KATIBU: CWT NI CHAMA KIKUBWA WATAENDA WATARUDI
>>Asema hana taarifa ya walimu zaidi ya 20 kuhama chama
>>Asema hajamzuia mtu kuondoka, wenye nia ya kuondoka waondoke
Na Waandishi, Wetu Musoma
KATIBU wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Musoma Magero Misana amesema Chama chama cha Walimu Tanzania ni kikubwa na kwamba walimu wanaotaka kuhama chama waondoke yeye hajawazuia.
DIMA Online imewasiliana na Katibu huyo kufahamu kama amepata taarifa za walimu zaidi ya 20 katika shule kongwe ya Sekondari wanaodaiwa kuhama chama hicho na kujiunga na chama cha kulinda na kutetea haki za walimu Tanzania (CHAKUHAWATA).
Imedaiwa kuwa sababu ya walimu kuhama ni kutokana na Chama cha Walimu Tanzania kuwakata makato asilimia mbili ya mshahara kiasi ambacho kimedaiwa ni kikubwa hivyo kujiunga na CHAKUHAWATA ambacho makato yake ni Tsh. 5,000 kwa mwezi.
Katibu huyo wa CWT amesema hana taarifa ya walimu zaidi ya 20 kuhama chama na kujiunga na chama kingine isipokuwa ana taarifa ya mtu mmoja kuhama chama huku akisema mwanachama huyo aondoke tu kwani amekuwa ni msumbufu kwenye chama.
"Hahahaaaa! kwani wewe umesikia ofisi za mkoa za hicho chama zipo wapi hapa Manispaa? nimepata huyo mmoja tu wengine sijawaona, naamini watarudi tu. CWT ni chama kikubwa, wewe ulishaona chama cha CCM kinanyanyaswa na vyama vidogovidogo?, aniletee nakala tu barua yeye apeleke kwa Mkurugenzi"amesema huku akicheka.
Amesema hajaona waliojiondoa" Sijaona zaidi ya huyo mwalimu mmoja aliyekuja akiwa na hasira nikamwambia siwezi kukusikiliza wewe ondoka tu.Yule kwanza namhurumia kwasababu ni miongoni mwa walimu wangu wenye shida kuliko wote Musoma mjini.
"Ana kesi nyingi mahakamani za utapeli yeye anajiondoa akidhani huko makato ni marahisi, anayekata makato siyo Katibu yeye aende kwa Mkurugenzi watoe" amesema Magero.
Katibu huyo amesema kuwa CWT hukata makato asilimia mbili ya mshahara ambayo yapo kisheria kwenye chama na kwamba anawaruhusu wanaotaka kujiondoa waondoke.
"Kwanza ilikuwa siyo barua yangu ni nakala, mimi nina waruhusu wao waendelee tu mimi sina shida wao hata wakienda watakwama hawajui hata huo uongozi.
Ameongeza" Wewe utajiungaje na chama ambacho hujui hata ofisi wala hujui hata kiongozi, tena huyo akiondoka tunapata unafuu kwasababu anatusumbua kila leo kwenda mahakamani kudaiwa, ana kesi kibao mahakamani" amesema Magero.
Hata hivyo Mwalimu wa shule ya Sekondari Mara Mwl.Amon Kimacha aliyedai kufika kwa Katibu CWT na kutosainiwa barua yake ya kujiuzuru na kuagizwa kuondoka ofisini kama ilivyoripotwa DIMA Online saa chache zilizopita, amesema amejiondoa kutokana na makato makubwa ya mshahara.
Pia amekanusha kauli iliyotolewa na Katibu wa CWT kuwa yeye amekuwa msumbufu, tapeli na ana kesi nyingi mahakamani.
Amesema yeye hana kesi mahakamani zinazohusiana na Chama cha CWT, siyo tapeli na kwamba ana haki ya kujiunga na Chama akitakacho .
>>>Rejea
Saa chache DIMA Online imeripoti habari juu ya walimu 20 wa shule kongwe ya Sekondari Mara, iliyoko katika manispaa ya Musoma mkoani Mara wamekihama chama cha walimu Tanzania (CWT) na kujiunga na chama cha kulinda na kutetea haki za walimu Tanzania (CHAKUHAWATA).
Post a Comment