HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WATUMIA MAJI YASIYO SAFI NA SALAMA


Na Dinna Maningo, Tarime 

WANANCHI wa Mtaa wa Nyakihenene Kata ya Nyandoto wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wanatumia maji ya mto Kigera yasiyo safi na salama hali ambayo ni hatari kwa afya zao.

Wakizungumza na DIMA Online katika mtaa huo wamesema kuwa maji wanayotumia si safi na salama kwakuwa wakati wa mvua maji hutiririka katika mto huo yanayotoka mgodi wa uchenjuaji wa dhahabu uliopo katika mtaa huo.

Rhobi Ryoba amesema wananchi wanatumia maji ya mto yasiyo safi ambapo huchangia na mifugo huku baadhi yao wakitembea umbali wa km.3 kutafuta maji ya kunywa kwenye visima vya watu binafsi.


"Tuko jirani na migodi ya kuosha mchanga wenye dhahabu, (Seneti)wakati wa mvua maji yanatiririka kutoka mgodini na kuingia mtoni. Maji haya tunatumia kufua na kupikia na wengine wanakunywa.

"Ukitaka maji ya kunywa au ya bomba mpaka utembee kilomita 3 kuyatafuta. Zaidi ya Kaya 50 kwenye huu mtaa zinategemea maji kwenye huu mto Kigera ambayo siyo safi na salama" amesema Rhobi.


Rose Magesa ameiomba Serikali kuwapatia huduma ya maji ya bomba safi na salama, tunatumia maji machafu yanatotoka mgodini.

"Watu wa mgodi hawajali afya zetu kwakuwa mabosi wa hiyo migodi ni Wakenya na wakati huohuo tunachangia na mifugo inajisaidia mtoni pindi inapokunywa maji.


"Wakati mwingine tunafuata maji shuleni na yanakosa, haya maji ya mtoni asubuhi unaweza kuyaona masafi lakini ikifika mchana ni tope maana ng'ombe wanakuja kunywa maji, na siyo maji tu hata umeme hatuna tunatembea km.5 kwenda kusaga unga.

Mwenyekiti wa mtaa wa Nyakihenene Thomas Jovinalis  amesema mtaa huo una kaya zaidi ya 300 na una watu zaidi ya 900 na kwamba migodi hiyo imezunguka kwenye makazi ya wanachi ambapo wakati wa mvua maji hutiririka hadi mtoni.


"Kaya zaidi ya 70 hazijanufaika na mradi wa maji safi na salama wa Gamasara,tukiuliza wanasema tuendelee kuvumilia kwamba maji yatakuja kutoka ziwa Victoria, tunaomba na sisi wananchi kwakuwa tupo ndani ya Halmshauri ya mji Tarime tupate maji kama wananchi wengine " amesema Thomas.


DIMA Online ikafia hadi ofisi ya Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tarime kufahamu sababu ya wanamtaa huo kutokuwa na maji ya bomba licha ya kuwepo mradi wa maji  Gamasara unaotoa huduma ya maji kwa baadhi ya wanamtaa huo na mitaa jirani.


Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira wilaya ya Tarime, Mhandisi Malando Masheku amesema Tayari kuna mradi mpya wa maji wa Itununu, Nyakihenene na Mnagusi utakaonufaisha wananchi wa mitaa hiyo mitatu.

Amesema mradi huo utagharimu  kiasi cha zaidi ya Tsh. Milioni 453.568 na upo hatua ya asilimia 30 na kwamba unatarajia kukamilika Septemba, 2023.


"Tenki litakuwa na ujazo wa lita laki moja, ujenzi wa mradi umeshaanza tayari vituo vitatu vimeshakamilika,  mradi utanufaisha wananchi wa Mtaa wa Itununu, Nyakihenene na Mnagusi.

Meneja huyo amesema changamoto iliyopo inayochelewesha mradi ni mvua kwakuwa zinaponyesha inabidi mafunzi wasifanye kazi na kwamba mradi una vituo 10.









No comments