SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATAKAOBAINIKA NA UPOTEVU WA DAWA
Na WAF- Dodoma
SERIKALI imepanga kuwachukulia hatua kali wale watakaobainika kuhusika na upotevu wa dawa ili iwe funzo kwa wengine wenye nia ovu ambayo inawanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupata huduma ya dawa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Mei 23, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge Luhaga Joelson Mpina katika Mkutano wa kumi na moja kikao cha 31, Bungeni Jijini Dodoma.
Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya iliona dalili za upotevu wa Bilioni 83 hivyo itashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuhakikisha wote watakaobainika kuhusika na upotevu huo wa dawa wanachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia hiyo.
Amesema Serikali imefanya mikakati mbalimbali katika kutatua tatizo la wizi na ubadhilifu wa dawa na vifaa tiba ikiwemo kufanya suala la upotevu wa dawa na vifaa tiba kama agenda katika vikao vya kamati za ulinzi na usalama za Mikoa na Wilaya.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa bidhaa za Afya ikiwemo kufunga mifumo ya kielectroniki pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa bidhaa hizo.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI imeendelea kuimarisha kamati za usimamizi za vituo kwa kuzijengea uwezo kuhusu majukumu yao katika usimamizi wa bidhaa za Afya.
Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema Wizara imeendelea kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wabunge kushiriki katika upokeaji wa bidhaa hizo na taarifa zote wapewe ili kujenga uwazi zaidi juu ya bidhaa hizo za afya.
Aidha, Dkt. Mollel amesema suala la kupambana dhidi wizi na ubadhilifu wa bidhaa za Afya siyo la Serikali pekee bali ni suala la kushirikiana pande zote, hasa wawakilishi wa wananchi.
Post a Comment