CHANJO YA MIFUGO YAZINDULIWA KUKABILIANA NA MAGONJWA
Na Samwel Mwanga,Maswa
SERIKALI katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imezindua zoezi la chanjo ya Mifugo kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu kwa ng'ombe na ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo.
Akizindua zoezi hilo katika Kijiji cha Zanzui wilayani humo,Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge amesema kuwa ni vizuri wafugaji wa wilaya hiyo wakaunga mkono juhudi za serikali kwa kuhakikisha Mifugo yao yote inapata chanjo hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge (mwenye miwani) akimkabidhi, Afisa Mifugo wa wilaya hiyo, Dk Charles Musira(kushoto) vifaa vitakavyotumika katika chanjo ya Mifugo wakati wa uzinduzi wa zoezi la chanjo ya Mifugo wilayani humo katika Kijiji Cha Zanzui.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imetoa fedha kwa ajili ya kununua chanjo hizo na lengo ni kuwasaidia wananchi hasa wafugaji kukabiliana na magonjwa hayo yanayosambulia mifugo yao.
Kaminyonge amesema kuwa zoezi lilianza mapema April mosi mwaka huu lakini uzinduzi wake umefanyika Aprili, 23, 2023 lakini limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo na wafugaji kutokuwa na Elimu ya kutosha juu ya chanjo hiyo.
"Zoezi hili nimeelezwa kuwa lilianza tangu April mosi mwaka huu katika wilaya yetu ya Maswa na tayari kuna Kata nane mifugo imepata chanjo ila kulizuka sintofahamu kutoka kwa Wananchi kutoka na kutokuwa na Elimu ya kutosha juu ya chanjo hiyo,"
"Wafugaji zoezi hili halina uhusiano wowote na zoezi lililositishwa na serikali la kuweka hereni kwenye mifugo hivyo nitoe rai yangu kwa wafugaji wote wa wilaya ya Maswa wapeleke Mifugo yao ikapate chanjo,"amesema.
Pia ameagiza maeneo ambayo zoezi hili limefanyika na baadhi ya Mifugo haikuchanjwa zoezi hilo lilirudiwe mara baada ya Kata zote kumalizika.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya Maswa, Onesmo Makota amesema kuwa zoezi hilo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho hivyo ni vizuri likafanywa kwa kufuata taratibu zote ambazo zimewekwa ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wafugaji yaliyojitokeza hapo awali.
Pia ametumia muda huo kuwaomba wafugaji wa wilaya hiyo kutokuacha kupeleka mifugo yao kupata chanjo kwani ina faida kubwa kwao kwa kulinda Afya ya Mifugo yao
Awali Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Dk James Kawamalwa alisema kuwa katika utekelezaji wa mapambano dhidi ya magonjwa ya wanyama wameanza na magonjwa hayo mawili kwa pamoja ambayo yamekuwa kero ya muda mrefu kwa mifugo katika wilaya hiyo.
Afisa Mifugo wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Dk James Kawamalwa(mwenye kipaza sauti)akieleza umuhimu wa Chanjo ya Mifugo Kwa wafugaji wa Kijiji Cha Zanzui kilichoko wilayani humo.
Amesema tangu zoezi kuanza wamekwisha kuchanja ng'ombe 31,442,Mbuzi 3,483 na kondoo 2,320 katika Kata hizo na malengo ni kuchanja ng'ombe 305,640,mbuzi 122 na kondoo 76,410.
Amesema katika zoezi hilo mfugaji atachangia kiasi cha Sh 800 kwa ng'ombe mmoja na Sh 400 kwa kondoo na mbuzi mmoja mmoja.
Aidha amesema Ili waweze kukidhi vigezo vya kitaalam katika udhibiti wa magonjwa na Kwa mujibu wa kanuni za chanjo na uchanjaji Mifugo ya Mwaka 2020 ni lazima wachanje Mifugo angalau asilimia 80.
Post a Comment