WATOA HUDUMA 3000 WAJENGEWA UWEZO KUTAMBUA WAGONJWA WA VIKOPE
Na WAF, Mbarali
ZAIDI ya watoa huduma wa afya ngazi ya jamii 3000 wa mikoa ya Njombe, Mbeya, Songwe,Iringa na Manyara wamejengewa uelewa wa kuwatambua wagonjwa wa Vikope(Trakoma) na mtoto wa jicho ili kuwasaidia wananchi kuondoa uoni unaoweza kutibika
Hayo yameelezwa na Meneja Mradi kutoka Shirika la Hellen Keller International la nchini hapa Bw. Athuman Tawakal kwenye kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho unaofanyika katika hospitali ya wilaya ya Mbarali.
Meneja Mradi kutoka Shirika la Hellen Keller International la nchini hapa Bw. Athuman TawakalBw. Tawakal amesema kuwa njia hiyo imesaidia sana kuhakikisha kwamba wanawafikia jamii kwa asilimia kubwa kwani wahudumu hao wanatoka kwenye jamii zao.
"Tunahakikisha tunawafundisha wahudumu ngazi ya jamii na baadae kupita kaya kwa kaya jambo ambalo limesaidia wananchi kuhakikisha wanajikinga na uoni unaoweza kuzuilika".
Ameongeza kuwa njia hiyo ya kuwafundisha wahuduma ngazi ya jamii kutoka kila kitongoji imesaidia kuwabaini wenye matatizo na hivyo wataalamu huweza kufika na kuwathibitisha wagonjwa na baadae kuandaa kambi za upasuaji bila malipo.
Aidha, Bw. Tawakali ameipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu kwenye hospitali nchini zikiwemo zile za wilaya na kuongeza kuwa kwa mara ya kwanza wameweza kufanya upasuaji katika 'theater' ya hospitali ya Mbarali.
Naye, Mhudumu wa afya ngazi ya jamii Bw. Wilbroad Mkwama kutoka kijiji cha Mpolo amesema muitikio wa wananchi katika kaya umekua ni mkubwa na hivyo kuweza kuwaibua wagonjwa.
Kuhusu mafunzo waliyoyapata Bw. Mkwama amesema wameyafurahia kwani wananchi wamekua wakiwapigia simu hata kama wanaumwa macho ya kawaida na kuwashauri kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Post a Comment