UJENZI WA DARAJA WAONDOA KERO KWA WANAFUNZI
Na Dinna Maningo, Tarime
WANAFUNZI wanaosoma katika shule ya msingi Gamasara, Kata ya Nyandoto wilaya ya Tarime mkoani Mara, wameishukuru Serikali kwa kujenga Daraja mto Kigera.
Wamesema msimu wa mvua walilazimika kuomba msaada wa kuvushwa mto huku baadhi yao wakikaa utoro kutokana na mto kujaa maji na kusababisha washindwe kuvuka kwenda shule.
Ferista Kisabo mwanafunzi wa darasa la pili amesema kabla ya daraja kujengwa walilazimika kuvua viatu vya shule na kuingia ndani ya maji kuvuka mto.
Wanafunzi wa shule ya msingi Gamasara
"Namshukuru Rais Samia kwa kutujengea daraja, wakati wa mvua tulikaa utoro mto ulijaa maji tukashindwa kuvuka, mvua ikiisha tunasubiri mpaka maji yapungue ndiyo tuvuke, tulichelewa kwenda shule "amesema Ferista.
Neema Ghati amesema kabla ya kujengwa daraja hilo jipya mvua iliponyesha maji yalijaa na kuwapa tabu kuvuka hivyo walizazimika kuomba msaada wa kuvushwa na watu wanaoishi jirani na mto huo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Nyakihenene Thomas Jovinalis amesema kuwa kabla ya daraja hilo wananchi na wanafunzi walijawa hofu kuvuka mto wakihofia usalama wao lakini sasa kero hiyo imekwisha.
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini, Mhandisi Charles Marwa amesema ujenzi wa daraja hilo umegharimu Tsh. Milioni 37.
Post a Comment