DED BUTIAMA ADAIWA KUTUMIA VIBAYA MADARAKA KATIKA TEUZI
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Patricia Kabaka amedaiwa kutumia vibaya madaraka kwa kuvunja sheria na kanuni za utumishi wa umma kwa kufanya teuzi kwa maslahi binafsi bila kushirikisha mamlaka za uteuzi.
Habari zinasema kwamba Mkurugenzi Patricia Kabaka mwezi Septemba,04, 2022 alimteua Lomitu P.L. Lilayon ambaye ni afisa Mifugo Daraja la II kushikilia ofisi ya Maliasili na Mazingira kwa muda kama mkuu wa idara baada ya aliyekuwa mkuu wa idara hiyo Kustaafu.
Mkurugenzi huyo alimteua mtumishi kutoka idara nyingine kushikilia ofisi ya Maliasili na Mazingira hilihali ofisi hiyo kuna mtumishi ambaye ni afisa wanyamapori ambaye angeweza kuangalia ofisi wakati taratibu zingine zikifuatwa.
Habari zinasema uteuzi huo haukufuata sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2009 na kanuni za utumishi wa umma ambapo kanuni za uteuzi kuziba nafasi katika nyadhifa za ukuu wa idara, Taasisi n.k katika utumishi wa umma zinahitaji kupata kibali kwa Katibu Kiongozi, au Katibu mkuu utumishi kwa ajili ya kujaza, kuziba pengo lililo wazi.
Pia mtumishi lazima awe na sifa stahiki kuhusu elimu, taaluma, cheo cha muundo na upekuzi hufanyika kuona iwapo ana kidhi vigezo vya kusimamia nafasi husika.
Inaelezwa kwamba mtumishi anayetakiwa kuhudumu katika nafasi hiyo anaweza kuombwa pia kutoka kwa Katibu Tawala mkoa (RAS) na pia anaweza kuazimwa toka mamlaka zingine, taasisi zingine ilimradi sheria na kanuni zimelindwa.
Habari zinasema Mkurugenzi kafanya uteuzi bila kibali kwani kibali ili kitoke kuna maandalizi, na akiandika barua ya uteuzi kama Kaimu na ananukuu barua ya kibali.
Inaelezwa kwamba hatua za uteuzi huwa zinapita kwenye vikao hasa Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango na kwamba kibali hutolewa kwa mtu aliyebadilishwa muundo ili afanye kazi hiyo kulingana na kiwango cha taaluma na hairuhusiwi kutoa mtumishi nje ya idara husika.
Mwandishi wa DIMA Online amewasiliana na Mkurugenzi huyo wa halmashauri kumzungumzia suala hilo la teuzi ambalo limekuwa sintofahamu ambapo amesema hajatumia vibaya madaraka.
"Mi nina mamlaka kwa utaratibu wa ndani kumkaimisha mtumishi ila kama anatakiwa kuwa confirmed (kuthibitishwa) ndio kinaombwa kibali kwa mamlaka ulizosema.
"Na mtumishi niliyemkaimisha ana sifa zote za kushika idara hiyo usisikilize uzushi mwandishi tunafanya kazi kulingana na taratibu hakuna matumizi mabaya ya madaraka hapo" amesema Mkurugenzi Patricia.
Post a Comment