HEADER AD

HEADER AD

SHUHUDA: ASKARI ALIOMBA 300,000 ALIPONYIMWA AKAMPIGA RISASI

>>>Mashuhuda wasema chanzo cha kupigwa risasi ni askari kunyimwa rushwa ya 300,000

>>>Askari mbaroni kwa mauaji

Na Dinna Maningo, Tarime

MASHUHUDA ambao ni waendesha pikipiki walioshuhudia tukio la mwenzao Ng'ondi Marwa Masiaga kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi mwenye namba H. 4489 PC KULULETELA wa Kituo cha Polisi Sirari,Wilaya ya Tarime mkoani Mara na kumsababishia kifo, wameeleza kuwa chanzo cha tukio ni rushwa ya 300,000.

Mashuhuda wameeleza kuwa marehemu alikuwa akisafirisha saruji mifuko mitano aliyokuwa amekwenda kununua nchi jirani ya Kenya na kisha askari huyo kumpiga risasi mbili katika mwili wake na kumjeruhi ambapo alipoteza maisha akiwa anapatiwa matibabu hospitali ya wilaya ya Tarime.

Mwendesha pikipiki mfanyabiashara jina lake limehifadhiwa aliyekuwa eneo la tukio lililotokea Machi, 31,2023 majira ya saa mbili asubuhi katika kijiji cha Kubiterere Kata ya Mwema, amesema sababu ya marehemu kupigwa risasi ni baada ya kukataa kumpatia askari huyo Tsh. 300,000 kama rushwa ili aweze kusafirisha saruji alizokuwa amebeba kwenye pikipiki akizitoa nchi jirani ya Kenya kama anavyosimulia.

"Chanzo ilikuwa ni pesa tulikuwa eneo la Kumumwamu Kijiji cha Kubiterere eneo ambalo limepkana na nchi jirani na Kenya tulienda kununua saruji ya Kenya kwa ajili ya kujitafutia riziki,Polisi alimfosi marehemu atoe pesa Tsh. 300,000 alikuwa amebeba Ciment ya Kenya (Saruji) mifuko mitano yenye thamani ya pesa ya Tanzania Tsh. 65,000.

" Marehemu akamwambia hiyo pesa hana aliyokuwa nayo amenunua mzigo, yule Polisi akajifanya kama anarudi nyuma akamwambia bila laki tatu haondoki mtu, marehemu akasema ngoja nirudishe mzigo nilikonunua"anasema.

Anaongeza" Polisi akamsukuma marehemu akaanguka chini ile anataka aamke akampiga risasi hajakaa sawa akampiga risasi nyingine, tulipojaribu kumchukua ili tumuwahishe hospitali,huyo Polisi akawa ameelekeza silaha mbele yetu akasema atakayesogea nampiga risasi.

"Tulioshuhudia tukio tulikuwa watatu, Polisi walikuwa wawili ila aliyefanya tukio alikuwa huyo mmoja, wananchi ambao ni majirani wakasogea maana ni eneo la wazi, tukamchukua na kumkimbiza hospitali ya wilaya Tarime.

"Polisi huwa wanatabia ya kuomba sh. 2,000 kwa kila pikipiki, sasa kwa bodaboda mgeni huwa wanaombwa kiwango zaidi kulingana na utakavyojirahisi" anasema shuhuda.

Shuhuda wa pili anasema kuwa marehemu alipigwa risasi baada ya kushindwa kumlipa askari aliyemuomba  sh.300,000 ili amwachie mzigo wake wa saruji tano alizokuwa amebeba kwenye pikipiki.

"Wakati tunaenda kununua saruji askari Polisi huwa wanatutaka tuwape pesa ndiyo tuvuke mpaka kuingia kumumwamu upande wa Kenya kununua saruji sasa kila mtu hulipa fedha kulingana na makubaliano yenu.

"Wakati tunaenda tulikuwa bodaboda watano tulipofika mpakani kumumwamu upande wa Tanzania askari kama kawaida yao huwa wanakuwa eneo hilo,walikuwepo askari wawili wakatuomba pesa tukawabembeleza tukawapa elfu 10,000 kila mmoja akatoa 2,000"anasema shuhuda.

Shuhuda huyo anaongeza" mwenzangu atakuwa alijisahau hatukuwa watatu tulikuwa watano, tukaingia kumumwamu upande wa Kenya tukanunua saruji wakati tunarudi tumeshaingia kumumwamu upande wa Tanzania hao polisi wakamsimamisha tena marehemu wakamuomba laki tatu vinginevyo wachukue pikipiki waipeleke TRA.

"Wakamkamata, marehemu aliwaambia hana pesa aliwabembeleza sana wamwachie lakini wakamkatalia wakikomalia wapewe laki tatu. Mimi nikambembeleza huyo askari anaitwa Samwel nikamwambia muache kwakuwa umemwambia ngoja aende atafute pesa alafu atakuletea" anasema.

