga utakutana na minong'ono ya wananchi wakiulizana maswali kuhusu kusimamishwa uongozi Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Magunga Magige Mahera.

Kinachowaumiza vichwa ni pale Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Mwenyekiti CCM Kata ya Mirwa Moris Onyango Odhiambo na Katibu Patrick Roche Pius wa Kata hiyo kumsimamisha uongozi Mwenyekiti huyo huku wananchi wakiwa hawajui sababu za kusimamishwa uongozi.

Mbali na kutofahamu sababu za Mwenyekiti kusimamishwa uongozi, wanashangazwa kuona Chama cha Mapinduzi kupitia viongozi hao wa Chama kumkaimisha kimyakimya mjumbe nafasi ya ukaimu mwenyekiti wa Kijiji bila wananchi kupewa taarifa kupitia mkutano mkuu.

Inaelezwa kwamba pengine Mwenyekiti na Katibu wa CCM Kata wanatumia uzoefu wao wa kazi kuwadhoofisha kisiasa baadhi ya viongozi kutokana na kuongoza kwa miaka mingi nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama na Serikali ya kijiji hicho.

Habari zinasema kwamba Mwenyekiti huyo wa CCM Kata amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji kwa miaka 5, amekuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi miaka 10, na amekuwa Mwenyekiti wa CCM Kata kwa kipindi cha miaka 10 ambapo mwaka jana amechaguliwa tena kuhudumu nafasi hiyo.

Inaelezwa kuwa Katibu wa CCM Kata hiyo ya Mirwa amekuwa mjumbe wa serikali ya kijiji kwa miaka 20 na nafasi ya ukatibu wa Kata kwa miaka 10 huku akihudumu vyeo vyote hadi uchaguzi wa Chama wa 2022 ndiyo alijiondoa ujumbe serikari ya Kijiji na kubaki na cheo cha ukatibu.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho aliyesimamishwa uongozi nae anadai kuwa kusimamishwa kwake kunatokana na kufuatilia matumizi ya fedha za miradi na alipoonekana kuhoji viongozi wakamuundia njama ya kumkataa ili kulinda maslahi yao katika Kijiji hicho.

        Magige Mahera Msyomi (CCM)

Baadhi ya wajumbe wakiwemo Wenyeviti wa Vitongoji nao wanasema kwamba viongozi wa CCM Kata ndiyo tatizo pamoja na Diwani wa Kata hiyo Willy Brouwn.

Inaelezwa  kwamba viongozi hao wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya na kufanya njama kwa baadhi ya viongozi kwa kutumia fedha kushawishi wajumbe ili kuwakataa kisha kuwasimamisha uongozi bila kujadiliwa kwenye vikao halali kitendo ambacho ni uonevu.

Viongozi wengine wa Serikali wanalalamika kuona posho ambazo ni fedha za miradi ya Serikali ya Kijiji hicho zikitumika kulipa posho vikao vya CCM ambapo viongozi hao uishinikiza Serikali ya Kijiji kuwalipa posho kwa kile wanachoeleza kwamba Serikali ni ya CCM ndiyo baba hivyo lolote watakalosema lazima litekelezwe.

Mwenyekiti CCM afunguka  

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mirwa Moris Onyango Odhiambo anakanusha tuhuma zinazoelekezwa kwao na kusema kuwa huo ni uongo unaoenezwa na Mwenyekiti wa Kijiji aliyesimamishwa uongozi.

        Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mirwa Moris Onyango Odhiambo

Anasema Viongozi wa Chama hawajatumia vibaya madaraka na hawana mmlaka kuiagiza serikali ya kijiji kulipa posho vikao vya CCM na kwamba kazi yao kama Viongozi wa CCM ni kusimamia utekelezaji wa Ilani.

" Tatizo la Mwenyekiti ni mtu muongomuongo, CCM Tawi la Magunga waliandika barua ya kumkataa, CCM Kata ikamjadili na ikaona ana makosa ikamsimamisha uenyekiti, tukapeleka malalamiko uongozi wa CCM Wilaya na huko Wilaya bado sijapata taarifa.

"Tuna mhitasari kwa Katibu kuna pesa alichukua kwa mwananchi, akachukua pesa ya matofari ya vijana, anasema ule uwanja ambao vijana wanautumia kucheza mpira ni wa Serikali ya Kijiji, ule uwanja ni wa CCM alete ushahidi"Anasema Moris.

