HEADER AD

HEADER AD

MWALIMU NATTA SEC. KUMLIPIA NAULI YA NDEGE MWANAFUNZI

 

>>Aahidi Neema kwa wanafunzi

>>Mbunge awaomba wazazi kuwamotisha walimu

>>Wanafunzi waiomba Serikali kujenga uzio

Na Mwandishi Wetu, Serengeti

MKUU wa shule ya Sekondari Natta Mwl. Mwema Warioba ameahidi kumlipia nauli ya usafiri wa ndege mwanafunzi Bahati A. Jumamne katika chuo chochote atakachopangiwa kujiunga pindi atakapofaulu mtihani wa kuhitimu kidato cha sita.

Mkuu huyo ameyasema hayo wakati wa mahafali ya 11 ya kidato cha sita ambapo jumla ya wanafunzi 111 wanatarajia kufanya mtihani utakaoanza Mei, 02, 2023.


"Mimi binafsi nitatoa tiketi moja ya ndege ya kwenda na kurudi (go and return) kwa mwanafunzi aliyekuwa bora katika taaluma kwa kipindi chote BAHATI A. JUMANNE kwenda katika chuo chochote atakachopangiwa hapa nchini.

"Wanafunzi watano watakaopata division one ya point 3 na 4 tutawalipia gharama za hosteli(accomodation)kwa mwaka mmoja kwa kila mmoja akiwa chuoni" amesema mkuu huyo.

Mwema Warioba, ametoa wito kwa wanafunzi hao katika kuelekea mitihani yao ya mwisho kuzingatia waliyofundishwa na kuelekezwa na walimu wao kuhakikisha wanafanya vizuri katika mtihani wao wa kuhitimu kidato cha sita.

"Naomba kila mmoja wenu azingatie tuliyowafundisheni na asome kwa bidii na kuhakikisha anafanya vizuri katika mitihani hii ya mwisho kama tulivyokubaliana"amesema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Serengeti Amsebi Mrimi amewahimiza wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kutoa  motisha ama zawadi kwa walimu kutokana na kazi yao ya ufundishaji na malezi kwa vijana wawapo shuleni.


Amsebi aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mahafari hayo amesema zawadi hizo zitawatia moyo kuzidi kuongeza juhudi katika ufundishaji.

"Nawapongeza wahitimu na walimu kwa juhudi kubwa walizofanya hadi kufikia hatua hiyo, niwaombe wazazi na walezi wa wanafunzi kuwa na utamaduni wa kutoa motisha ama zawadi kwa walimu ili kuwapongeza na kuwatia moyo katika kazi yao njema ya ufundishaji na malezi kwa vijana wao.

"Hii itachochea walimu kuzidi kufanya vizuri ili shule ya Natta iendelee kufanya vizuri zaidi katika taaluma.Tunapokutana katika sherehe kama hizi wakati mwingine  bebeni zawadi kwa ajili kuwapongeza  walimu ili wapate motisha ya kufanya vizuri zaidi''amesema Amsebi.

Mbunge huyo ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kufanya vizuri katika utawala na matokeo ya mitihani ya kitaifa ambapo kwa matokeo ya mwaka jana 2022 shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kati ya shule 22  kimkoa na nafasi ya 11 kati ya shule 644 kitaifa.


Pia, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawanunulia vitabu watoto wao na kuwapa muda wa kutosha wa kusoma ili waweze kupata maarifa, ujuzi na wafaulu katika masomo yao. Amewataka wanafunzi hao kumtanguliza Mungu katika masomo na mitihani yao yote.

Mkuu huyo wa shule ya Natta Mwl. Mwema ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupatiwa fedha jumla ya Tsh. 80,000,000.


Amesema fedha hizo zimetumika kuboresha miundombinu katika shule hiyo kwa kujenga madarasa manne kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita hali ambayo imepunguza mrundikano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa. 

Kwa upande wa wahitimu, wameushukuru uongozi wa shule kwa namna ilivyowajali katika kuwahudumia na kuwapa elimu bora kwa kipindi chote walichokuwa shuleni na kuahidi kufanya vizuri zaidi katika mitihani  yao ya Taifa. 

Pia wametoa wito kwa serikali kuisaidia shule kwa kujenga uzio katika shule hiyo kutokana na hatari mbalimbali zinazojitokeza mara kadhaa ikiwemo kuvamiwa na wanyama wakali pamoja na vibaka wanaohatarisha usalama wa wanafunzi na mali za umma.







No comments