HEADER AD

HEADER AD

MGONJWA WA MARBURG ARUHUSIWA BAADA YA KUPONA

Na Catherine Sungura,Dar es Salaam

MGONJWA mmoja wa Marburg mwenye umri wa miaka (26) ameruhusiwa akiwa na afya njema  huku jamii ikitakiwa kumpokea vyema na kushirikiana nae katika shughuli zake. 

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa  wa Marburg ulioripotiwa Wilaya ya Bukoba vijijini mkoani kagera.

     Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

“Ninayo furaha  kubwa kuwajulisha kuwa leo tumemruhusu mgonjwa mmoja  mwanaume mwenye umri wa miaka (26) akiwa na afya njema, ni matumaini yangu jamii itampokea vyema na kushirikiana nae kama kawaida, ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa hatujapata wagonjwa wapya wala vifo”.

Aidha, tangu kuripotiwa ugonjwa huo Machi 21, 2023 kufikia Aprili 4, 2023 jumla ya visa ni 8 na vifo 5.Waziri Ummy ameongeza kuwa wagonjwa wawili waliolazwa wanaendelea vizuri na matibabu katika vituo maalumu vilivyoandaliwa.

Hata hivyo Waziri amesema kuwa jumla ya watu 212 waliochangamana na wagonjwa wamebainishwa na kati ya hao watu 35 wamemaliza siku 21 za uangalizi bila kuonesha dalili  zozote za ugonjwa .

Hii ni ishara  nzuri sana kwetu, Wizara ya afya , serikali na taifa kwa ujumla kwa kuwa maambukizi ya Virus vya Marburg nchini yamedhibitiwa kwa wakati.Serikali bado inahimiza wananchi wote na hasa wa mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua tahadhari, kudhibiti na kuzuia maambukizi mapya katika jamii”.

Vilevile Waziri Ummy amewahakikishia  watanzania na jamii ya Kimataifa kuwa Tanzania ni salama hivyo wananchi waendelee na shughuli na safari bila hofu yeyote na kwamba serikali bado inahimiza wananchi wote hasa wa mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua tahadhari kudhibiti ugonjwa na kuzuia maambukizi mapya katika jamii.

No comments