HEADER AD

HEADER AD

MAONESHO YA BIASHARA NI KIVUTIO CHA UTALII

Na Dinna Maningo, Mara

IMEELEZWA kuwa maonesho ya biashara ni kivutio cha Utalii kinachochangia kukuza pato la uchumi pindi bidhaa za wafanyabiashara na wajasiriamali wanapozionesha na kuzitangaza kwenye makongamano mbalimbali ya kitalii.

Pia maonesho ya bidhaa yanasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali kuongeza mtandao wa kibiashara baina yao na wafanyabiashara wa mataifa mbalimbali.

DIMA Online imefanya mahojiano na baadhi ya viongozi wa Kampuni binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition yenye makao yake makuu mkoani Arusha nchini Tanzania.


Kampuni hiyo inatarajia kufanya uhamasishaji wa Utalii wa mkoa wa Mara, Mei, 22-28, 2023 mjini Musoma ambapo Mwandishi wa Habari hii alitaka kufahamu umuhimu wa maonesho ya biashara katika kuinua uchumi wa mkoa wa Mara hususani sekta ya utalii.

Je Utalii wa maonesho ya biashara ni nini?. Afisa Masoko Kampuni ya Utalii Awesome Expedition, Daines Yahya Hemed amesema " Utalii wa maonyesho ya biashara, ni maonyesho ya bidhaa ambazo huwa ni kivutio kwa watalii.

      Afisa Masoko Kampuni ya Utalii Awesome Expedition, Daines Yahya Hemed

"Mfano maonyesho ya vitu vya asili Kama vikapu, mikeka, vyungu, mavazi ya asili, dawa za asili, vyakula, mazao, mifugo. Kutangaza utalii wa Tanzania na vivutio vilivyopo mkoani Mara, Maliasili kama ziwa Victoria, bidhaa za burudani kutoka mkoa wa mara, bidhaa zinazotumiwa hotelini na vitu vya kumbukumbu" amesema Daines.

Je ni kwa vipi maonesho na mkutano wa kutangaza vivutio vya Utalii mkoa wa Mara yatachochea watu wakiwemo wa kutoka nje ya nchi kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo hifadhi ya Serengeti?


 Afisa huyo wa Masoko ameeleza "Matokeo ya kongamano hili itapelekea kupata manufaa yafuatayo; Kuiunga mkono Serikali yetu katika kutangaza utalii, kuendelea kuitangaza nchi yetu kimataifa, kuchangamsha mwili, kujenga afya bora na kupunguza magonjwa yasiyo ya lazima.

"Kongamano litaongeza idadi ya watalii nchini Tanzania, tukio hili litaongeza mapato kwa serikali pamoja na jamii, kufungua fursa za ajira, biashara na fursa mbalimbali za utalii na zisizo za utalii Tanzania, kuongeza fursa za uwekezaji wa biashara miongoni mwa fursa zilizopo nchini Tanzania na
kuitangaza Tanzania na vivutio vyake mbalimbali"ameeleza Daines.

Je ni kwa namna gani maonesho ya bidhaa za Wafanyabiashara na wajasiriamali ni muhimu katika uhamasishaji wa Utalii mkoa wa Mara?.

Meneja Maendeleo ya Biashara Kampuni hiyo, Baraka Mohammed Abdallah amesema" "Maonesho ya bidhaa yanasaidia Mawakala wa utalii wa mkoa wa Mara kuweza kufikia masoko makubwa duniani bila kutumia gharama.

   Meneja Maendeleo ya Biashara Kampuni ya Utalii ya Awesome Expedition, Baraka Mohammed Abdallah

 "Bodi ya utalii imekuwa inaenda sokoni kutaganza utalii na kuweza kuandaa maonesho ili kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka pande zote duniani.

"Wafanyabishara wa utalii wataweza kuunganishwa na wadau wakubwa wa utalii na kufanya appointment moja kwa moja kwa kutumia  mfumo wa Speed Network ambao ni rahisi sana" Amesema Baraka.

Meneja huyo amesema maonesho ya biashara ni njia ya mawasiliano kwa Wafanyabiashara wakiwemo wa bidhaa za utalii.

