HEADER AD

HEADER AD

TARURA YAJENGA VIVUKO 42 KUWAONDOLEA KERO WATUMIA BARABARA TARIME DC

Na Dinna Maningo, Tarime

UKOSEFU wa Vivuko Barabarani ni moja ya changamoto kubwa inayowakera wananchi, na kuwapa usumbufu wanapotumia barabara wakati wanapoenda katika majukumu yao au kupata huduma za kijamii.

Kuwepo kwa chagamoto ya mawasiliano ya barabara maeneo ya vijito, mito na barabara korofi wakati wa mvua, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan imewaondolea adha wananchi katika baadhi ya barabara.

Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha ikaidhinisha Bajeti ya Matengenezo ya Barabara kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime, Tsh.Bilioni 2.209 kutengeneza barabara zilizopo  Halmashauri ya wilaya ya Tarime.

MENEJA Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa anasema vyanzo hivyo ni tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti  Sh. 100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli kiasi cha Tsh Bilioni moja.
   Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa

Fedha ya Jimbo la uchaguzi Tsh. Milioni 500 na fedha kutoka mfuko wa barabara Tsh. Bilioni 1.27. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 TARURA imepokea Tsh.Bilioni 1.265 sawa na asilimia 50 zilizotekeleza miradi mbalimbali ambapo matengenezo yamefikia asilimia 80.

Mhandisi Charles anasema kuwa baadhi ya barabara zilikuwa ni chagamoto kwa wananchi kutokana na kutokuwa na vivuko na hivyo kuwa kero kwa wananchi wakati wapitapo kwenda katika shughuli zao.

Anasema  kupitia bajeti hiyo ya 2022/2023, TARURA imewaondolea adha wananchi kwani imefanikiwa kujenga Vivuko 42 kwa baadhi ya Vijiji  katika Halmashauri hiyo.


"Tumejenga vivuko vikubwa na vidogo, kwa mfano, tumejenga kivuko kikubwa Nyarwana -Turuturu chenye urefu wa mita 11,kimekamilika wananchi hawahangaiki  wanapita bila shida.

"Tumefungua barabara mpya jumla km 36.4 ambazo zilikuwa changamoto, mfano Kikomori tumefungua barabara ya km 5, tumefungua barabara ya Kebweye- Magoto na tumejenga kivuko kikubwa. Watu walikuwa wanahangaika kuzunguka Pemba au kupita Nyamwaga" anasema Mhandisi Charles.

Meneja huyo anaongeza "Tumejenga barabara za changarawe km 151, tumekarabati barabara za udongo km 219.5, na zingine zitaendelea kutengenezwa kadri pesa itakavyopatikana.

"Kaulimbiu ya TARURA tunasema 'Tunakufungulia barabara kufika kusikofikika', Kule kulikokuwa hakufikiki sisi tunakufanya ufike', TARURA Tarime tunasema 'Alipo Mwananchi barabara iwepo' ndio kaulimbiu yetu akitoka ndani akutane na barabara.

Mhandisi Charles anasema inawezekana kwakuwa Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikiendelea kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara, ushirikiana na wananchi na Madiwani  katika utekelezaji.

"Rais Dkt Samia ametuletea fedha kwanini tusitekeleze? , wananchi na Madiwani tunashirikiana vyema katika utekelezaji wa miradi ya barabara" Anasema Meneja huyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakonga Kata ya Nyakonga John Ryoba mtumiaji wa barabara ya Kebweye- Magoto ameipongeza Serikali kwa kujenga barabara na Kivuko na anaishukuru TARURA Tarime kwa kuwaondolea usumbufu.

"Wananchi tulipata shida ili mtu aende Kebweye alilazimika kupita Kijiji cha Nyakonga aende Borega ndio afike Kebweye, mzumguko ulikuwa mrefu, watu walipata shida kwenda kupata huduma ya afya Kituo cha afya Magoto" anasema John.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandage Kata ya Nyanungu Mwita Kiha anasema" Barabara kwakweli imejengwa vizuri imenyooka kama vile unakula wali, ukitoka Nyandage kwenda Kegonga senta yaani ipo vizuri, isipokuwa maeneo ya Zahanati ndio bado tunaomba nako ijengwe"anasema Mwita.

Mkazi wa Kijiji cha Nyakunguru Kata ya Kibasuka Matiko Nyaiho anasema kujengwa kwa kivuko cha Nyarwana kilichopo Kitongoji cha Mwara ni faida kwa wakulima.

Mkazi wa Kijiji cha Nyarwana Kata ya Kibasuka Matiko Nyeiho

"Tunaishukuru Serikali na TARURA kutujengea kivuko, kabla ya kujengwa kivuko wananchi walihangaika sana mvua ikinyesha huvuki, mto unajaa maji, inabidi msubiri maji yapungue ndipo mvuke, wakati wa mvua mkulima alikuwa hawezi kusafirisha mazao.

Matiko anasema Wagonjwa na Wajawazito walipata shida kwakuwa wananchi wa Kitongoji cha Mwara na maeneo mengine ili wapate huduma ya afya ni lazima wavuke mto.

Anasema vipindi vya mvua pikipiki zilishindwa kuvuka mto na hivyo watu kulazimika kuwabeba mgongoni Wajawazito, wagonjwa na wanafunzi kuwavusha mto.

"Kivuko hicho kimewaondolea adha wananchi sasa hivi watembea kwa miguu wanapita bila shida, isipokuwa gari ndio bado hazijaruhusiwa kupita nadhani wanasubiri kikauke vizuri. Kivuko kitawasaidia wakulima kusafirisha biashara ya mazao, pia ni kiungaishi cha kwenda Nyamongo.

Matiko anasema kuwa bado kuna changamoto katika kivuko kinachounganisha wakazi wa Kijiji cha Nyakunguru  na Nyarwana ni kibovu kimeharibika na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara

Anasema  madereva wa gari zikiwemo zinazokwenda Nyamongo na pikipiki hushindwa kupita hali inayowalazimu kusubiri kwa saa kadhaa maji yaishe ndipo wavuke.

Anaiomba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwaondolea kero ya kivuko hicho kwani msimu huu wa mvua wananchi wanapata tabu.







No comments