KAMPUNI YA LODHIA KUANZISHA KIWANDA CHA MABATI
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Lodhia ambao ni wazalishaji wa bidhaa za ujenzi hapa nchini inayotengeneza bidhaa za chuma na Plastiki ipo mbioni kuongeza soko la ajira kwa kuanzisha kiwanda kipya cha uzalishaji mabati.
Kampuni hiyo inaendelea kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sera ya uwekezaji.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Lodhia, Sailesh Pandit katika maonesho ya bidhaa za viwandani yaliofanyika kwa siku mbili yakienda sambamba na mkutano wa bodi ya wakandarasi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond jijini Dar es salaam Mei, 25-26, 2023.
Pandit amesema kuwa, Sera nzuri ya uwekezaji imeendelea kuwapa fursa ya kuwa mbioni kuanzisha kiwanda hicho cha mabati ambacho kitaanza kazi mwakani 2024.
"Tunaishukuru Serikali kwa namna inavyoonyesha nia katika miradi mikubwa inayojengwa kutumia bidhaa zetu za ndani.
"Lodhia katika kuongeza ajira nyingine iko mbioni kuanzisha kiwanda cha uzalishaji wa mabati ambayo yatakuwa imara na ya kipekee" amesema Pandit.
Aidha, Pandit ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuthamini na kutumia bidhaa za ndani ili kuleta tija kwa kuongeza ajira na kukuza uchumi.
Pia ameishukuru Serikali kwa namna inavyoonyesha nia katika miradi mikubwa inayojengwa kutumia bidhaa ikiwemo ya kiwanda hicho cha ndani.
Nae Mwenyekiti Msaidizi wa kampuni hiyo ya Lodhia, Mihiri Anand ameiomba Serikali kuharakisha mradi mkubwa wa bwawa la Mwl. Nyerere uliopo Rufiji mkoa wa Pwani ili kusaidi kukabilina na changamoto ya umeme katika uzalishaji utakaosaidia kupunguza gharama katika matumizi ya nishati hiyo.
Mwenyekiti msaidizi wa kampuni ya Lodhia, Mihiri Anand (mwenye shati jeupe) Akizungumza katika tukio hilo
Ameongeza kuwa ongezeko la viwanda mbalimbali hapa nchi litasaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa watanzania sanjari na kuongeza ujuzi ili kujikwamua kiuchumi.
Post a Comment