Mwenyekiti wa Chama anaongeza " Viongozi wa CCM wanawezaje kulipwa posho fedha za Serikali huo ni uongo, sisi tunafuata maadili ya Chama, wao wanapokea fedha wanashindwa kuzisimamia sisi tufanyeje?kama kuna vitu anaona hatujamtendea haki aende ngazi za juu za uongozi.

Akizungumzia changamoto ya kukwama kwa miradi ya maendeleo anasema kuwa anayekwamisha ni Mwenyekiti huyo wa kijiji kwa kile anachoeleza kwamba tangu aingie madarakani hajawahi kuwasomea wananchi mapato na matumizi.

"Ile Choo ya mnadani yeye ndiyo kaikwamisha amejenga banda la biashara akaambiwa atoe ili choo kijengwe lakini amekataa, wanasema sisi tuna matumizi mabaya ya madaraka hayo ni mawazo yao, amekwambia kuwa amesimamishwa kwa makosa gani? kamuulize akwambie.

"Sisi kazi yetu ni kusimamia ilani itekelezwe tunaposimamia wao wanaona tunatumia vibaya madaraka, muulize fedha alizomchangisha mwananchi alipeleka wapi? na matofari 500 ya vijana kwa ajili ya ujenzi alipeleka wapi" anasema Moris.

Kuhusu swala la kuwa madarakani kwa muda mrefu amesema hiyo siyo sababu kwani yeye ni mzoefu katika uongozi hivyo si kweli kwamba anatumia madaraka yake vibaya kwakuwa ameongoza kwa miaka kadha.

"Mimi nimeongoza kwa miaka mingi nimekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji miaka mitano, nimekuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi miaka 10 na sasa Mungu akinijalia uhai na nikamaliza kipindi cha uongozi nitakuwa nimekamilisha miaka 15 nafasi hii ya uenyekiti Kata" anasema Moris.

Katibu wa CCM akataa kuzungumza

Mwandishiwa DIMAOnline akamtafuta Katibu wa CCM kata ya Mirwa,Patrick Roche Pius ili kueleza tuhuma zinazoelekezwa kwakwe na Chama hali inayosababisha chama kuingia doa lakini alikataa kuzungumza zaidi ya kuzungumzia tu suala la machinjiyo anayomiliki.

     Katibu wa CCM kata ya Mirwa, Patrick Roche Pius

"Mwenyekiti wa Kijiji aliyesimamishwa uongozi anasema kwamba machinjio ipo kwenye eneo la kijiji sio kweli ipo eneo la mgodi na ushuru nalipa vizuri mpaka wa mgodi na kijiji unajulikana.

Kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, na vikao vya CCM kujilipa posho fedha za miradi anasema" unauliza maswali magumu nashindwa hata nijibuje kwakweli ninaumwa siwezi kuzungumza ningekuwa siumwi tungezungumza". anasema Katibu huyo.

Kiongozi huyo alikataa katakata kuzungumza. Mwandishi akawasiliana na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Magunga  Victor Wambura kufahamu iwapo walimjadili Mwenyekiti wa Kijiji kwa tuhuma mbalimbali.

Anasema" Mgogoro wa Mwenyekiti wa Kijiji ulianzia kwenye tawi akajadiliwa kwenye vikao ikaenda CCM Kata hadi Wilaya, alishindwa kuheshimu Chama, kusimamia Ilani ya Chama, tunapotoa maelekezo kama kusoma mapato na matumizi hatekelezi.

"Tuhuma zake zilikuwa nyingi na mihitasari ya vikao yote ipo, tulikuwa tunamuita kwenye vikao hafiki, ofisi ya Kijiji bendera ya Taifa haipandishwi. Tangu achaguliwe 2019 zipo tuhuma nyingi zilizopelekea asimamishwe uenyekiti Novemba, 2022.

Anaongeza" Sisi hatuna mamlaka ya kumsimamisha uongozi, sisi tunapeleka mapendekezo ngazi za juu wao wanachukua hatua, nitakutumia mihitasari ya vikao tulivyomjadili ili ujue kuwa hakuonewa" Anasema Victor.

Mwandishi wa habari akamuuliza Mwenyekiti huyo wa Tawi kuhusu malalamiko ya wajumbe wa Serikali ya Kijiji wanaodai kusimamishwa uongozi bila kujadiliwa wala kupewa barua ya kusimamishwa kazi.

"Wajumbe tuliwajadili tukapeleka malalamiko kwenye Chama Kata wakasimamishwa, kuna mjumbe alipewa kukusanya fedha akawa hawasilishi zote, wajumbe wengine wana kadi mbili ya CCM na CHADEMA, Chama kimechukua hatua" anasema Mwenyekiti huyo wa Tawi.

