BILIONI 440 KUTEKELEZA MRADI WA MAJI ZIWA VICTORIA MKOANI SIMIYU
Na Samwel Mwanga,Bariadi
MKOA wa Simiyu unatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria utakaozifikia wilaya zote za mkoa wa Simiyu unaotarajia kugharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 440 hadi kukamilika.
Mradi huo utatekelezwa katika Wilaya za Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu ambapo ukikamilika utaondoka tatizo la upatikanaji wa Maji safi na salama katika mkoa huo.
Hayo yameelezwa Mei, 27, 2023 na Waziri wa Maji Jumaa Aweso mjini Bariadi mara baada ya Serikali kupitia Wizara ya Maji kusaini mkataba wa Tsh. Bilioni 169 na Kampuni ya China Civil Engineering Constraction Cooperatin kwa awamu ya kwanza kwa ajili utekelezaji wa mradi huo.
Waziri wa Maji,Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa mkoa wa Simiyu katika mji wa Bariadi mara baada ya utiwaji wa saini wa ujenzi wa Mradi Mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka katika wilaya zote za mkoa wa Simiyu.
Amesema kuwa Serikali inatambua kwamba mkoa huo asilimia kubwa ya wakazi wake ni wakulima na wafugaji na kwamba watahakikisha mradi huo unatekelezwa ipasavyo ili kuondoa kabisa changamoto za huduma ya maji kwa wananchi na mifugo yao.
"Mkoa wa Simiyu tunafahamu wakazi wake shughuli zao kuu ni kilimo na ufugaji hivyo katika kutekeleza mradi huu tutazingatia pia suala hilo kwa msingi, mifugo itapata maji sambamba na ujenzi wa mabwawa ambayo yatatumika kwenye kilimo cha umwagiliaji,"amesema.
Amesema kuwa kulingana na uhitaji wa maji katika mkoa huo katika utekekezaji wa mradi hakutakuwa na awamu utatekelezwa kwa pamoja ili kuhakikisha dhamira ya Rais Dkt Samia Suluhu ya kumtua mama ndoo kichwani inakamilika.
Baadhi ya Viongozi na wabunge wa Mkoa wa Simiyu wakishuhudia utiaji wa saini kati ya serikali na kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperating kwa ajili ya Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria hadi mkoa wa Simiyu
"Sitaki kusikia mradi huu unatekekezwa kwa awamu tutautekeleza kwa pamoja ili uweze kufika wilaya zote za mkoa wa Simiyu nikuagize Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mama Kemikimba tutafute fedha kwa wadau wetu na kwa Rais ili mradi huende kwa pamoja na ile dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani itimie katika mkoa huu,"amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Maji na Mazingira,Jackson Kiswaga amesema kuwa miongoni mwa miradi mikubwa mitatu inayotekelezwa hapa nchini mmojawapo ni mradi huo.
Mwenyekiti huyo wa Kamati amewaomba wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi.
Baadhi ya Viongozi na wananchi waliohudhiria hafla ya utiaji saini ya Mradi Mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria kupeleka mkoani Simiyu iliyofanyika kwenye viwanja vya Stendi ya Zamani mjini Bariadi.
"Huu ni miongoni mwa miradi mikubwa ya maji hapa nchini inayotekelezwa, hivyo niwaombe wanasimiyu tutoe ushirikiano wa kutosha kwa mkandarasi atakapoanza kazi ili lengo la serikali ya awamu ya sita ya kutoa huduma ya Maji safi na salama kwa wananchi inatimia katika mkoa huo,"amesema.
Ameendelea kueleza kuwa mradi huo umekuwa wa muda mrefu tangu uasisiwe na Rais wa awamu ya tano lakini sasa Rais Samia anakwenda kuutekeleza na kwamba jambo Hilo linadhihirisha dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda amesema kuwa watahakikisha kuwa mkandarasi anafanya kazi zake vizuri bila usumbufu wowote na mkoa huo utampatia ushirikiano wa kutosha.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda akizungumza na wananchi wa mji wa Bariadi mara baada ya kushuhudia utiaji wa saini juu ya utekekezaji wa mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mkoani Simiyu.
Amesema kuwa wananchi wa mkoa huo wanaendelea kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya utekekezaji wa miradi mbalimbali ya maji .
Awali Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki aliomba katika kutekeleza mradi huo ni vizuri ukanufaisha na mifugo iliyopo kwenye mkoa huo na kutaka baadhi ya kazi zitakazotekelezwa ziwanufaishe wakazi wa mkoa huu hasa vijana.
Katika hatua nyingine,Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemteua Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala kuwa msimamizi wa mradi huo sambamba na kuwa mkurugenzi wa mamlaka kubwa ya maji itakayoanzishwa katika mkoa huo mara baada ya mradi huo wa maji kukamilika mwezi Julai mwaka 2025.
Post a Comment