HEADER AD

HEADER AD

ONGEZEKO BAJETI YA MATENGENEZO ILIVYOPUNGUZA KERO ZA BARABARA TARIME TC

>>Kutoka Milioni 729 hadi Bilioni 2.209

>>Barabara zajengwa,Madaraja, Vivuko, Mitaro

Na Dinna Maningo, Tarime

MENEJA Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha katika bajeti ya matengenezo ya barabara.

Akizungumza na DIMA Online ofisi ya TARURA, Mhandishi Charles amesema katika uongozi wa Rais Samia Halmashauri ya Mji Tarime katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilitengewa bajeti ya matengenezo ya barabara Tsh. Bilioni 2.209.

Amesema bajeti hiyo ni ongezeko la zaidi ya mara tatu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha Tsh. Milioni 729  hali ambayo imesaidia kuwapunguzia wananchi kero za barabara.

   Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa

"Awali Halmashauri ya Mji Tarime tulikuwa tunapata bajeti ya mwaka ya Matengenezo kati ya Milioni 500 hadi 729, lakini tangu mwaka wa fedha 2021-2023 bajeti iliongezeka hadi kufika Bilioni 2.209 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

" Utaona bajeti hiyo ni zaidi ya mara tatu ya Milioni 729 ya mwaka wa fedha 2020/2021. Dhamira ya Rais Dkt Samia ni kuhakikisha kero za barabara zinatatuliwa lakini pia kuhakikisha kila mwananchi anaweza kutoka nyumbani kwakwe na kwenda sehemu za uzalishaji mali na huduma za jamii bila shida" amesema Meneja TARURA.

Bajeti hiyo ya matengeneze ya barabara ni kutoka katika vyanzo vitatu ambavyo ni fedha ya tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti ambayo ni makato ya Tsh. 100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli kiasi cha Tsh. Bilioni moja.


Fedha ya Jimbo la uchaguzi Tsh. Milioni 500 na fedha kutoka mfuko wa barabara kiasi cha zaidi ya Milioni 700 na kwamba hadi kufikia Machi, 2023 TARURA imepokea fedha Bilioni 1.295 sawa na asilimia 58.6 ambapo matengenezo hadi mwezi huo yamefikia asilimia 91.3.

Charles amesema kupitia bajeti hiyo zimefunguliwa barabara mpya zenye  jumla ya km 18.76 zenye urefu wa kati ya mita 300-500 katika maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki.

"Barabara zimefunguliwa katika maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki kama kule mtaa wa uwanja wa ndege,Nyamisangura, Turwa, Kenyamanyori,Nyandoto, Nkende, kila Kata ilipata barabara mpya ambayo imefunguliwa"amesema Charles.

Amesema zimetengenezwa barabara  km 15.4 kwa kiwango cha changarawe, na madaraja mawili la Nkongore lililojengwa kwa gharama ya Tsh. Milioni 675  na lingine linajengwa Kinyambi litakalogharimu Tsh. Milioni 546 lenye urefu wa mita 21.


"Tumetengeneza kwa changarawe zenye ubora tulikuwa tunatoa kule Gamasara, lengo kumwezesha
 mwanachi aweze kupita kwa urahisi anapokuwa katika shughuli zake za uzalishaji na huduma za jamii" amesema Meneja.

Pia Vivuko/Karavati 24 vimejengwa pamoja na Mitaro ya maji ya mvua yenye jumla ya urefu wa mita 1,900 sawa na km 1.9 pamoja na ukarabati wa barabara za udongo jumla km 145.02  Kata mbalimbali katika Halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kokehogoma Musa Nehemia ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha barabara ikiwemo ujenzi wa vivuko katika mtaa huo.

   Mwenyekiti wa Mtaa wa Kokehogoma Musa Nehemia

"Naipongeza Serikali na TARURA kwa kutuboreshea barabara, mtaani kwangu barabara ilikuwa na changamoto walipoweka karavati changamoto ya tope barabarani imepungua kwasababu mvua iliponyesha maji yalijaa katikati ya barabara na kuleta usumbufu kwa watumia barabara.

Mwendesha pikipiki Lucus Marwa mkazi wa Mtaa wa Rebu Senta ameipongeza TARURA kwa kuendelea kutengeneza barabara na kuweka vivuko jambo ambalo limewapunguzia usumbufu wanapokuwa kwenye shughuli zao za kusafirisha abilia na mizigo.













No comments