HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI ZATAKIWA KUTENGA MAENEO YA VIWANJA VYA MPIRA WA KIKAPU


Na Dinna Maningo, Tarime

HALMASHAURI za Manispaa, Miji na Wilaya zimetakiwa kutenga maeneo ya kujenga viwanja vya mpira wa kikapu (Basketball Club) na kutenga bajeti za ujenzi wa viwanja ili kukuza mchezo wa mpira wa kikapu.

Imeelezwa kuwa ukosefu wa viwanja vya mpira wa kikapu ni changamoto kubwa inayokabili mchezo huo na kusababisha Halmashauri hizo kuendelea kubaki nyuma katika mchezo wa mpira wa kikapu.

Akizungumza katika uzinduzi wa ligi ya mpira wa kikapu kimkoa inayofanyika viwanja vya chuo cha ualimu wilayani  Tarime Mei, 28, 2023, Afisa Tarafa ya Inchugu, Zacharia Chambili aliyemwakilisha mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mntenjele amezisistiza halmashauri kutenga maeneo ya kujenga viwanja vya mpira wa kikapu.

  Afisa Tarafa ya Inchugu, Zacharia Chambili akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya Tarime

Afisa huyo amezihimiza halamashauri baada ya Mwenyekiti wa Mpira wa kikapu mkoa wa Mara Sylvanus Gwiboha katika tarifa yake kusema wanakabiliwa na changamoto za viwanja vya mpira wa kikapu katika Halmashauri mbalimbali mkoani humo.

"Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuruhusu mchezo huu wa kikapu katika shule zetu za msingi. Nimshukuru mkuu wa chuo cha ualimu Tarime kwa kukubali timu hizi kushiriki michezo kwenye viwanja vyao".amesema Zacharia.

"Mlimwalika mkuu wa wilaya ya Tarime kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi lakini amepata dharura Waziri wa maliasili na Utalii yupo Tarime wameenda vijijini, yote mliyoyatoa atapokea na kuyafanyia kazi"amesema Zacharia.

         Zacharia Chambili akizindua ligi ya mpira wa Kikapu unaochezwa kimkoa wilayani Tarime

Kuhusu kutokuwepo viwanja vya mpira katika halmashauri zikiwemo za Tarime amesema" Wilaya ya Tarime haina viwanja vingi vya michezo  na kwasababu tuna afisa michezo hapa anayemwakilisha mkurugenzi basi nimtake kwamba wanapokuwa wanatenga bajeti na wanapokuwa wanapima viwanja ebu wakumbuke viwanja vya mpira wa kikapu.

"Mpira wa kikapu ni muhimu sana, Marekani mpira wa kikapu ndio kipaumbele na mnaona maendeleo yalivyo kule Marekani. Kwa hiyo ndugu zangu na sisi tunaomba vijana mnaokua na ninyi mnaocheza mchezo huu muuzingatie ni ajira.

"Msiupende tu kwa sababu ni sehemu ya mazoezi, huu mpira ni ajira nawaomba mfundishe watoto wenu, vijana wenu ili mnapokwenda kupumzika muwe mmewarithisha watoto wenu nao wauendeleze" amesema Zacharia.

Mwenyekiti wa mpira wa kikapu mkoa wa Mara ambaye pia ni afisa kilimo halmashauri ya wilaya Tarime, Sylvanus Gwiboha amesema wanakabiliwa na ukosefu wa viwanja kwa ajili ya kukuza na kuendeleza mpira huo wa kikapu.

Mwenyekiti wa mpira wa kikapu mkoa wa Mara Sylvanus Gwiboha akizungumza

" Viwanja vingi ambavyo timu zetu zinatumia ni viwanja vya taasisi ambavyo vingi vina taratibu na masharti yao. Tunashukuru uongozi wa chuo cha ualimu Tarime na kituo cha matumaini ya vijana Musoma kuendelea kuruhusu vilabu kufanya mazoezi.

" Lakini pia kufanya ligi ya mkoa katika viwanja vyao, tunaomba waendelee kutuvumilia pamoja na mapungufu ya hapa na pale wakati ambao chama mkoa kinaendelea na taratibu za kutafuta wafadhili wa kujenga viwanja, tunawashukuru sana.

Chama cha Mpira mkoa wa Mara (MARBA) kimeziomba Halmashauri za Manispaa, Miji na Wilaya katika mkoa wa Mara kutenga maeneo ya viwanja vya mpira wa kikapu na kutenga bajeti za kutosha kusaidia vilabu vilivyopo katika maeneo yao.


Hata hivyo chama hicho kinaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kuendelea kuweka mazingira mazuri ya michezo kisera nchini. Pia kuhusu kurudishwa mpira wa kikapu kuchezwa ngazi ya shule ya msingi jambo ambalo litaongeza chachu ya ukuaji wa mpira wa kikapu wilaya, Mikoa na Taifa.

Diwani wa Kata ya Regicheri John Bosco ambaye ni mdau wa mpira wa kikapu amewaomba wachezaji kucheza vyema ili kuwapa watu burudani.

      Kushoto ni Diwani wa Kata ya Regicheri John Bosco akiteta jambo na Mwenyekiti wa mpira wa Kikapu mkoa wa Mara Sylvanus Gwiboha

"Mimi ni mdau wa mchezo huu japo kwa sasa umri wangu umeenda siwezi kuruka natamani ningerudi ujana niwe kama ninyi. Niwaombe sana mcheze vizuri ili mtupatie furaha.

Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Bomani Michael Newland amezipongeza timu zilizoshiriki ligi hiyo huku akiwasihi wanamichezo kuonesha nidhamu uwanjani kwa kufanya hivyo watafika mbali kimchezo na ajira.

     Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Bomani Michael Newland

"Natoa pongezi kwa timu zilizoshiriki mashindano haya, michezo ni afya, urafiki, mahusiano pamoja na fursa mbalimbali. Michezo ni fursa ambayo sisi vijana inatufikisha mbali.

"Ukionekana unacheza vizuri unaaminiwa na timu za juu, kwahiyo kama una kipaji kizuri ebu kitumie vizuri kuwakilisha kile ambacho Mungu amekubariki.

Amewaomba kuwa na nidhamu wanapokuwa uwanjani kwani itawasaidia kuonekana kwa watu mbalimbali na kuwa na imani nao.

Amewashauri wasitumie vibaya vipaji vyao kufanya mambo ambayo hayaeleweki bali watumie vipaji vyao kuonesha watanzania kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa na mazuri huku akiwatakia kheri na afya njema katika mashindano hayo ya mpira wa kikapu.

Uzinduzi huo ulienda sambamba na mashindano ambapo timu ya mpira wa kikapu ya wanawake TANESCO ya Musoma imeshinda vikapu 40 dhidi ya Tigres queen ya Tarime ambayo imeambulia vikapu 21.

     Waliovaa jezi ya njano ni Timu ya TANESCO ya Musoma wakishindana na timu ya Tigres queen ya Tarime

Kwa upande wa wanaume timu ya mpira wa kikapu North Mara ya Tarime imeibuka mshindi kwa vikapu 58- 51 dhidi ya Mwembeni Club ya Musoma.

Kwa mwaka huu ligi hiyo ya mkoa imeanza Mei,7,2023 na itahitimishwa Julai, 22,2023 ambapo vilabu saba vinashiriki ligi hiyo.

      Timu ya North Mara ya Tarime



    Timu ya Mwembeni Club ya Musoma











No comments