HEADER AD

HEADER AD

TARURA TARIME YAPIGA MARUFUKU WANANCHI KUWEKA MATUTA BARABARANI

Na Dinna Maningo, Tarime

MENEJA Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa amepiga marufuku kitendo cha wananchi kuweka matuta barabarani bila kibali kwa madai kwamba uwekaji wa matuta una taratibu zake.

Akizungumza na DIMA Online, Mhandishi Charles amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuweka matuta barabarani na kwamba uwekaji matuta ni kazi ya TARURA na si wananchi vinginevyo wawe na kibali kutoka TARURA cha kuwaruhusu kuweka matuta.

    Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa

"TARURA ndio inaweka matuta barabarani au TANROAD ndio wanafahamu je eneo fulani kweli linahitaji tuta?, kuna viashiria vya kuweka tuta kwa mfano kuna huduma za jamii kama hospitali, shule, zahanati, kanisa, msikiti au soko sehemu ambayo wanapita watu wengi.

"Sio tu mwananchi ajiamlie kisa tu hapa ni kwangu naona mtoto anaweza kugongwa ngoja niweke tuta, hatufanyi hivyo. Mimi nikimkuta mtu aliyeweka matuta pasipo kibali huwa nakamata namwambia ondoa na anaondoa, nimeshawashughulikia kadhaa" amesema Mhandishi Charles.

Amesema endapo wananchi wanataka kuweka matuta wafuate taratibu " Kama wanataka kuweka matuta wanatakiwa waombe kuweka tuta sehemu fulani sisi twende tutathmini kuwa hapa panahitaji tuta au alama za barabarani.

"Tukishaona kama panahitaji tuta tunashauri wawekeje, matuta mengi wanaweka unakuta eneo la ajali ni hili hapa yeye anaweka tuta pale, sasa mimi nikija na spidi maana yake hata kama wameweka tuta nakugonga.

"Maana yake nikishika breki spidi itarudi 30 sasa ikikugusa lazima nitakuumiza. Kama tunataka kulinda hapa tunaweka kutoka pale tunapotaka kulinda mita 30 juu na chini yanakuwa matuta mawili ili hiyo mita 30 nikifika namuona yulee napunguza mwendo.

" Sasa wao wanaweka tuta palepale wanapoona panasababisha ajali haiwasaidii, watoto wengi wanagongewa kwenye tuta, ukichora Zebra kwa kawaida lazima uweke mita 20 au 30 kabla ya hiyo sehemu, kuna barabara za TARURA na TANROAD" amesema Mhandisi Charles.


Pia, amewanyooshea kidole watumiaji wa vyombo vya moto hasa vijana waendesha Pikipiki (Bodaboda) na Bajaji kwa kile alichosema kwamba wamegeuza pikipiki kuwa majanga.

"Tukishazitengeneza barabara zikawa nzuri wao wanakuwa waharibifu, tumejitahidi kuweka alama lakini hawatii sheria, yaani yeye akiwa barabarani anawaza abiria ntampata wapi hajali sheria za barabarani zinamtaka afanyeje.

"Vibao vipo lakini wanakimbiza spidi, tumeshatoa elimu kwa kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani RTO ametushirikisha sana katika kutoa elimu lakini ilishakuwa hurka kwa vijana ni tabia ya mtu japo sio wote lakini walio wengi uendeshaji wao sio wa kistaarabu.

Mhandisi huyo amesema uendeshaji pikipiki kwa mwendo kasi unapelekea wananchi kujiwekea matuta barabarani jambo ambalo limechangia uharibifu wa barabara.


"Ukiweka tuta kila sehemu hiyo siyo barabara, kwanza matuta yanapelekea uharibifu wa barabara maji yakija yanaziba mitaro maana hayajawekwa kitaalam, wengine wanaweka mawe matokeo yake wanaziba mitaro maji yanaenda barabarani.

" Nikikuta hivyo nasimamia wanaondoa hilo tuta kisha nawaeleza fuateni taratibu kama kweli panahitaji tuta liwekwe, wananchi wafuate taratibu" amesema Charles.

Samsoni Mwita mkazi wa mtaa wa Rebu shuleni amesema wananchi wanalazimika kuweka matuta kutokana na kasi ya waendesha pikipiki ambayo huatarisha usalama wao wakiwemo watoto.

"Wananchi wanaweka baada ya kuona ajali zimezidi ili vyombo vya moto vipunguze ajali, tuna watoto alafu eneo unaona linaleta shida ukae kusubiri TARURA ambao ili waje kutengeneza hadi waweke kwenye bajeti zao wapitishe wapate pesa ndio waje kuweka.

"Jambo hilo mtasubiri mpaka mchoke hawaji kuweka, sasa watu waendelee kuumia kisa tunasubiri bajeti za serikali wakati wananchi wana uwezo wa kutumia nguvu zao kubeba jembe na kutengeneza tuta bila gharama. Wananchi wanaamua kuweka matuta wenyewe ili kujilinda na ajali" amesema Samson.

Peter Werema ni mwendesha pikipiki mkazi wa mtaa wa Kebikiri mjini Tarime amesema uwekaji wa matuta bila kufuata sheria za barabarani umekithiri na kuwa kero.

    Peter Werema ni mwendesha pikipiki mkazi wa mtaa wa Kebikiri mjini Tarime

"Hata mtaani kwangu wananchi walishaweka matuta mengi hadi imekuwa kero kwasababu unaweza kupita hatua tatu unakuta kuna tuta, wao wanaona ni sawa lakini sisi tunaoendesha vyombo vya moto inakuwa ni changamoto.

"Kinachochangia wananchi kuweka matuta ni bodaboda unakuta wanapita sehemu ni makazi ya watu hawatambui kuwa unapofika unatakiwa kupunguza spidi lakini hawapunguzi" amesema. 

Peter ameongeza kuwa hali hiyo hupelekea wananchi kujichukulia maamuzi na kuweka matuta ili kusaidia kuondoa ajali kwakuwa maeneo hayo yanakuwa na watu wengi wakiwemo watoto.

Amesema pamoja na changamoto hiyo si vyema wananchi kuweka matuta barabarani wanatakiwa wafuate sheria za barabarani kwani wanaotakiwa kuweka matuta ni TARURA na TANROAD.

Ameongeza kuwa uwekwaji wa matuta barabarani uliozingatia sheria husaidia waendesha pikipiki kupunguza mwendo au kusimama pindi wananchi wavukapo barabara wakiwemo wanafunzi.

No comments