DARAJA JIPYA FURAHA KWA WATUMIA BARABARA TARIME WALIOTESEKA KWA MIAKA 20
>> Awali wakati wa mvua watu na mifugo walisombwa na maji, vifo
>> Wananchi walisubiri kwa saa kadhaa maji yapungue ili wavuke mto
>>Iliwabidi kuvua nguo zao na viatu wakati wa kuvuka mto
>>Wazazi walienda kukaa mtoni kusubiri kuwavusha wanafunzi
Na Dinna Maningo, Tarime
KWA zaidi ya miaka 20 wananchi wanaotumia barabara ya Gamasara- Mtana, inayopita kata ya Nyandoto kuelekea kata ya Manga wamekuwa wakikumbwa na adha wakati wa msimu wa mvua.
Msimu wa mvua mto ulijaa maji na kulifunika daraja jambo lililowalazimu wananchi kukaa kwa saa kadhaa kusubiri maji yapungue wavuke mto na wengine walilazimika kuvua nguo zao wakati wa kuvuka mto.
Barabara hiyo inayopita mto Kigera iligeuka kuwa kero kubwa kwa watembea kwa miguu na watumiaji wa vyombo vya moto kwani wakati mwingine watu walisombwa na maji pamoja na mifugo huku kukitokea vifo baada ya kuzama majini wakati wakijaribu kuvuka mto.
Katika kuondoa kero za madaraja, barabara, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini humo, Dkt. Samia Suluhu Hassan imerejesha furaha kwa watumia barabara baada ya kuwajengea Daraja jipya (Kivuko) na kuliondoa daraja la zamani lililoleta adha kwa wananchi, sasa wanavuka mto kwa amani na usalama.
Meneja TARURA anena
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Charles Marwa anasema ujenzi wa daraja hilo umegharimu Tsh. Milioni 37.
Anasema bajeti hiyo ni ongezeko la zaidi ya mara tatu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha Tsh. Milioni 729 hali ambayo imesaidia kuwapunguzia wananchi kero za barabara.
Wananchi waeleza walivyopata adha kuvuka mto
Wananchi wanasema kuwa kabla ya kujengwa daraja jipya kulikuwa na daraja dogo ambalo halikuwa na uwezo wa kuhimili maji ili wananchi kuweza kuvuka wakati wa mvua kwakuwa maji yalijaa na kufunika daraja.
Chacha Mgusuhi mkazi wa Mtaa wa Nyakihenene anasema daraja lililokuwepo lilikuwa bovu mvua ziliponyesha wanafunzi hawakwenda shule, hata watu wazima walishindwa kupita, iliwaladhimu kusubiri maji yapungue ndipo wavuke.
"Maji yakijaa tunakaa masaa manne kusubiri maji yapungue ndio tuvuke. Watu wazima waliokuwa na uwezo wa kuvuka walivuka maji ambayo yalikuwa yanawafikia kiunoni, wengine walivushwa " anasema Chacha.
Anasema kuwa watu walipata tabu kuvuka mto msimu wa mvua wakiwemo wafanyabiashara wa maziwa hali iliyosababisha wengine kupoteza maisha na wengine kunusurika kusombwa na maji.
"Watu waliteseka wakiwemo wapeleka maziwa mjini wakitokea Bukenye, kuna mmoja alitoka kuuza maziwa mjini wakati anarudi nyumbani akiwa anavuka mto alikuwa na baiskeri akiwa amebeba sabuni alipelekwa na maji tulienda kumuokoa akaponea chupuchupu kwa vile watu walikuwepo.
" Kuna mwendesha pikipiki wakati anavuka mto akakosea kupita akapita mahali kusiko na daraja akasombwa na maji tulimwokoa na pikipiki iligota kwenye maukindu tukaiokoa " anasema Chacha.
Mwikwabe Samo anasema " Daraja lilikuwa bovu lilileta athari hata kuna binti wa Wakwi Makandaiga alikufa baada ya gari kupinduka kutokana na ubovu wa barabara.
