HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI AIOMBA TARURA KUJENGA MITARO BARABARA ZA MTAA WA KOKEHOGOMA

Na Dinna Maningo, Tarime 

MWENYEKITI wa Mtaa wa Kokehogoma kata ya Turwa wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, Musa Nehemia ameiomba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga mitaro ili kulinda miundombinu ya barabara.

Amesema licha ya barabara za mtaa wa Kokehogoma kujengwa na zingine kukarabatiwa pamoja na uwekwaji wa Vivuko/Karavati lakini bado kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa mitaro katika barabara.

   Mwenyekiti wa Mtaa wa Kokehogoma kata ya Turwa wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, Musa Nehemia

Mwenyekiti huyo aliongozana na Mwandishi wa DIMA Online kutembelea baadhi ya barabara zenye changamoto ya mitaro.

Musa amesema Serikali inatenga fedha nyingi kujenga barabara, vivuko/Karavati na madaraja lakini zinadumu kwa miaka michache kutokana na maji ya mvua kuingia barabarani na kuharibu barabara.

    Mwenyekiti wa Mtaa wa Kokehogoma kata ya Turwa wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, Musa Nehemia

"Barabara zimejengwa na baadhi zimekarabatiwa lakini shida ipo kwenye mitaro,barabara zilikuwa nzuri lakini baadhi zimeharibiwa na maji ya mvua kwasababu hakuna mitaro inayokusanya maji kupeleka mtoni, mvua ikinyesha yanajaa barabarani watu wanashindwa kupita.

"Kuna barabara zimeanza kukatika kwasababu ya kuzidiwa maji, naomba Serikali itutizame ijenge mitaro kunusuru gharama za kila mara zinazotumika kukarabati barabara kwa sababu tu hakuna mitaro.

" TARURA wachimbe mitaro kuelekeza kwenye makaravati yaliyojengwa ili maji yote yajikusanye yapite kwenye karavati" amesema.

 
Musa amesema changamoto nyingine ni upanuzi wa barabara kwani kuna baadhi ya barabara wamezitenga lakini hazijajengwa na hivyo kusababisha mtaa huo kuonekana upo porini licha ya kwamba ni mtaa uliopo ndani ya Halmashauri ya mji Tarime.

"Tunaonekana tupo porini japo ni mtaa ambao upo mjini kwasababu ya vichaka vilivyopo, Serikali iutazame mtaa wetu itulimie barabara walau hata kuparua kuonesha kuna barabara" amesema.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa changamoto nyingine ni Wakandarasi kutowashirikisha viongozi wa mitaa pindi miradi inapokamilika ili nao wajiridhishe juu ya miradi hiyo ya barabara.

        Karavati Barabara ya Kebikiri - Kokehogoma

"Wakandarasi huwa wanatushirikisha pale wanapokuja kuanza kujenga mradi lakini wanavyoendelea kujenga hadi ukamilishaji hatushirikishwi.

"Tunaomba TARURA itushirikishe sisi viongozi wa mitaa katika hatua zote za ujenzi ili nasi tufike tujiridhishe,wao wakikamilisha wanondoka bila sisi kukagua matokeo yake unakuta mradi unakasoro na wao wameshakabidhi mradi TARURA wanaondoka zao" amesema Mwenyekiti.

Ameongeza" Sisi ndio tunaziomba hizi barabara wanapokuwa hawashirikishi viongozi wa mtaa tunashindwa namna ya kuchangia mawazo yetu juu ya miradi hiyo.


"Mradi ukiwa na changamoto sisi viongozi ndio tunahojiwa na wananchi sisi ndio tuna watu, mradi ukiwa na kasoro wanaoulizwa ni sisi viongozi wa mitaa tunakosa majibu ya kuwaambia kwasababu hatushirikishwi kwenye miradi hiyo ya barabara "amesema Musa.

Mbali na hayo Mwenyekiti huyo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha za barabara zilizofanikisha kupunguza changamoto za barabara katika mtaa wa Kokehogoma.

