HEADER AD

HEADER AD

MTANGAZAJI KBC : SIJAWAHI KUFIKA TANZANIA ITAKUWA FURSA KUTANGAZA UTALII MARA

Na Dinna Maningo, Mara

MTANGAZAJI katika Shirika la Utangazaji la Serikali ya nchi ya Kenya (KBC) Joyce Kahiga ameipongeza Kampuni Binafsi ya Utalii Awesome Expedition yenye makao yake makuu mkoani Arusha, nchini Tanzania kwa kumpatia mwaliko kushiriki kongamano la kuhamasisha Utalii wa mkoa wa Mara.

Akizungumza na DIMA Online Joyce amesema hajawahi kufika nchi ya Tanzania na kwamba fursa aliyoipata ataitumia vyema kutangaza Utalii wa mkoa wa Mara kupitia chombo cha habari cha KBC.

      Mtangazaji katika Shirika la Utangazaji la Serikali ya Kenya (KBC) Joyce Kahiga 

"Mimi ni mtangazaji na mwandaaji wa vipindi Shirika la Utangazaji la Serikali ya Kenya KBC, sijawahi kufika Tanzania wala kufanya ziara yoyote na sijawahi kutembelea hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Hii itakuwa ziara ya kwanza kabisa, nitaweza kuandaa habari za kuangazia mkoa wa Mara kwa lengo na kuhamasisha umma kutembelea vivutio vya Mara."amesema Joyce.

Mtangazaji huyo nchini Kenya ameongeza kusema "Nina matarajio mengi sana ikizingatiwa kwamba ni mara yangu ya kwanza kuzuru Tanzania. 

"Nataka nilinganishe wanyama walioko katika mbuga za Kenya na zile za Tanzania. Watanzania mpoo? Na Jaja Jaja kutalii nanyi mbugani Mara" amesema Joyce.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu ya Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy kutoka Kampuni Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition amesema kampuni inaandaa Kongamano la kuhamasisha Utalii.

Amesema Kongamano hilo lijulikanalo Awoke International Sports Tourism Conference and Expo litafanyika Mei,22-28, 2023 mjini Musoma mkoani Mara.

                Buchebuche Enosy

Amesema mpango huo wa uhamasishaji wa Utalii utakwenda sambamba na Mkutano wa Kimataifa,maonesho ya biashara na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Kutakuwa na mkutano wa Kimataifa        (International Conference)  utakaofanyika ukumbi wa NHC Mukendo Plaz, tunategemea kuwa na wageni 350 utakaofanyika kwa siku tatu, tarehe 23/05/2023 hadi 25/05/2023.

"Zitajadiliwa mada sita ambazo zitahusu  Safari, Michezo na Burudani (Travelling for businesses, Sports and Leisure),Utalii (Ecotourism), Mitumbwi ya makasia (Canoeing), Kutembea kwa miguu (Trekking), Matamasha ya asili (Cultural Festivals) na Mchezo wa kuvua samaki (Sport Fishing).

"Baada ya nadharia kutafanyika vitendo kutokana na mada zilizotajwa ambavyo vitahamasisha utalii zaidi baada ya kumalizika kwa kongamano. Pia Mei, 26-28/2023 kutafanyika Bush Party Serengeti National Park kisha kutoka hifadhini na kurudi kufunga maonesho"amesema Buchebuche.

Buchebuche ameongeza kusema kuwa maonesho ya biashara (Business Expo) yatafanyika kwa siku nane ambapo Wajasiriamali na Wafanyabiashara mbalimbali wataweza kuonesha na kuuza bidhaa zao.

Ameongeza kuwa Waandishi wa habari wa mkoa wa Mara nchini Tanzania kwa kushirikiana na Waandishi wa Habari kutoka nchi 24 ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Ghana, Uturuki, USA, Canada, India na Israel kupitia vyombo vyao vya habari wataripoti habari kuhamasisha utalii yakiwemo maonesho ya bidhaa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Waandishi hao wa Habari wataripoti habari na kuandaa vipindi na makala na kuvirusha katika vyombo vyao vya habari katika nchi zao kwa lengo la kutangaza vivutio vya mkoa wa Mara ili kuwavutia watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kufanya utalii mkoani Mara sambamba na kuitembelea hifadhi ya Serengeti.

Buchebuche amesema mpango huo umelenga kuhamasisha utalii na kwamba ni wa kwanza kuanzishwa Afrika ya Mashariki utakayoanzia mkoa wa Mara.
Buchebuche amewaomba wananchi wa Mara kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mukendo kuona maendeleo ya utalii na sanaa mbalimbali kwani kutakuwepo na bidhaa nyingi za kuuza na kuuza.





No comments