HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI WACHANGISHWA MILIONI 18.6 UJENZI WA MADARASA 3 AMBAYO SERIKALI IMETOA MILIONI 75

>>Ni katika shule ya msingi Kamimange Kijiji cha Magunga yenye zaidi ya wanafunzi 2,200 ikiwa na  vyumba vya madarasa 11 na nyumba moja ya mwalimu.

>> Katika kupunguza changamoto hiyo Serikali Kuu imetoa fedha Milioni 75 kujenga vyumba vitatu vya madarasa  na Milioni 6.6 kujenga choo matundu 3.

>>Licha ya Serikali kutoa fedha hizo wananchi wanatakiwa kuchangia tena Milioni 18.6 ya viashiria katika madarasa hayo.

>>Ded Butiama asema ofisi yake haijatoa maelekezo wananchi kuchangia fedha. 

>>>Tembelea www.dimaonline.co.tz kwa habari zaidi

Na Dinna Maningo, Butiama 

SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imesikia kilio cha wananchi wa Kijiji cha Magunga Kata ya Mirwa, wilaya ya Butiama mkoani Mara, kwa kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Kamimange.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Patricia Kabaka amesema shule ya msingi Kamimange imeletewa fedha kutoka Serikalini za ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa Tsh Milioni 75 na fedha Tsh. Milioni 6.6 ya matundu matatu ya vyoo.

    Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Patricia Kabaka

Hata hivyo licha ya Serikali kutoa fedha hizo viongozi wa Kata ya Mirwa na Kijiji cha Magunga katika kikao cha wazazi wenye watoto wanaosoma shule ya msingi Kamimange kilichoketi shuleni April, 28,2023, waliwaagiza wananchi kuchanga fedha ya viashiria kwa ajili ya kununua mawe, kokoto na mchanga kama nguvu kazi katika ujenzi wa madarasa hayo matatu.

Habari zinasema kuwa jumla ya Tsh. Milioni 18.6 zinatakiwa kuchangwa na wananchi katika vitongoji viwili, Kitongoji cha Kitalamanka Tsh. Milioni 9.3 na Kitongoji cha Wakiriba Tsh. Milioni 9.3 huku kila kaya ikitakiwa kulipa kati ya Tsh.20,000 na 15,000.

Changizo hilo limeibua maswali kwa wananchi na wazazi katika Vitongoji hivyo kudai kwanini wachangishwe fedha wakati Serikali yao imeshatoa fedha za ujenzi.

Wananchi wengine wamegoma kuchanga. Wakizungumza kwa sharti la kutotaka maji yao yatajwe ili kulinda watoto wao wanaosoma shule ya msingi Kamimange wamesema;

"Kijiji hakina Mwenyekiti wa Kijiji, alisimamishwa na Chama chake cha CCM tangu Novemba, 2022 hadi sasa ni kimya kijiji hakina Mwenyekiti.

"Mtendaji wa Kata ya Mirwa aliitisha kikao cha Wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule ya msingi Kamimange kilichofanyika shuleni.

" Mtendaji wa Kata na Mtendaji wa Kijiji wakatuambia kuwa Serikali imeleta pesa kiasi ambacho hatujui ni sh. ngapi, wakasema Serikali imeleta pesa na sisi wazazi tunatakiwa kuchangia kama viashiria kwa ajili ya kununua kokoto, mawe na mchanga" amesema mzazi mmoja.

Mzazi Mwingine amesema" Eti tukaambiwa kuwa tusipotoa viashiria kwa maana ya kuchangia fedha kwa ajili ya kununua mawe, mchanga na kokoto kujenga hayo madarasa, fedha hizo zitahamishwa kwenda kujenga shule nyingine.Walitoa maagizo wazazi hawakupewa nafasi ili kuuliza maswali kisha kikao kikafungwa.

      Shule ya msingi Kamimange Kata ya Mirwa wilayani Butiama

" Baada ya hapo wananchi walianza kuchangishwa fedha Kitongoji kimoja Mwenyekiti alikataa akasema mpaka aitishe mkutano wa Kitongoji wananchi waamue wenyewe.

"Kitongoji kingine Mwenyekiti wa Kitongoji yeye anaendelea kuchangisha, wananchi, wengine wamechanga na wengine wamegoma kuwa hawawezi kuchanga kwakuwa Serikali imeleta fedha" amesema.

Mwananchi mwingine amesema" Agizo la wananchi kuchangia fedha limesemwa na Mtendaji wa Kata na wa Kijiji kwenye kikao cha wazazi, kwanini hilo jambo hawakulileta kwenye mkutano wa Kijiji au mkutano wa hivyo vitongoji na badala yake maamuzi ya ujenzi yatolewe kwenye kikao cha wazazi kisha wananchi waanze kuchangishwa?!.

"Leo unamwambiaje mwananchi achangia ujenzi wakati hajui serikali imeleta sh. ngapi ili tupige hesabu kujua darasa moja linagharimu sh. ngapi tuone mapungufu tujadiliane na siyo Mtendaji wa Kata na Kijiji kusema kwamba zinahitajika Milioni 18.6 ambazo sisi wananchi hatujajiridhisha hesabu yake katika ujenzi.

