HEADER AD

HEADER AD

JOYCE SOKOMBI AWAFUNDA WAJASIRIAMALI MBINU ZA KUKUZA BIASHARA ZAO


>>>Asema kabla ya kufanya biashara fanya tafiti

>>>Atahadharisha fedha za mikopo

>>>Aahidi ushirikiano na Wajasiriamali walioshiriki kongamano la Waandishi wa Habari


Na Dinna Maningo, Musoma

MFANYABIASHARA anayefanya biashara zake nje ya nchi Joyce Sokombi, amesema kuwa baadhi ya Wanawake wamekuwa wakifanya biashara kwa muda mrefu bila mafanikio kwakuwa huifanya kwa mazoea jambo ambalo limesababisha washindwe kuyafikia malengo yao.

Amesema wajasiriamali wengine wamekuwa na mikopo ya fedha isiyonufaisha biashara zao kutokana na kukopa fedha nyingi ikilinganishwa na vipato vyao na hivyo kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati na kujikuta mali zao zikipigwa mnada.

Joyce ameyasema hayo hivi karibuni Machi, 04, 2023 Katika kongamano lililoandaliwa na Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists ) mkoani Mara kuelekea siku ya Wanawake duniani inayofanyika Machi, 08  ya kila mwaka.

Kikundi hicho cha Waandishi wa habari wanawake wenye maono kimetoa elimu kwa wajasiriamali wanawake kupitia wawezeshaji kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi lililofanyika viwanja vya Mukendo mjini Musoma.

       Mfanyabiashara Joyce Sokombi akizungumza kwenye Kongamano la Waandishi wa habari Wanawake mjini Musoma.

"Tusifanye biashara kwa mazoea kwamba mama fulani kafanya biashara ya kuuza dagaa ngoja na mimi nikachukue niuze dagaa bila kufanya tafiti kujua faida na hasara ya kuuza hao dagaa.

Amesema baadhi ya wanawake wanakopa fedha kufanya biashara bila kuwa na malengo na hivyo kujikuta wakishindwa kurejesha mikopo na wakati mwingine kukatika mitaji licha ya kukopa fedha kuendesha biashara zao.

           Wajasiriamali wakiwa kwenye kongamano

"Kuna wengine wanakimbilia kukopa, unapokwenda kukopa kuna mawili lazima uangalie faida na hasara ya kukopa, kuna wanawake wapo kwenye vikundi tunaita Vicoba hatukatai kuwa kwenye Vikoba lakini navyo unatakiwa uangalie kama una uwezo wa kuchanga fedha.

" Unawekesha elfu 20 au elfu 50 kila wiki jiangalie je nina uwezo wakutoa hii pesa kila wiki? usije ukawalaumu watu wengine ukashindwa kutoa pesa kwa wakati au unaanza kupiga simu kwa mama Yohana niazime kiasi fulani nipeleke marejesho mama Yohana anakupa.

"Wiki inayofuata utaomba pesa kwa mama Yuni naye atakupa wiki inayofuata mwishowe wewe mwenyewe unaona aibu, tunaingia kwenye hali ya uombaji pasipo kuelewa na yote hii inatokana na kutopata elimu."amesema Joyce.

Amesema kuwa wajasiriamali wengi hawana elimu ya namna ya kutunza mapato na matumizi ambapo aliwaahidi kuwa siku zijazo atawapatia elimu hiyo.

           Wajasiriamali wakisherekea kongamano pamoja na Janeth Peter Mafipa afisa maendeleo ya jamii msaidizi Kata ya  Mukendo. 

"Elimu ya ujasiriamali ingetolewa mara kwa mara namna ya kutunza mapato na matumizi tungekuwa tulishavuka kwenye ujasiriamali tungekuwa ni wafanyabiashara wa kati na wakubwa .

"Kwani hao wanaoendesha magari wana nini na sisi tumekosa nini? wanawake wanaosomesha watoto bila kutegemea wao wana nini na sisi tuna nini,ndugu zangu nina waahidi nitakuja kutoa hii elimu ya ujasiriamali namna ya kufanya biashara ikakupa faida "amesema Joyce.

Amesema kuwa wapo baadhi ya wanawake wamefanya biashara miaka mingi lakini bado biashara zao hazikui kufikia hatua ya kuwa wafanyabiashara wa kati au wakubwa.



"Mwanamke umefanya kazi ya ujasiriamali miaka 10 lakini matokeo hujayaona, tunafanya kazi kwa kupiga makitaimu yaani leo kunakucha unaona bora ya jana ni kwasababu gani?tunatakiwa tujiulize.

" Kwanini uwe tu mjasiriamali mdogo? kuna ujasiriamali wa kati na mkubwa ni lazima tutoke kwenye hii nafasi ya Wajasiriamali wadogowadogo, tutafundishana na tutashikana mikono na tutapiga hatua, nitahakikisha naona akina mama hawa mmefikia wapi" amesmea.

Pia amewashauri wanawake kutokata tamaa na kuvunjika moyo kwani biashara zipo nyingi huku akisisitiza kwa wale wanaoanza kufanya biashara waanze na biashara yenye mtaji mdogo.

        Wajasiriamali na Waandishi wa habari Wanawake wakiwa katika maandamano wakisherekea kuelekea siku ya Wanawake duniani

"Kuna vikundi vimefanya mambo makubwa tusikate tamaa kwasababu unaweza kuanzisha biashara ya mchicha mtu anaanza kusema eti fulani anauza mchicha na wewe ukishasikia hivyo unakata tamaa.