Anaongeza kusema "Akakataa wakaanza kuvutana kuhusu pesa, Marehemu akawa anataka aokoe pikipiki ili akimbie nayo wakati wanavutana pikipiki askari Samwel akamwambia nitakupiga risasi, sisi tukafikiri masiala unajua akampiga risasi tunashuhudia kwa macho akampiga tena risasi ya pili.

"Wakiwa wametusonteshea silaha askari hao wakatuambia rudi nyuma hatua tano la sivyo nawapiga risasi, kwakuwa watu walisikia mlio wa risasi wakasogea karibu, wakati tunataka kumbeba ili tumuwahishe hospitali hao Polisi wakasema mwacheni gari linakuja kumbeba.

"Nikakataa nikasema tumbebe kwa pikipiki tumuwahishe hospitali askari wakazuia nikakataa wakasema tutakupiga risasi nikasema niueni tukalazimisha tukamchukua akiwa na hali mbaya akivuja damu nyingi tukamsafirisha kwa pikipiki tukampeleka hospitali akafariki akiwa hospitali.

" Amefariki kwasababu yakuchelewa kupelekwa hospitali endapo ule ule muda aliopigwa risasi askari wasingetuzuia huwenda angefika kupona maana alikuwa anavuja damu nyingi"anasema.

Shuhuda huyo anasema kwamba ni kawaida askari hao wa Kituo cha Polisi Sirari kuomba fedha na wanapokamata pikipiki wanawaamuru kuwapa sh. 300,000 kama fedha ya kukomboa pikipiki hivyo waendesha pikipiki hulazimika kuwapa ili kunusuru pikipiki zao zisifikishwe TRA kwakuwa ikifika huko ili uikomboe utozwa Tsh. 800,000.

"Hao askari walikuwa lindo la usiku kabla hawajarudi kazini hukaa pale kumumwamu ili wajipatie fedha kutoka kwa waendesha pikipiki wanaofuata saruji Kenya, tukio lilifanyika mida ya saa 2:35 asubuhi.

"Wakikukamata na pikipiki wanakuomba 300,000 ukikataa wanakwambia chagua moja utoe laki tatu uachiwe pikipiki au tuichukue tuipeleke TRA ukaikomboe kwa 800,000? ,unaona bora uwape laki tatu uokoe hiyo pesa nyingine uendelee na shughuli zako.

"Kama huna pesa utalazimika utafute namna uwakimbie ili uokoe pikipiki ukizingatia ndiyo chanzo kinachokuingizia pesa na familia inakutegemea, unaona ikikamatwa kuikomboa ni milolongo mirefu sana na bado utapelekwa mahakamani na ikichukuliwa kuipata itachukua muda sana utapoteza kazi na familia inataka ipate mlo na mahitaji mengine" anasema shuhuda.

Anaongeza" Askari wote wawili walikuwa na silaha ila aliyefanya tukio ni huyo Samwel, Marehemu amepigwa risasi mbili na maganda ya risasi yalikuwa mawili Polisi hao wakayachukua.

"Hao Polisi ni waonevu sana huwa wanatembea na mipini ya jembe walishampiga hata bodaboda mmoja wa Sirari wakamtoa meno, Polisi wa Kituo cha Sirari walishawageuza bodaboda wa saruji kama mtaji wao.

Mke wa Marehemu amlilia mmewe

Akizungumza kwa majonzi Jesca Maridadi mwenye umri wa miaka 17 anasema mmewe amemwacha akiwa na mtoto mmoja wa mwaka mmoja.

"Nimeambiwa saa tatu asubuhi, baba mkwe alinipigia simu tukiwa nyumbani, mme wangu Thomas Marwa Masiaga ana miaka 19, alikuwa ni tegemeo langu sina kazi, maisha yetu ni magumu, wao wamezaliwa watoto 7 wamebaki sita wakiume watatu na wakike watatu, ameniacha na mtoto mmoja wa mwaka mmoja.

"Ameacha baba na mama, alikuwa anafanya kazi ya kufuata mazigizaga (bidhaa mbalimbali) Sirari anakuja kuuza tunapata chakula, Polisi wameniulia mme nitaishije na yeye ndiyo alikuwa tegemeo langu ameniacha na mtoto mdogo" anasema Jesca huku akilia.

Polisi watakiwa kugharamia mazishi

Mwenyekiti wa mtaa wa Regoryo Yomed Mekere Nyeitange anawataka Askari wa Jeshi la Polisi kutojichukulia sheria mkononi kwakuwa anaamini wamejifunza maadili ya kazi na kusimamia sheria za nchi.
       Mwenyekiti wa mtaa wa Regoryo Yomed Mekere Nyeitange

Pia amelitaka Jeshi hilo kugharamia mazishi kwakuwa askari wa jeshi hilo amekatisha maisha ya mwananchi mwake huku akiipa pole familia na ndugu katika kipindi hicho kigumu cha kuondokewa na ndugu yao.

"Marehemu ni mwanamtaa wangu alikuwa anajitafutia maisha askari akampiga risasi iliyopelekea kifo, nimewahoji walioshuhudia tukio wamesema Polisi walimuomba marehemu 300,000. Hao askari wakawaambia wenzake nyie piteni huyu abaki, askari akamwambia bila laki tatu hutoki hapa, aliposema hana akamshuti risasi mbili.