"Kupitia maonesho ya biashara wafanyabiashara wa bidhaa za utalii wataweza kufanya mazungumzo na wadau wakubwa na kuweka makubaliano na hii itasaidia kupata mazungumzo nao ya kibiashara na wanunuaji tofauti.

"Pia inasaidia kuongeza mtandao wa biashara, kuongeza ubora wa bidhaa na kuboresha teknolojia, kutafuta wabia wapya wa kibiashara pamoja na kufanya utafiti wa masoko" amesema Baraka.

Je ni aina gani za bidhaa ambazo zikitangazwa kwenye maonesho ya bidhaa zinachochea uhamasishaji wa Utalii mkoani Mara?.

Meneja huyo wa Maendeleo ya Biashara amesema " Bidhaa za utalii, mashine na teknolojia, bidhaa za ujenzi thamani za nyumba na ofisini, kilimo na mifugo, usindikaji na vinywaji, bidhaa za nguo na ngozi, bidhaa za sanaa na kazi za mikono, bidhaa za mawasiliano ya habari pamoja na bidhaa za utalii na maliasili" amesema Baraka.


Meneja huyo ameongeza kuwa bidhaa zinazopendwa na watalii na kununuliwa ni pamoja na vyungu, mikeka, vikapu,nguo, dawa za asili na samaki.

Je nini kifanyike ili kuwezesha bidhaa za wafanyabiashara na wajasiliamali kununuliwa kwa wingi na watalii mbalimbali wakati wa maonesho ya bidhaa?.

Baraka amesema " Kabla ya yote wafanyabiashara waandaliwe mapema kwaajili yakuhakikisha wana bidhaa nyingi zenye ubora, zakipekee na kuvutia.

Pia yafanyike matangazo mengi ya bidhaa zao. Katika maonesho ya bidhaa yatakayofanyika viwanja vya Mukendo Mei, 22-28, 2023 kutakuwa na mabanda mengi katika maonesho hayo, ambayo yanakadiriwa kushirikisha jumla ya wafanyabiashara maelfu kutoka ndani na nchi za nje.

Meneja huyo wa Maendeleo ya Masoko ametoa wito kwa watanzania hususani mawakala wa masuala ya utalii wakubwa na wadogo kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho ya kujionea bidhaa mbalimbali.

Ameongeza kuwa, katika maonesho hayo kutakuwa na semina  zitazoendeshwa na wataalam waliobobea kwenye masuala ya utalii sambamba na mada mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu ya Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy kutoka Kampuni Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition amesema kampuni inaandaa Kongamano la kuhamasisha Utalii lijulikanalo Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, litakalofanyika Mei,22-28, 2023 mjini Musoma mkoani Mara.

    Mratibu wa Programu ya Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy

Amesema mpango huo wa uhamasishaji wa Utalii utakwenda sambamba na Mkutano wa Kimataifa,maonesho ya biashara na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Kutakuwa na mkutano wa Kimataifa  (International Conference)  utakaofanyika ukumbi wa NHC Mukendo Plaz, tunategemea kuwa na wageni 350 utakaofanyika kwa siku tatu, tarehe 23/05/2023 hadi 25/05/2023.

"Zitajadiliwa mada sita ambazo zitahusu  Safari, Michezo na Burudani (Travelling for businesses, Sports and Leisure),Utalii (Ecotourism), Mitumbwi ya makasia (Canoeing), Kutembea kwa miguu (Trekking), Matamasha ya asili (Cultural Festivals) na Mchezo wa kuvua samaki (Sport Fishing).

"Baada ya nadharia kutafanyika vitendo kutokana na mada zilizotajwa ambavyo vitahamasisha utalii zaidi baada ya kumalizika kwa kongamano. Pia Mei, 26-28/2023 kutafanyika Bush Party Serengeti National Park kisha kutoka hifadhini na kurudi kufunga maonesho"amesema Buchebuche.

Buchebuche ameongeza kusema kuwa maonesho ya biashara (Business Expo) yatafanyika kwa siku Saba ambapo Wajasiriamali na Wafanyabiashara mbalimbali wataweza kuonesha na kuuza bidhaa zao.




No comments