Mwandishi akamuuliza iwapo yeye amekwisha shuhudia kuona kama wajumbe hao wana kadi mbili lakini hakuthibitisha na badala yake akasema wapo waliofuatilia na kubaini wajumbe hao kuwa na kadi mbili za uanachama.

Licha ya Katibu huyo kuahidi kumpatia Mwandishi wa habari mihitasari ya vikao vilivyomjadili Mwenyekiti huyo ili ajiridhishe hakuweza kumpatia yapata siku saba sasa tangua alipoahidi kutoa.

DIMA Online yadaka barua ya kusimamishwa Mwenyekiti wa Kijiji

Mwandishi wa chombo hiki cha habari akafanikiwa kupata barua ya malalamiko ya  CCM Kata kwenda CCM wilaya na walivyomsimamisha uongozi iliyoambatana na makosa saba ya Mwenyekiti wa Kijiji.

Octoba, 31, 2022 Chama cha CCM ngazi ya Kata kiliandika barua kwenda kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Butiama ikieleza kero ya Serikali ya Kijiji cha Magunga kutotendea wananchi haki.

Barua hiyo inaekeza kuwa Chama hicho tarehe hiyo walikuwa na kikao cha Chama na viongozi wa Serikali, ajenda kuu ilikuwa Ilani ya utekelezaji ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi ya 1977, ndipo wajumbe walipouliza ni kwanini Serikali ya Magunga haisomi mapato na matumizi ?inaeleza barua.

Barua inaeleza " Mbona Mirwa wanatekeleza Ilani hiyo, kila tunapokaa Chama tunaagiza lakini utekelezaji haupo, pia halmashauri ya Wilaya imeleta mradi wa choo hata ujenzi umeshindikana .

"Ndipo wajumbe wakasema shida ya Halmashauri hiyo ni Mwenyekiti aitwae Magige Mahera kutokutekeleza majukumu na kusababisha hasara Kama vile;

Kutosoma mapato na matumizi, kukwamisha ujenzi wa choo, kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari, kuchukua mali za Chama matofali 500 na mawe Mali ya umoja wa vijana na kupeleka nyumbani kwake pasipo ridhaa ya Jumuiya hiyo" burua imeeleza.

Hasara nyingine ni " Kuchukua fedha ya mwananchi ya maji Tsh.367,000 bila stakabadhi ya Kijiji na kufanyia shughuli zake, Magige Mahera kufyngwa kwa kesi ya jinai Na. 6/2020 ZANAKI na kukatalia kwenye eneo la Serikali (Daire) na kufanya makazi" Barua imeeleza.

Kwa kupitia mambo hayo yote kikao kimeridhia kuwa Mwenyekiti wa Kijiji na wajumbe hawastahili kuwa viongozi maana vipengele hivyo vimewagusa wote, kikao kinashauri watu hawa wamedhaminiwa na Chama cha Mapinduzi na sisi kikao tumekubaliana wavuliwe dhamana ya chama kwa kusoma ibara ya 18 mstari 1 hadi 3.

Barua imeeleza kuwa "Kupitia kikao hiki tunataarifu Chama wilaya kama kuna ushauri watoe, pamoja na hayo hii ni mara ya pili kufutiwa dhamana.
Kwa maelekezo ya kikao ofisi ya Kijiji cha Magunga imekabidhiwa Mtendaji wa Kijiji na Wenyeviti wa Vitongoji kushikilia mpaka ushauri utakapotoka juu.

Barua hiyo ilisainiwa na Katibu wa CCM Kata na kugongwa mhuri wa Chama na Nakala ya Taarifa Kwenda kwa DC Butiama, DED Butiama, OCD Butiama, OCS Buhemba, Diwani Mirwa, Weo Mirwa, Veo Magunga-Simamia maelekezo, Ofisi ya CCM Tawi, Mwenyekiti na Serikali yako -Maagizo.

Barua hiyo iliambatana na nakala ya maelezo ya Ezekiel Samson kulipa Tsh. 300,000 za uharibifu wa miundombinu wa mradi wa maji alizokabidhi mbele ya Mwenyekiti wa Kijiji Magige Mahera ikiwa na mhuri wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji tarehe 17,12,2019.

Je Mwenyekiti wa Kijiji Magige Mahera anasemaje juu ya Chama kumsimamisha uongozi ?  Endelea kufuatilia DIMA Online.


No comments