Ameongeza" Wenye maamuzi ya kujadili michango ya ujenzi wa shule na maendeleo mengine ni mkutano mkuu wa Kitongoji, Kijiji au Kata na sio kikao cha Wazazi kwasababu kikao cha wazazi kinahusisha wazazi wachache wenye watoto wanaosoma katika hiyo shule.

Mtendaji wa Kata na Kijiji au Diwani wameshindwa nini kuitisha mkutano wa wananchi ambao ndio wenye watu wengi ili tujadili?. Tumechoka kupelekeshwa na viongozi wasiofuata taratibu za mikutano, pia wamekuwa na tabia ya kutumia mahudhulio ya wananchi wanaoshiriki vikao kuwa ndiyo wamekubali michango kumbe sivyo" amesema Mwananchi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha  Kitalamanka Jackson Maseko anayekusanya fedha za michango kwenye Kitongoji chake alipoulizwa sababu ya wananchi kuchangishwa fedha licha ya Serikali kutoa fedha amesema yeye anatekeleza maagizo.

"Dada yangu sisi ni watu wa kuagizwa tunatekeleza wajibu na mkutano wa wazazi uliketi wazazi waliitishwa kikao wakakubali.

"Kwani Serikali imetoa sh. ngapi?,suala hili la michango hata Mkurugenzi wa Halmshauri wanalijua, Diwani anajua  mimi ni mtu wa chini sana siwezi kujua kiundani" amesema Mwenyekiti huyo wa Kitongoji.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Wakiriba Ronald Korneli amesema anashangaa licha ya fedha kutolewa na Serikali lakini wameagizwa kuchangisha wananchi michango ya fedha katika ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa vilivyogharamiwa na Serikali.

      Shule ya msingi Kamimange Kata ya Mirwa wilayani Butiama

"Mtendaji wa Kata ambaye ana mwezi mmoja tangu aletwe kwenye Kata hii sijamfahamu jina lake, Mei, 28,2023 alihitisha kikao cha wazazi kilichoketi shuleni akatutangazia kuwa Serikali kuu imeleta Tsh. Milioni 80 za ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na choo matundu matatu.

"Mtendaji wa Kata akasema Serikali imeleta pesa hivyo viashiria vya wananchi vinatakiwa kuonekana ili nao waweke nguvu zao kuchangia mawe, mchanga na kokoto. Mtendaji wa Kijiji nae akakazia kuwa wananchi ni lazima wachangie maendeleo.

"Tukaambiwa kwa viashiria hivyo zinatakiwa fedha Tsh. Milioni 18 na laki sita ambapo ikigawanywa kwenye vitongoji viwili vyenye hiyo shule kila kitongoji kinatakiwa kuchangia Tsh. Milioni 9.3 "amesema.

Mwenyekiti huyo wa Kitongoji amesema Kitongoji chake kina Kaya 668 " Kwenye Kitongoji changu ili kupata hiyo Milioni 9.3 kila kaya inatakiwa kulipa Tsh.15,000 ya viashiria.

"Niliitisha mkutano wa Kitongoji ili nikawaeleze kilichosemwa kwenye kikao cha wazazi, mkutano ulikuwa ufanyike jana (Jumapili) lakini haukufanyika watu walikuwa wachache walikuwa kanisani.

"Mkutano huo utafanyika kesho (Jumanne) ili wananchi wao waamue. Ila najiuliza inakuwaje Serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu Samia Suluhu imetuondolea adha ya michango ikaleta pesa ili kujenga madarasa lakini bado wananchi wachangishwe fedha kujenga madarasa hayo hayo?.

"Ukipiga hesabu ya fedha zilizoletwa zinatosha kujenga madarasa na madawati ndani yake pamoja na choo. Fedha za UVIKO zilizotolewa na Serikali Kuu kujenga vyumba vya madasara wananchi hawakuchangishwa.

"Na zilikuwa Milioni 20 kwa kila darasa, madarasa yamejengwa hadi kukamilika jengo, viti na meza ndani yake pesa ikatosha, kwanini huku kwetu pesa zimeongezwa lakini bado tunaambiwa tuwachangishe wananchi?, tutakaa mkutano wananchi wenyewe wataamua.

Mtendaji wa Kijiji cha Magunga Lucus Kagina alipoulizwa kuhusu uchangishaji wa fedha na taratibu za michango amesema" Usinisumbue narudia tena usinisumbue" amesema kisha akakata simu.

Juhudi za kumpata Mtendaji wa Kata ziligonga mwamba baada ya kutofanikiwa kupata mawasiliano yake.

Diwani wa Kata ya Mirwa Willy Brouwn alipoulizwa kama ana taarifa ya wananchi kuchangishwa na kama ni sahihi wananchi kuchangia fedha ujenzi wa madarasa ambayo serikali tayari imeshatoa fedha hakuwa tayari kutoa ushirikiano wala kujibu chochote.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Patricia Kabaka amesema "Hakuna kitu kama hicho, hakuna maagizo yoyote yaliyotoka katika ofisi ya Ded kama hayo" amesema Patricia.

Machi, 18, 2023, DIMA Online kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter iliripoti habari ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kamimange yenye wanafunzi zaidi ya 2,200 huku ikiwa na vyumba vya madarasa 11 na nyumba moja ya mwalimu.

No comments