" Kuna kijana wa Bisarwi alikuwa anatoka kupeleka maziwa wakati anarudi nyumbani daraja lilikuwa limebomoka kwenye kingo za daraja, maji yalikuwa yameziba akashindwa kunyoosha baiskeri akapiga kichwa kwenye ukingo wa daraja maji yakamsomba akafa.
"Mto huo uliua watu wawili na wengine kadhaa kuokolewa baada ya kusombwa na maji. Mmoja alivushwa kwa kamba tukamtupia kamba akashika tukamwokoa" anasema Mwikwabe.
Mwikwabe anasema kuwa wakati wa mvua mto ulipojaa na kufunika daraja hasa nyakati za usiku walishindwa kuvuka na hivyo baadhi ya wananchi kulazimika kuomba hifadhi nyumba zilizopo jirani na mto.
"Watu wengine walivushwa, mimi nilikuwa navusha watoto. Kipindi cha mvua wazazi walikuja darajani kukaa kusubiri wanafunzi ili wawavushe mto.
"Kwakweli tunaishukuru Serikali ya Rais mama Samia, maji yalikuwa yakijaa watu wanaomba hifadhi wanalala. Mtu ulikuwa umevaa viatu vyako ukifika mtoni unavua, watu wanakunja nguo zao wanabaki uchi ili nguo zisilowane wanavuka kisha wanaendelea na safari zao.
Shukrani kwa Serikali
Watumiaji wa Barabara ya Gamasara- Mtana wakiwemo wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Gamasara wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia kwa kujenga Daraja mto Kigera.
Wanafunzi wanasema kuwa msimu wa mvua walikaa utoro kwakuwa mto ulijaa maji na hivyo kushindwa kuvuka kwenda shule.
Ferista Kisabo mwanafunzi wa darasa la pili anasema tangu daraja jipya lijengwe hawapati tabu kuvuka mto kwani kabla ya daraja kujengwa walilazimika kuvua viatu vya shule na kuingia ndani ya maji kuvuka mto.
"Namshukuru Rais Samia kwa kutujengea daraja, wakati wa mvua tulikaa utoro mto ulijaa maji tukashindwa kuvuka, mvua ikiisha tunasubiri mpaka maji yapungue ndiyo tuvuke, tulichelewa kwenda shule "anasema Ferista.
Neema Ghati anasema kwa sasa hawaombi msaada wa kuvushwa mtoni kwani kabla ya kujengwa daraja hilo jipya mvua iliponyesha maji yalijaa na kuwapa tabu kuvuka hivyo walizazimika kuomba msaada wa kuvushwa na watu wanaoishi jirani na mto huo.
Jane Mwikwabe mtumia barabara mkazi wa Mtaa wa Nyakihenene anasema" Kwakweli tunamshukuru Rasi Samia Suluhu katika uongozi wake daraja lililokuwa kero kwetu kwa miaka mingi limejengwa.
"Hakika wanawake tunaweza, Rais Samia anaweza, tunamshukuru sana wanawake tulipata tabu sana kuvuka mto kwenda mjini Tarime tulilazimika kuvua nguo kuzipandisha juu ndipo tuvuke mto tena hadharani, tulivua viatu wakati wa kuvuka mto.
"Rais Samia wewe ni mwanamke msikivu na shupavu kwa kutujali wananchi, umewaondolea kero hata watoto wadogo walioshindwa kwenda shule Gamasara wakati wa msimu wa mvua kutokana na maji kujaa mtoni" anasema Neema.
Pamoja na mafanikio hayo ,Mwita Nyehiyo ameiomba TARURA kuwawekea Karavati jirani na barabara hiyo kwa kile alichosema kuwa wakati wa kujenga daraja barabarani kuna eneo kulikochimbwa mtaro na kusababisha wapate changamoto wakati wa kuvuka mtaro kuelekea kwenye makazi yao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakihenene Thomas Jovinalis anasema watu walipata adha kubwa kwa zaidi ya miaka 20 tangu daraja la zamani lilipojengwa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakihenene Thomas Jovinalis
"Naipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi wa mtaa wangu ambao ili uende mjini lazima uvuke mto, daraja jipya limewasaidia wananchi kuvuka bila shida tofauti na awali daraja lilikuwa tabu.