"Unatoka kwenye biashara ya kuuza mchicha unaenda kwenye biashara ya kuuza mchele kufuata Mbeya wakati uwezo huna matokeo yake mtaji unakatika,mwanamke simama kwenye nafasi yako kama mwanamke ambaye umeamua kufanya biashara kwa hiari yako na usimame kwenye biashara moja.

Mfanyabiashara huyo amewasisitiza wanawake wajasiriamali kumshirikisha Mungu katika maombi ili abariki biashara zao.



"Kila mtu hapa ana dhehebu lake na dini yake,kabla ya kuanza kufanya chochote tumuombe Mungu, hakuna kitu ambacho tunaweza kufanya bila kumshirikisha Mungu lazima tumshirikishe.

"Mwambie Mungu nataka kufungua biashara ya kuuza mchele hivi pesa nitatoa wapi? nahitaji mtaji wa Milioni 5 na mimi uwezo wangu ni Milioni moja hii Milioni 4 naitoa wapi? Mungu atakupa njia kupitia umoja wako au kikundi chako utakopa pesa na peza za kulipa zitapatikana ilimradi uwe mwaminifu kurejesha pesa ulizokopeshwa"amesema Joyce.

" Tunataka kufanya kitu kupitia hawa wanawake ili uwe mfano kwa wanawake wengine,umepata hasara mara ya kwanza songa mbele usikate tamaa, umepata hasara mara ya pili angalia nimekwama wapi nimechemka wapi mara ya kwanza kisha songa mbele hatimaye utafikia lengo lako ulilokusudia" amesisitiza.

Amewaomba wanawake kutochukiana kwani adui wa mwanamke ni mwanamke mwenzake na kwamba yupo tayari kuwaonesha mwanga wajasiriamali hao na akawaomba kusajili vikundi ili washirikiane kuhakikisha wanakuza biashara zao.

"Adui wa mwanamke ni sisi wenyewe tunafanyiana chuki kwa wanawake wenzetu, tupunguze midomo, tukipunguza midomo tutasonga mbele, hii biashara ya kubebe dishi kichwani unatembeza dagaa iwe kazi ya ziada umeifanya miaka 10 kabla saizi tusonge mbele.

"Mimi nafanya biashara za nje ya nchi napeleka Nyanya chungu, Hoho na Matango pori, nimewahi kuwa mbunge miaka mitano hivi ningekuwa sina biashara ningekuwa hivi? kupitia mimi akina mama mtakuwa kama mimi, mimi Joyce nimeweza hata ninyi mtaweza, kikubwa msikate tamaa na msirudishane nyuma, jisimamie mwenyewe na muwe waaminifu katika biashara zenu"amesema.

Joyce  Sokombi amewasisitiza wajasiriamali kuheshimu pesa na kuwa na nidhamu ya pesa lakini pia ameziomba Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi kuwawezesha Wajasiriamali katika shughuli zao mbalimbali ili kukuza mitaji yao.

Wajasiriamali walioshiriki kongamano hilo wamewapongeza Waandi wa habari Wanawake kwa kuwashirikisha na kuketi pamoja nao huku wakizipongeza Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi zilizowapa elimu kupitia mada mbalimbali.

       Mjasiriamali Winfrida Johnson

"Kwakweli hili ni tukio la kwanza sisi Wajasiriamali wanawake kualikwa kwenye Kongamano la Waandishi wa habari kusherekea siku ya wanawake Duniani.

"Hii fursa hatukuwahi kuipata hata kwenye makongamano mengine, sisi kama wajasiriamali huwa hatushirikishwi kwenye maadhimisho ya siku ya mwanamke lakini nyie mmetukumbuka tunawashukuru sana.

"Mafunzo haya tuliyopata yametujenga sana, tumefahamu mambo mengi kama masuala ya kifedha na mikopo, mifuko ya afya ya jamii, namna ya kukuza biashara yako, haki katika kazi na ajira, masuala ya ndoa na mirathi. 

Ameongeza "Kwakweli tumepata nondo za nguvu, tunaomba isiwe mwisho mwendelee kutupatia elimu" amesema Winfrida Johnson.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists), Jovina Massano amesema kuwa Kikundi hicho kimeamua kufanya kongamano la wanawake na kuwashirikisha wajasiriamali wanawake kwakuwa ni kundi ambalo ni muhimu kuelimishwa katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
 Mwenyekiti wa Kikundi cha Waandishi wa Habari Wanawake wenye maono (Visionary Women Journalists), Jovina Massano akizungumza

Amesema miongoni mwa malengo ya kikundi hicho ni kuwakutanisha Wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali na kupatiwa elimu ya ujasiriamali kupitia wawezeshaji mbalimbali ili kumkomboa mwanake mjasiriamali katika kujiinua kiuchumi.

Ameongeza kuwa lengo lingine la kikundi ni Waandishi wa habari Wanawake kusaidiana katika shida na raha pamoja na kuchangishana fedha na kukopeshana ili kujikwamua kiuchumi na kuanzisha miradi mbalimbali itakayowainua kiuchumi badala ya kutegemea kazi ya uandishi wa habari pekee.

"Tunataka kuwa wanawake wenye maono kwelikweli, Waandishi wa Habari katika kikundi chetu watajitahidi kiripoti habari mbalimbali ndani ya jamii.

Miongoni mwa habari ni pamoja na kuibua ili kumwezesha mwanachi kupata habari ikiwa ni pamoja na kuandika habari za Wajasiriamali wanawake kama njia ya kutangaza biashara zao pamoja na wadau wengine.

         Waandishi wa Habari Wanawake wakiwa katika picha ya pamoja na wageni waaalikwa

Baadhi ya watoa mada waliotoa mada mbalimbali wakati wa kongamano






No comments