      Barabara ya Mtaa Kokehogoma

"Namshukuru Rais Samia kwa kutuona kwasababu huko nyuma barabara kwenye mtaa wangu zilikuwa na chagamoto kubwa, watembea kwa miguu na watumiaji wa vyombo vya moto walihangaika sana, mvua iliponyesha ilikuwa tabu kuvuka vijito na mito.

" Barabara zingine zilikatika kutokana na maji kujaa barabarani, tulishughulikia na wananchi lakini tulishindwa kutokana na wingi wa maji, lakini baada ya kulalamika kwa Diwani wetu alipeleka kilio chetu Halmashauri na TARURA" amesema Musa.

Ameongeza " Tunashukuru mwaka jana TARURA ilikuja ikatuwekea Karavati sehemu ambazo zilikuwa shida kwasababu ya maji ya mvua, tunawashukuru Serikali na TARURA kwa kusikia kilio chetu" amesema Musa.

Musa ameiomba Serikali katika bajeti ya 2023/2024 kuitengea TARURA fedha za kutosha kutengeneza mitaro ambayo imesababisha barabara kuharibika licha ya kukarabatiwa mara kadhaa kwa sababu ya kutokuwepo mitaro.


Km 1.9 za mitaro zajengwa 

Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2003 TARURA imefanikiwa kujenga mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa  mita 1,900 sawa na km 1.9 katika halmashauri ya mji Tarime.

   Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa

"Changamoto kubwa tunayoipata maeneo ya mjini hususani Halmashauri ya Tarime Mji ni namna gani unaweza kukusanya maji ya mvua, huwezi kuchepusha kwasababu ukichepusha tu yanaenda kwenye makazi ya watu wamejenga mji umeenea" amesema. 

Ameongeza " Tumewekeza kwenye ujenzi wa mitaro kuhakikisha tunaondoa kero kwa wananchi ya maji ya mvua lakini pia kulinda miundombinu ya barabara ndiyo maana tumejenga mitaro jumla ya urefu wa Mita 1900 sawa na Km 1.9.

      Mtaro barabara ya Dkt. Wainani

" Kwahiyo utaona kuwa barabara zetu fupi za mita 300 au mita 200 tumegusa maeno mengi mojawapo maeneo ya posta kuanzia Criss Pub wanachi wa pale mvua iliponyesha walikuwa hawalali maji yalikuwa yanakwenda kwenye nyumba za watu.

" Pia Tumejenga mtaro mrefu unaokusanya maji kuyarudisha mtoni, lakini pia tumejenga pale maeneo ya Dkt. Wainani, maeneo ya magereza tumejenga mitaro barabara mbili.

Wakati wa mvua mchanga wote ulikuwa unaingia barabarani tumejenga mitaro na barabara ipo vizuri, maeneo yaliyokuwa korofi tumejenga mitaro maji yanaingia kwenye maeneo yake vizuri" amesema Mhandishi Charles.

           Mtaro barabara ya Posta

Meneja huyo ameishukuru Serikali inayoongozwa na  Rais Samia kutoa fedha nyingi za ujenzi wa barabara katika Halmashauri ya Mji kwa kile alichoeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilitengewa bajeti ya matengenezo ya barabara Tsh. Bilioni 2.209.

Amesema bajeti hiyo ni ongezeko la zaidi ya mara tatu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha Tsh. Milioni 729  hali ambayo imesaidia kuwapunguzia wananchi kero za barabara.


Mhandisi Charles amesema bajeti hiyo ya matengenezo ya barabara ni kutoka katika vyanzo vitatu vya mapato ambavyo ni fedha ya tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti ambayo ni makato ya Tsh. 100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli kiasi cha Tsh. Bilioni moja.

Fedha ya Jimbo la uchaguzi Tsh. Milioni 500 na fedha kutoka mfuko wa barabara kiasi cha zaidi ya Milioni 700 na kwamba hadi kufikia Machi, 2023 TARURA imepokea fedha Bilioni 1.295 sawa na asilimia 58.6.

Ameongeza kuwa fedha zote zimepokelewa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara katika Halmashauri ya Mji Tarime, ambapo matengenezo hadi kufikia mwezi Machi ni asilimia 91.3.




No comments