BRELA YATOA ELIMU KWA WADAU WA UWEKEZAJI, WANAFUNZI VYUO VIKUU
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa Elimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini juu ya usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara katika semina iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.
Awali akiwasilisha mada katika semina hiyo, Afisa usajili kutoka Wakala wa usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Greyson Mushi ametoa mada juu ya umuhimu wa urasimishaji wa biashara na kampuni kwa kufuata taratibu maalum za kufungua ambazo pia zinapatikana kwenye mfumo wa Brela.
Aidha, Greyson amezitaja aina tatu za kampuni zinazosajiiwa BRELA kuwa ni Kampuni za nje (Foreign Company), Kampuni binafsi (Private Company), na Kampuni za Umma (Public Company).
Afisa usajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Greyson Mushi (mwenye tisheti nyeusi) katika semina hiyo
"Taratibu za usajili wa kampuni ambao unafanyika kwa njia ya mtandao wa (ORS) unaopatikana katika tovuti ya BRELA www.brela.go.tz ni rahisi kwa kila mtu kutumia, ni hatua bora na nzuri kwani imerahisisha utoaji wa huduma." Amesema Greyson.
Semina hiyo imehudhuriwa na wadau wa uwekezaji kutoka vyuo vikuu, watu binafsi wenye makampuni na wanafunzi wa vyuo chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), na Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa uwekezaji na wajasiriamali nchini, Sebastian Kingu amewasisitiza vijana kutumia fursa ya kujiunga katika umoja ili kufungua kampuni zao binafsi zitakazo wawezesha kujikwamua kiuchumi na kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sayansi na tekinolojia.
Semina hiyo iliyofanyika katika chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT), cha Jijini Dar es Salaam iliandaliwa na umoja wa uwekezaji na wajasiriamali nchini Tanzania Pan African Investers Association (TAPAIA), ilihusu fursa za vijana kujiunga na kufungua makampuni binafsi ili kujikwamua na changamoto za ajira nchini sambamba na kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na tekinologia.
Post a Comment