BODABODA WAONDOA TUTA BARABARANI WALILOLIWEKA BILA KIBALI CHA TARURA
Na Dinna Maningo, Tarime
WAENDESHA Pikipiki (Bodaboda) katika kituo cha Mabanzini mtaa wa Ronsoti Kata ya Nyamisangura halmashauri ya mji Tarime mkoani Mara wameondoa tuta waliloliweka barabarani kwa lengo la kujilinda na ajali za barabarani.
Wakizungumza na DIMA Online katika barabara ya Lema wamesema wameondoa tuta hilo baada ya Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa kuwaagiza kuliondoa kutokana na kuwekwa bila kufuata taratibu za uwekaji matuta pamoja na kibali kutoka TARURA.
Mwenyekiti wa Kituo cha maegesho ya Pikipiki cha Mabanzini Charles Jakayongo amesema wamelazimika kuliondoa baada ya kushauriwa na Meneja huyo wa Tarura kuwa liliwekwa bila kufuata taratibu za uwekaji matuta barabarani.
"Meneja TARURA alikuja hapa akatuambia tuondoe tuta hilo kwamba tumeweka kimakosa, akatuelekeza utaratibu wa uwekaji tuta kisha akasema inatakiwa tuweke matuta mawili moja juu na lingine chini na sio kuweka tuta moja katika eneo ambalo ni hatarishi.
"Tumeondoa na kuweka matuta mawili kama unavyoyaona Mwandishi wa Habari. Tuliweka kwa ajili ya waendesha vyombo vya moto kupunguza mwendo kasi na ajali zisizo tarajiwa.
"Sehemu hii ni hatari bodaboda wanakimbiza spidi, tukaweka kwa ajili ya usalama wa bodaboda kwenye kijiwe chetu kwasababu tunaegesha Pikipiki karibu na barabara" amesema.
"Tunaomba watu wa TANROAD waweke tuta kwenye ile barabara ya lami ya Zambia -Nairobi pale njia panda ukiwa unaingia barabara inayokwenda Tarime mjini na inayokwenda Sirari kuelekea Kenya, wengine wanaita barabara ya Kenyata" amesema Charles.
Mwendesha pikipiki Pascal John amesema waliweka tuta ili kuepusha watoto kugongwa na pikipiki lakini baada ya kuliweka Meneja TARURA aliwaagiza kuliondoa akidai limekaa vibaya .
"Alikuja huyo Meneja akasema tuta limekaa vibaya tuliondoe, ilikua kipindi cha nyuma wakati wanakwangua barabara,tuliliondoa baada ya hapo tukampigia simu Diwani tukamwambia mazingira ya hapa yalivyo akaturuhusu akasema tuweke lakini tusiweke kubwa sana tuweke la wastani tuendelee kutumia tukaweka.
"Sasa leo (Jana) huyu kiongozi amepita hapa akatuambia tutoe na ni mara nyingi amekuwa akitusisitiza tuondoe, akasema lihame kutoka hapa tuweke pale na lingine pale chini yawe mawili na sio moja, tumefuata maelekezo yake kama unavyoona Mwandishi wa Habari tulijiongeza wenyewe kuweka tuta.
Pascal ameongeza kuwa watoto wamekuwa wakikoswakoswa kugongwa kutokana na mwendo kasi wa waendesha pikipiki katika barabara hiyo hivyo wameweka matuta mawili kwakuwa ni muhimu kwa ajili ya usalama kwa watumiaji wa barabara.
"Sisi ni wakazi wa hapa tunaona pikipiki zinavyokuja spidi, tumeona kabla ya ajali tuweke kinga, tumeweka tahadhali kwasababu mtu anatoka huko spidi sana mpaka chini, tukaamua tuweke kwa ajili usalama wetu na watembea kwa miguu.
"Pia tumeweka ili kupunguza vumbi kutokana na spidi za pikipiki wanapopita kwenye eneo hili wanapofika wanapunguza mwendo " amesema Pascal.
Wameiomba TARURA kuweka tuta katika barabara hiyo kuliko na kibao kwakuwa ni hatarishi kwa wanafunzi wanapovuka barabara kwenda shule za msingi zilizopakana na barabara hiyo.
Diwani wa Kata ya Nyamisangura Thobias Ghati amesema " Meneja alinipigia simu kuwa kawaambia waondoe tuta na akawapa maelekezo namna ya kuweka matuta, amefanya jambo jema kutoa hiyo elimu kwa wananchi ya uwekaji sahihi wa matuta "amesema Thobias.
