WAFANYABIASHA WATAKA MAAGIZO YA RAIS SAMIA YATEKELEZWE
>>> Ni kuhusu utitiri wa ushuru na tozo
>>>Wasema Rais Samia alipokuwa Kagera aliagiza kero za wafanyabiashara zitatuliwe lakini bado.
>>>Wasema utitiri wa ushuru na tozo unawatesa wafanyabiashara.
Na Alodia Babara, Bukoba
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoa wa Kagera (JWT), Nicholaus Basimaki amesema Serikali itoe ushirikianao kwa wafanyabiashara ili kuondoa kero za ushuru na tozo mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara mkoani humo na kusababisha kufungiwa biashara zao.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Machi 06, 2023 amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea mkoani Kagera mwaka jana walitoa kero zao mbalimbali kwake ikiwemo kero ya utitiri wa ushuru na tozo kwa wafanyabiashara.
Nicholaus amesema kuwa Rais Samia aliagiza kero zao zitatuliwe na kwamba zipo zilizotatuliwa na zipo ambazo bado hazijatatuliwa ikiwemo kero ya utitiri wa ushuru na tozo.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Kagera Nicholaus Basimaki akiongea na waandishi wa habari kuhusu kero na changamoto zinazowakumba wafanyabiashara mkoani humo.
“Tozo na ushuru mbalimbali ni pamoja na kulipia stoo, leseni, kulipia Osha ( usalama mahali pa kazi), kodi ya mapato, ushuru wa taka, gharama za ukaguzi, kodi ya ongezeko la thamani (VAT), maegesho, mlinzi, vibari vya afya, vilevile huyo mfanyabiashara ataugua ataenda hospitali.
"Sasa sisi tunasema huyo ni mfanyabiashara gani anakifua gani kinachoweza kuhimili vitu vyote hivyo, kwa hiyo tunasema hivi watengeneze kapu moja ya tozo na ushuru wao wenyewe waende wagawane huko, hivi wamekaa na nani kupitisha hizo tozo na ushuru mbalimbali” Amesema Mwenyekiti.
Ametaja kero nyingine kuwa ni kuundwa kwa kikosi kazi katika manispaa ya Bukoba kilichokuwa kinapita kwa wafanyabiashara bila kushirikisha sekta binafsi na kuanza kufunga maduka na vibanda vya watu.
"Wakawataka hata wajasiliamali wadogo kwenda TRA kukadiliwa ili walipie leseni na baadhi yao walikuwa na vibanda vya mama ntilie, nyanya, mchicha"Amesema.
Naye Meya wa Manispaa ya Bukoba Godson Gybson amesema kuwa, Manispaa walikubaliana ukawekwa utaratibu mzuri kwa wajasiliamali wadogo ambao hawapaswi kulipa leseni kutokana na kipato chao kuwa kidogo.
Ameongeza kuwa wajasiriamali wao wanatakiwa kulipa Tsh. 30,000 manispaa ambapo elfu 20,000 ni ya kitambulisho na elfu 10,000 ushuru wa huduma (Service Charge).
“Baada ya kukaa manispaa tuliona kuwa hawa ambao walikuwa na vitambulisho vya wajasiliamali wafike halmashauri wakiwa na vitu vifuatavyo ,atambulishwe na ofisa mtendaji wa kata au wa mtaa mahali anapofanyia biashara kwamba huyu ni mfanyabiashara mdogo katika kata husika na wanamtambulisha kwa Mkurugenzi.
" Baada ya kupata barua ya mtendaji wa Kata au wa Mtaa anakuja moja kwa moja manispaa ya Bukoba anakutana na ofisa biashara ambaye atamuhoji na kumpa control namba anaenda kulipia benki sh. 20,000 ambayo ni thamani ya kitambulisho na analipia sh 10,000 ya ushuru wa huduma ofisa biashara anamgongea muhuri kwenye slip na ile ndiyo inakuwa leseni yake” Amesema Meya Gybson.
Mmoja wa wafanyabiashara ambaye anauza nyanya na vitunguu katika mtaa wa Kasalani kata ya Bakoba Merina Thadeo amesema kuwa baada ya kufungiwa kibanda chake na kuhofia bidhaa zake kuoza alilipia leseni sh 50,000 manispaa ya Bukoba baada ya kwenda TRA na kurudishwa manispaa.
Post a Comment