"Alitolewa pale akiwa anapumua amefia hospitali akipatiwa matibabu, mimi nilikuwa kwenye shughuli zangu za mtaa mwananchi mmoja akanipigia simu nikaenda hospitali nikakuta ndugu wanalia"anasema.

Anaongeza " Nikawaambia tuandamane hadi kwa mkuu wa Wilaya tukaenda hatukumkuta tukawakuta wasaidizi wake wakasema poleni wakasema watashughulikia, tukaondoka na baba wa marehemu kwenda Kanda maalum RCO akapigiwa simu akasema yupo kwenye eneo la tukio.

"Tulimuomba RPC watuchangie fedha tukasema hatuna hata jeneza, fedha za kuendesha msiba, RCO alifika tukamuona akatuahidi kwamba watasimamia kitakachopatikana japo hakusema wazi kitakachopatikana nini!, kesho tunarudi (leo) hospitali kwa ajili ya mwili kufanyiwa uchunguzi" anasema Yomed.

"Wakati wa tukio bodaboda wenzake walifanikiwa kuchukua pikipiki yake wakaondoka nayo ila baadae Polisi walihitaji ipelekwe kituo cha Polisi kama kielelezo wakasema waichukue taarifa wakimaliza watairudisha ili ikasaidie usafiri siku ikihitajika mahakamani ipelekwe, kwahiyo bado wanayo ila saruji wananchi walifanya unyang'anyi wakazichukua"anasema Mwenyekiti.

Mjumbe wa Mtaa wa Regoryo Rozalia Gesero anasema chanzo cha kifo cha Marehemu ni baada ya kupigwa risasi iliyopelekea kifo huku akilaani kitendo hicho cha Polisi kujichukulia sheria mkononi kupoteza maisha ya vijana.

Katibu wa Waendesha Pikipiki (Bodaboda) wilaya ya Tarime Dickson Christopher ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Kata ya Turwa amelaani kitendo cha askari Polisi kujichukulia sheria mkononi huku akiomba mtuhumiwa awajibishwe kama watuhumiwa wengine.

      Katibu wa Waendesha Pikipiki (Bodaboda) wilaya ya Tarime Dickson Christopher

Askari aliyeua akamatwa na kupelekwa mahabusu ya Polisi 

JESHI la Polisi mkoa wa Polisi Tarime, Rorya linamshikilia askari Polisi namba H. 4489 PC KULULETELA wa Kituo cha Polisi Sirari kwa kosa la kumfyatulia risasi na kumjeruhi mwendesha pikipiki (Bodaboda) Ng'ondi Marwa Masiaga na kumsababishia kifo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime, Rorya ACP Geofrey Sarakikya amesema tukio hilo limetokea majira ya saa mbili asubuhi, Machi, 31,2023 katika Kitongoji cha Nyansisine Kijiji cha Kubiterere Kata ya Kubiterere.

     Kamanda wa Polisi mkoa wa Polisi Tarime, Rorya ACP Geofrey Sarakikya

Kamanda ACP Sarakikya amesema Marehemu mwenye umri wa miaka 22 mkazi wa mtaa wa Regoryo Kata ya Nkende alifyatuliwa risasi na askari huyo kwenye paja la kulia na kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Tarime.

"Marehemu alikuwa ni mfanyabiashara bodaboda, askari kwa uzembe wake mwenyewe alimfyatulia risasi kijana huyo asiyekuwa na hatia, tunamshikilia askari huyo yupo mahabusu Kituo cha Polisi Tarime.

"Huyu ni askari Polisi aliyefunzwa na kufuzu mafunzo ya Polisi yakiwemo matumizi ya silaha, hivyo alichokifanya ni kinyume na Taratibu na sheria za nchi anastahili kuwajibishwa kwa hilo.ndugu wanahabari askari huyo atachukuliwa hatua kama watuhumiwa wengine" amesema Sarakikya.

Kamanda ACP Geofrey Sarakikya amesema mwili wa Marehemu umehifadhiwa hospitali ya wilaya hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.

Saruji ya Kenya inapendwa kwakuwa ni bei poa

Inaelezwa kuwa baadhi ya Waendesha Pikipiki wamekuwa wakifuata saruji nchi jirani ya Kenya na kuiuza nchini kwakuwa bei ni nafuu Tsh. 13,000 kwa mfuko mmoja wa saruji ambapo akiingiza nchini huiuza Tsh. 16,000 ambapo kwa Saruji ya Tanzania huinunua kwa Tsh. 19,000-21,000.

Pia unafuu wa bei ya saruji ya Kenya umewarahisishia maisha wananchi kwakuwa saruji inayouzwa Tarime ni ghari jambo linalosababisha washindwe kumudu gharama na kukimbilia kununua saruji ya Kenya ambayo bodaboda huiuza kwa mwananchi Tsh. 16,000.

No comments