"Watu walisombwa na maji pamoja na mifugo wakati wa masika. Zaidi ya watu 15 waliokolewa baada ya kusombwa na maji wakivuka mto, wengine iliwabidi waache kuvuka mto na kwenda kutafuta maeneo yenye unafuu ya kuvuka" anasema Mwenyekiti wa mtaa.
Thomas anasema "Kwenye vikao vya WDC 2015 nilipeleka changamoto hii ili daraja litengewe fedha lijengwe.Tunashukuru limejengwa jipya watu wanapita kwa Raha, tunaomba wadhibiti magari makubwa zaidi ya tani 10 yamayopeleka vifaa mgodi wa uchenjuaji dhahabu, sijui kama litahimili kwa muda mrefu maana hayo magari yanayopita ni zaidi ya tani 10.
"Changamoto iliyobaki tunaomba TARURA ijenge mitaro mikubwa ya kuzuia maji yasije kuvunja daraja, wanaweka mitaro midogo ambayo haikidhi haja ya kuzuia maji yasiende kuharibu daraja.
Menjea TARURA Mhandisi Charles Marwa anaipongeza Serikali kwa ongezeko la bajeti ya ujenzi wa Barabara katika halmashauri hiyo ambayo imepunguza changamoto za barabara vikiwemo vivuko.
"Awali Halmashauri ya Mji Tarime tulikuwa tunapata bajeti ya mwaka ya Matengenezo kati ya Milioni 500 hadi 729, lakini tangu mwaka wa fedha 2021-2023 bajeti iliongezeka hadi kufika Bilioni 2.209 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
" Utaona bajeti hiyo ni zaidi ya mara tatu ya Milioni 729 ya mwaka wa fedha 2020/2021. Dhamira ya Rais Dkt Samia ni kuhakikisha kero za barabara zinatatuliwa lakini pia kuhakikisha kila mwananchi anaweza kutoka nyumbani kwakwe na kwenda sehemu za uzalishaji mali na huduma za jamii bila shida" amesema Meneja TARURA.
Bajeti hiyo ya matengeneze ya barabara ni kutoka katika vyanzo vitatu ambavyo ni fedha ya tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti ambayo ni makato ya Tsh. 100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli kiasi cha Tsh. Bilioni moja.
Daraja jipya
Fedha ya Jimbo la uchaguzi Tsh. Milioni 500 na fedha kutoka mfuko wa barabara kiasi cha zaidi ya Milioni 700 na kwamba hadi kufikia Machi, 2023 TARURA imepokea fedha Bilioni 1.295 sawa na asilimia 58.6.
"Fedha zote zimepokelewa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara katika Halmashauri ya Mji Tarime, ambapo matengenezo hadi kufikia mwezi Machi ni asilimia 91.3
Charles anasema kupitia bajeti hiyo zimefunguliwa barabara saba mpya jumla km.18.76 zenye urefu wa kati ya mita 300-500 katika maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki.
"Barabara zimefunguliwa katika maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki kama kule mtaa wa uwanja wa ndege,Nyamisangura, Turwa, Kenyamanyori,Nyandoto, Nkende, kila Kata ilipata barabara mpya ambayo imefunguliwa"anasema Charles.
Anasema zimetengenezwa barabara km 15.4 kwa kiwango cha changarawe, na daraja moja mtaa wa Nkongore limejengwa kwa gharama ya Tsh. Milioni 675 na lingine linajengwa Kinyambi litakalogharimu Tsh. Milioni 546 lenye urefu wa mita 21.
"Tumetengeneza kwa changarawe zenye ubora tulikuwa tunatoa kule Gamasara, lengo kumwezesha mwanachi aweze kupita kwa urahisi anapokuwa katika shughuli zake za uzalishaji na huduma za jamii" anasema Meneja.
Pia Vivuko/Karavati) 24 vimejengwa pamoja na Mitaro ya maji ya mvua yenye jumla ya urefu wa mita 1,900 sawa na km 1.9 pamoja na ukarabati wa barabara za udongo jumla km 145.02 Kata mbalimbali katika Halmashauri hiyo.
Post a Comment