HEADER AD

HEADER AD

WEJISA, DCPC WATOA HUDUMA YA KIJAMII HOSPITALI YA OCEAN ROAD



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

KAMPUNI ya Weka Jiji Safi (WEJISA), Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Dar es salaam (DCPC) Dar Lions Club na wadau wengine wamejumuika kwa pamoja kutoa misaada mbalimbali ya kijamii sambamba na zoezi la ufanyaji usafi katika Hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Zoezi hilo lenye kauli mbiu ya : "Tenganisha Taka, Okoa Mazingira" na Tenganisha Taka, Okoa Rasilimali" limeongozwa na Afisa Tarafa Kata ya Kariakoo,Christina Kalekezi aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewashukuru wadau kwa kujumuika na kufanya shughuli hizo za usafi na kutoa misaada.

"Niwapongeze sana, kwa niaba ya Mkuu wa wilaya, ni kwamba usafi ni ibada, na kufanya usafi hapa hospitali itasaidia wenzetu waliopo hapa kupata hewa safi.

Nitoe wito kwa wananchi wote kuunga mkono masuala yote ya usafi ikwemo kusafisha mazingira, lakini pia kupanda miti kumuunga mkono Rais wetu wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan." Amesema Christian Kalekezi.


Aidha, ameipongeza kampuni hiyo ya WEJISA namna ya kukusanya takataka hizo na namna ya kuzitenganisha.

Naye Mkandarasi wa usafi wa Kata za mjini Kati za Kisutu, Kivukoni na Mchafukoge Meneja Mkuu Mwendeshaji wa Kampuni ya WEJISA Ally Kunambi amesema kuwa kwa sasa kuna kampuni na wadau ambao wanazichukua taka kama fursa za kiuchumi tofauti na kuzipeleka dampo.

"Takataka kwa sasa tunazirejesha katika matumizi mengine ikiwemo mbolea, chakula cha wanyama na matumizi mengine ya viwandani ambapo hali hii inakuwa fursa za kiuchumi hivyo tunatoa elimu namna bora ya kutenganisha takataka hizo ilikuzuia magonjwa ikwemo taka za sindano, bandeji na nyenginezo kutenganishwa na taka tofauti." Amesema Kunambi.

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa DCPC, Fatma Jalala aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Chama hicho, amewakaribisha wadau kuendelea kujitokeza kushirikiana na DCPC katika shughuli za kijamii kwani Wanahabari ni kioo.


"Tunashukuru kujumuika na wenzetu WEJISA,Lions Club na wadau wengine katika zoezi la usafi, kwani Waandishi ni kioo katika Jamii hivyo mbali ya kuripoti matukio, pia tunaweza kufanya kwa vitendo na kuigusa jamii  kama hivi tukishirikiana na wadau" alisema Fatma Jalala.

Zoezi hilo mbali ya usafi  pia wadau wameweza kukabidhi vitu mbalimbali vya misaada kwa uongozi wa Hospitali hiyo sambamba na WEJISA kutoa vyeti vya  kutambua mchango wa wadau hao.



No comments