>>>Rejea
Siku chache zilizopita DIMA Online iliripoti habari yenye kichwa cha habari 'TARURA TARIME YAPIGA MARUFUKU WANANCHI KUWEKA MATUTA BARABARANI'.
Katika habari hiyo Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa alipiga marufuku kitendo cha wananchi kuweka matuta barabarani bila kibali kwa madai kwamba uwekaji wa matuta una taratibu zake.
Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa
Mhandisi Charles alisema kuwa kumekuwa na tabia ya wananchi kuweka matuta na kwamba uwekaji matuta ni kazi ya TARURA na si wananchi vinginevyo wawe na kibali kutoka TARURA cha kuwaruhusu kuweka matuta.
"TARURA ndio inaweka matuta barabarani au TANROAD ndio wanafahamu je eneo fulani kweli linahitaji tuta?, kuna viashiria vya kuweka tuta kwa mfano kuna huduma za jamii kama hospitali, shule, zahanati, kanisa, msikiti au soko sehemu ambayo wanapita watu wengi.
"Sio tu mwananchi ajiamlie kisa tu hapa ni kwangu naona mtoto anaweza kugongwa ngoja niweke tuta, hatufanyi hivyo. Mimi nikimkuta mtu aliyeweka matuta pasipo kibali huwa nakamata namwambia ondoa na anaondoa, nimeshawashughulikia kadhaa" alisema Mhandishi Charles.
Amesema endapo wananchi wanataka kuweka matuta wafuate taratibu " Kama wanataka kuweka matuta wanatakiwa waombe kuweka tuta sehemu fulani sisi twende tutathmini kuwa hapa panahitaji tuta au alama za barabarani.
"Tukishaona kama panahitaji tuta tunashauri wawekeje, matuta mengi wanaweka unakuta eno la ajali ni hili hapa yeye anaweka tuta pale, sasa mimi nikija na spidi maana yake hata kama wameweka tuta nakugonga.
" Maana yake nikishika breki spidi itarudi 30 sasa ikikugusa lazima nitakuumiza. Kama tunataka kulinda hapa tunaweka kutoka pale tunapotaka kulinda mita 30 juu na chini yanakuwa matuta mawili ili hiyo mita 30 nikifika namuona yulee napunguza mwendo.
" Sasa wao wanaweka tuta palepale wanapoona panasababisha ajali haiwasaidii, watoto wengi wanagongewa kwenye tuta, ukichora Zebra kwa kawaida lazima uweke mita 20 au 30 kabla ya hiyo sehemu, kuna barabara za TARURA na TANROAD" alisema Mhandisi Charles.
Pia, aliwanyooshea kidole watumiaji wa vyombo vya moto hasa vijana waendesha Pikipiki (Bodaboda) na Bajaji kwa kile alichosema kwamba wamegeuza pikipiki kuwa majanga.
"Tukishazitengeneza zikawa nzuri wao wanakuwa waharibifu, tumejitahidi kuweka alama lakini hawatii sheria, yaani yeye akiwa barabarani anawaza abiria ntampata wapi hajali sheria za barabarani zinamtaka afanyeje.
"Vibao vipo lakini wanakimbiza spidi, tumeshatoa elimu kwa kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani RTO ametushirikisha sana katika kutoa elimu lakini ilishakuwa hurka kwa vijana ni tabia ya mtu japo sio wote lakini walio wengi uendeshaji wao sio wa kistaarabu.
Mhandisi huyo aliongeza kuwa uendeshaji pikipiki kwa mwendo kasi unapelekea wananchi kujiwekea matuta barabarani jambo ambalo limechangia uharibifu wa barabara.
"Ukiweka tuta kila sehemu hiyo siyo barabara, kwanza matuta yanapelekea uharibifu wa barabara maji yakija yanaziba mitaro maana hayajawekwa kitaalam, wengine wanaweka mawe matokeo yake wanaziba mitaro maji yanaenda barabarani.
" Nikikuta hivyo nasimamia wanaondoa hilo tuta kisha nawaeleza fuateni taratibu kama kweli panahitaji tuta liwekwe, wananchi wafuate taratibu" amesema Charles.
Meneja huyo amewasisitiza wananchi na watumiaji wa vyombo vya moto kutunza barabara na kufuata sheria za usalama barabarani kwani Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa miradi ya barabara.
Post a Comment