JUMUIYA YA WAZAZI CCM YAAGIZA KUUNDWA KLABU ZA MAADILI SHULENI
Na Alodia Babara, Bukoba
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) mkoa wa Kagera Alfonsina Barongo ameagiza kuundwa Klabu za Wanafunzi za maadili pamoja na kuimarisha vipindi vya dini katika shule ya Sekondari Kashai na Bilele zilizopo manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ili vijana hao wawe na maadili mema.
Barongo ametoa maagizo hayo mawili jana katika kongamano la wanafunzi hao lililofanyika shule ya sekondari Kashai kwa kuunganisha wanafunzi wa shule mbili za sekondari za Kashai na Bilele zenye zaidi ya wanafunzi 1500.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi (CCM) mkoa wa Kagera Alfonsina Barongo akizungumza katika kongamano
Lengo la kongamano hilo lilikuwa ni kuondoa mmomonyoko wa maadili kwa vijana wa Tanzania kutokana na tatizo la ushoga na usagaji ambalo limeibuka katika jamii.
Ameagiza walimu wakuu, walimu wa nidhamu, walimu wa zamu na walimu wa kawaida kuungana pamoja na kuunda klabu za wanafunzi za maadili ambazo zitasaidia kuelimisha wanafunzi hao kuhusu maadili mema pamoja na kuimalisha vipindi vya dini mashuleni kwa kuhamasisha kuwepo msukumo wa ufundishaji kama vipindi vingine.
“Klabu hizi zitasaidia kufundishana sisi kwa sisi, kuonyana sisi kwa sisi, walimu wakuu, walimu wa nidhamu, walimu wa zamu na walimu wote kwa ujumla tuungane katika kuunda Klabu za maadili za wanafunzi na uwepo msukumo wa kufundisha vipindi vya dini maana najua vipo mashuleni lakini havina msukumo wa ufundishaji” Amesema Barongo
Amesema kuna wanafunzi wengine muda wa vipindi vya dini ndiyo muda wao wa kwenda kuvuta bangi na kwenda nyumbani hivyo vipindi vikiwepo mashuleni vitasaidia kufundisha maadili mema kwa watoto wetu na watoto watakaposhika dini wataweza kuepukana na mmomonyoko wa maadili na kuwa watoto wema na tutapata mama na baba wa badae.
Wanafunzi wa sekondari ya Bukoba walioshiriki katika kongamano
Aidha amemtaka Mtendaji wa kata ya Kashai kuhakikisha wanafunzi wote wanakunywa uji au kula chakula shuleni kutokana na kubaini shule ya Kashai yenye wanafunzi zaidi ya 800 lakini waliokuwa wanakunywa uji/kula chakula shuleni walikuwa wanafunzi 131 kutokana na mwitikio mdogo wa wazazi katika kuchangia chakula.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) mkoa wa Kagera Chuki Alex ametaja kazi za jumuiya hiyo kuwa ni kuunganisha nguvu wilaya na mkoa, kuwahusisha wazazi katika kuwaunganisha katika malezi na makuzi.
Katibu wa jumuiya ya wazazi (CCM) Mkoa wa Kagera Chuki Alex akizungumza katika kongamano na wanafunzi na walimu kuhusu mmomonyoko wa maadili.
Alex amesema katika maadhimisho ya miaka 68 ya kuzaliwa kwa jumuiya hiyo ya wazazi wamefanya makongamano mbalimbali katika shule za sekondari za Bukoba, Kashai na Bilele.
Amesema katika makongamano hayo wamefundisha mada mbalimbali za utandawazi, malezi na makuzi, mmomonyoko wa maadili, ukatili wa kijinsia na rushwa na kilele kitafanyika April 28, mwaka huu Bukoba vijijini katika kata ya Nyakato kituo cha kulelea wazee cha Kilima.
Akitoa mada ya malezi na makuzi kwa wanafunzi hao, mjumbe wa kamati ya utekelezaji mkoa John Bahebe aliwasisitiza wanafunzi kuacha kuiga tabia za kigeni ambapo amesema kuna tabia za ushoga na usagaji zinafanyika na kwamba tabia hizo zinaharibu mila na tamaduni za Kitanzania.
Amesema wanapaswa kutoa taarifa pale watakapogundua kuna vitendo vya ushoga na usagaji vinafanyika miongoni mwao kwani vitendo hivyo vikifanyika vinaharibu kizazi cha leo na kizazi kijacho.
“Mtu akijihusisha na ushoga na usagaji husababisha misuri ya uzazi kulegea na mwisho wake husababisha kama ni mwanamke au mwanamme kujikuta anatokwa kinyesi na aja ndogo ovyo jambo ambalo litamlazimu kujifunga pampasi” Amesema mwl Bahebe
Aidha ametoa Rai kwa walimu ambao ni walezi kuendelea kuwalea watoto kwa kuwafundisha maadili mema wanapokuwa shuleni na kuita mikutano ya wazazi na kujadiliana nao kuhusu tabia za watoto wao.
Post a Comment