MAKUMBUSHO YA TAIFA, UNESCO WAKUTANA KUJADILI UREJESHWAJI MIKUSANYO
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia kwa viongozi wake Waandamizi akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Lwoga na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya UNESCO Tanzania Prof. Hamis Masanja Malebo, wamekutana kwa ajili ya kujadili masuala ya urejeshwaji wa mikusanyo iliyochukuliwa na kupelekwa nchi za nje wakati wa ukoloni wa Waingereza na Wajerumani.
Viongozi hao wamekutana Machi, 06, 2023, kukutana huko, kunafuatia Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwa tayari imeunda kamati ya kuandaa mchakato wa urejeshwaji wa mikusanyo hiyo kutoka nchi hizo za Bara la Ulaya.
Mbali na Mkurugenzi Mkuu Dkt.Lwoga na Prof Malebo, wengine walioshiriki katika mkutano huo, ni pamoja na Dkt. Amandus Kwekason na Mhifadhi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa na Kamishna wa Haki za Binadamu ambaye pia ni Mwanasheria wa Kamisheni ya UNESCO Tanzania, Bi Caroline Mchome.
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (MB) wakati wa kufunga kilele cha Tamasha la kumbukizi la Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni lilillofanyika Mjini Songea Mkoani Ruvuma, aliweza zungumzia ombi la kurejeshwa kwa fuvu.
Fuvu hilo ni la Songea Mbano aliyekuwa mmojawapo wa Mashujaa wa Vita vya Majimaji lililochukuliwa na Wajerumani, ambapo alisema tayari Kamati ya kitaalam ya kuratibu zoezi hilo limeanza ikiwemo kubainisha malikale zote za Tanzania zilizopo nje ya nchi kwa ajili ya kuzirejesha hapa nchini.
Post a Comment