HEADER AD

HEADER AD

MWANDISHI : WAKONGOMANI WANAOFIKA TANZANIA WENGI HAWAFAHAMU VIVUTIO VILIVYOPO MIKOANI


Na Dinna Maningo, Mara

MWANDISHI wa Habari wa Redio ya Kijamii Kivu Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Lokendo Tenchi Luc amesema raia wengi wanaoishi Mashariki DRC wanatembelea nchi ya Tanzania lakini hawajui vivutio vilivyopo katika mikoa mbalimbali.

Akizungumza na DIMA Online, Lokendo amesema raia wa Congo hasa wanaoishi Mashariki mwa nchi hiyo wamekuwa wakiitembelea Tanzania lakini baadhi yao hawajapata elimu ya umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mikoa mbalimbali ya Tanzania.

     Mwandishi wa Habari wa Redio ya Kijamii Kivu Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Lokendo Tenchi Luc 

Amesema mwaliko alioupata kutoka Kampuni Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition kwa ajili ya kufika nchini humo katika mkoa wa Mara kuhamasisha Utalii, kongamano litakalofanyika Mei, 22,2023 mjini Musoma ni nafasi kwa wakongomani kujua vivutio vya mkoa huo.

"Raia wengi wa DRC hasa hawa wanaoishi Mashariki wengi wanatembelea Tanzania lakini wamekuwa hawajui mengi katika mikoa tofauti tofauti ya Tanzania.

"Wengi wanaishia Kigoma au Dar es Salaam, lakini suala la kufanya utalii kutembelea vivutio vya nchi hiyo wengi hawafanyi hivyo. Kupitia ziara hiyo nitakayoshiriki nitajitahidi niwape ujumbe wakongomani" amesema.

Lokendo ameongeza kusema " Nitawaambia wajue kile kinachoendelea nchini Tanzania hasa kuhusu hifadhi walizonazo kama hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara.

"Itakuwa ni fursa kwa wakongomani kujua mengi kupitia habari nitakazoripoti za uhamasishaji wa Utalii wa mkoa wa Mara katika chombo changu cha habari nchini Congo" amesema Lokendo.

Ameongeza kuwa fursa hiyo iliyoandaliwa na Awesome Expedition itaisaidia Tanzania kutangaza vivutio vyake kimataifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi.

Mwandishi huyo wa habari amesema alishafika nchini Tanzania lakini hajawahi kufika mkoa wa Mara wala kufanya utalii wa kutembelea hifadhi yoyote ya Taifa katika nchi hiyo.

"Nilishatembelea nchi ya Tanzania nimetembelea hasa mkoa wa Kigoma, Kagera, Mwanza na Dar es Salaam, nimefika huko kwa kazi za uandishi wa habari kwasababu mimi naripotia pia redio Kwizera FM ya Ngara iliyopo nchini  humo kama ripota wao kutoka DRC.

"Sijawahi kufanya utalii Tanzania, hii itakuwa mara yangu ya kwanza na sijawahi kufika mkoa wa Mara, endapo nikifika ndiyo itakuwa mara yangu ya kwanza kwasababu huwa napita tu nikiwa kwenye gari wakati naenda Nairobi, nina hamu kubwa na nitanufaika na mengi" amesema.

Ameishukuru Kampuni ya Utalii ya Awesome Expedition "Nawashukuru sana kwa kuweza kunialika kuwa miongoni mwa waandishi wa habari watakaokuja kuripoti matukio ya Utalii ikiwemo mbuga ya Serengeti.

"Nawashukuru waandalizi wa tukio hili ambao wamenifikiria wakasema na mimi niweze kujumuika pamoja na wengine. Mungu awaongoze kwasababu haya ni mambo muhimu ambayo watu wanatakiwa kuyajua na kuyaona" amesema Lokendo.

"les habitants de la province de Mara vous êtes là ? Nous serons ensemble à Musoma pour la sensibilisation touristique de Mara"
" Watu wa Mara mpooo? Tutakuwa pamoja Musoma kuhamasisha Utalii Mara."amesema Lokendo.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu ya Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy kutoka Kampuni Binafsi ya Utalii ya Awesome Expedition amesema kampuni inaandaa Kongamano la kuhamasisha Utalii lijulikanalo Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, litakalofanyika Mei,22-28, 2023 mjini Musoma mkoani Mara.

     Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu ya Awoke International Sports Tourism Conference and Expo, Buchebuche Enosy

Amesema mpango huo wa uhamasishaji wa Utalii utakwenda sambamba na Mkutano wa Kimataifa,maonesho ya biashara na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Kutakuwa na mkutano wa Kimataifa  (International Conference)  utakaofanyika ukumbi wa NHC Mukendo Plaz, tunategemea kuwa na wageni 350 utakaofanyika kwa siku tatu, tarehe 23/05/2023 hadi 25/05/2023.

"Zitajadiliwa mada sita ambazo zitahusu  Safari, Michezo na Burudani (Travelling for businesses, Sports and Leisure),Utalii (Ecotourism), Mitumbwi ya makasia (Canoeing), Kutembea kwa miguu (Trekking), Matamasha ya asili (Cultural Festivals) na Mchezo wa kuvua samaki (Sport Fishing).

"Baada ya nadharia kutafanyika vitendo kutokana na mada zilizotajwa ambavyo vitahamasisha utalii zaidi baada ya kumalizika kwa kongamano. Pia Mei, 26-28/2023 kutafanyika Bush Party Serengeti National Park kisha kutoka hifadhini na kurudi kufunga maonesho"amesema Buchebuche.

Buchebuche ameongeza kusema kuwa maonesho ya biashara (Business Expo) yatafanyika kwa siku nane ambapo Wajasiriamali na Wafanyabiashara mbalimbali wataweza kuonesha na kuuza bidhaa zao.

Ameongeza kuwa Waandishi wa habari wa mkoa wa Mara nchini Tanzania kwa kushirikiana na Waandishi wa Habari kutoka nchi 24 ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Ghana, Uturuki, USA, Canada, India na Israel kupitia vyombo vyao vya habari wataripoti habari kuhamasisha utalii yakiwemo maonesho ya bidhaa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Waandishi hao wa Habari wataripoti habari na kuandaa vipindi na makala na kuvirusha katika vyombo vyao vya habari katika nchi zao kwa lengo la kutangaza vivutio vya mkoa wa Mara ili kuwavutia watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kufanya utalii mkoani Mara sambamba na kuitembelea hifadhi ya Serengeti.

Buchebuche amesema mpango huo umelenga kuhamasisha utalii na kwamba ni wa kwanza kuanzishwa Afrika ya Mashariki utakayoanzia mkoa wa Mara.
Buchebuche amewaomba wananchi wa Mara kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mukendo kuona maendeleo ya utalii na sanaa mbalimbali kwani kutakuwepo na bidhaa nyingi za kuuza na kuuza.




No comments