HEADER AD

HEADER AD

CWT MASWA YALIA NA MIKOPO UMIZA

>>Yasema baadhi ya walimu wanasalimisha kadi zao za benki(ATM) kukopa mikopo yenye riba kubwa

>>Walimu wasema wanalazimika kukopa kutokana na kipato kidogo

Na Samwel Mwanga,Maswa

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT)wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kimetoa wito kwa Walimu katika wilaya hiyo kupunguza idadi ya mikopo wanayokopa katika taasisi za fedha hasa zile zenye riba"Umiza"ili kujinusuru na umasikini.

Wito huo umetolewa na Katibu CWT wilaya ya Maswa,Mwalimu Nazama Tarimo katika kikao kilichoandaliwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda kusikiliza kero za Walimu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

    Katibu CWT wilaya ya Maswa, Mwalimu Nazama Tarimo

Tarimo ameonyesha kusikitishwa na mienendo ya baadhi ya walimu kusalimisha hadi kadi zao za benki(ATM)kwenye taasisi za fedha ili kukopa fedha zinazowalipisha riba kwa asilimia kubwa kwa mwezi.

Amesema kuwa inafikia hatua mtumishi wa Umma anadhalilishwa kwa kupigwa kutokana na madeni ya mikopo hiyo Umiza  hivyo ni vizuri serikali ikalitazama upyaa jambo hilo.

"Walimu wanapigwa, wananyang'anywa kadi zao za benki zile za ATM  huko ni kudhalilishwa na huko ni kudhalilisha utumishi wa Umma kutokana na mikopo hiyo hivyo ni vyema serikali ikalitazama upya jambo hilo,"amesema.

Amesema pamoja na lengo zuri la CWT kuanzisha benki ya Walimu lakini cha kushangaza Walimu walio wengi hawaitumii na kwamba endapo kila mwalimu angepitisha mshahara wake katika benki hiyo wangeweza kupata mikopo lakini walio wengi wanatumia benki nyingine.

     Mwl Frank Tauzen(mwenye kipaza sauti)akiwasilisha kero yake kwenye kikao Cha kupokea kero za Walimu katika wilaya ya Maswa.

"Hii benki ya Walimu ni benki yetu tuitumie na kila mmoja wetu akipitishia mshahara wake kwenye hiyo benki tungeweza kupata mikopo ambayo ina riba nafuu hivyo tutaendelea kutoa elimu ili tuitumie na tuepuke na hii mikopo Umiza,"amesema.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Elysalver Nkanga ambaye ni Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Simiyu amesema ni vizuri walimu kuchukua mkopo kulingana na utaratibu uliowekwa wa mikopo kwani kuchukua mikopo hadi kupitiliza kunasababisha kudhalilika jambo ambalo amesema halikubaliki. 

    Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Elysalver Nkanga ambaye pia ni Afisa Elimu Taaluma mkoa wa Simiyu akijibu hoja za Walimu wa wilaya ya Maswa katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

Ameongeza kusema kuwa inafikirisha mno kuona mwalimu ana madeni mengi na makubwa kiasi hicho lakini bado serikali na jamii inamtegemea afundishe vizuri na kwa weledi ili kumpa matokeo chanya wanafunzi.

"Kuna kuendekeza mambo haya ya mikopo pamoja na tamaa ya kuishi maisha ambayo si yako ni vizuri kupanga maisha yako kulingana na kipato chako kuliko huko ambako baadhi yetu tunadhalilishwa na walimu tunaonekana kutokana na kuwa tuko wengi,"

"Tukope kwa kutumia vyombo rasmi vya mikopo kama hizi taasisi za fedha ambazo ni benki zetu zinazo tambulika pia tukumbuke kuwa waraka wa ukopaji kwa Mtumishi wa Serikali ukienda kinyume unaweza kushitakiwa,"amesema.

Baadhi ya Walimu wamesema kuwa wanalazimika kuingia kwenye mikopo hiyo kutokana na kipato kidogo walichonacho huku maisha yakiwa juu hivyo kushindwa kuyamudu.

"Madeni ya Walimu isiwe issue maana hata madaktari na wauguzi wanakopa kwenye hiyo mikopo Umiza, kinachotufanya tukope ni kipato kidogo tulichonacho na wakati mwingine unapandishwa daraja lakini hupewi fedha na maisha yenyewe kila kukicha yanapanda ndiyo maana tunaingia kwenye mikopo hiyo,"alisema Mwl Goodluck Musiba.

Naye Jerry Nyabululu ameomba benki ya Walimu itoe mikopo kwa Walimu ili kuwanusuru kujiingiza kwenye mikopo Umiza ambayo imekuwa ikiwatia umasikini baadhi ya walimu waliojiingiza kwenye mikopo hiyo.

Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Simiyu,Kulwa Dwess (aliyesimama) akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Walimu wa wilaya ya Maswa.

No comments