RC KAGERA KUSIMAMIA MIRADI SUGU ILIYOKWAMA
Na Alodia Babara, Bukoba
MKUU wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amekemea mambo matano ambayo ni uzembe, uongo, uvivu, ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo na ubadhilifu wa mali za umma na kuwa atashughulikia watendaji watakaojihusisha nayo.
Mwassa ameyasema hayo Mei 29, mwaka huu katika kikao na wakuu wa Taasisi za umma mkoani Kagera kilichofanyika katika ukumbi wa mkuu huyo.
Mwassa amesema kuwa hatokuwa tayari kuvumilia uzembe wa aina yoyote toka kwa watumishi watakaoonekana kukwamisha maendeleo huku akiahidi kutowasamehe.
"Watumishi wazembe tutawakataa tunahitaji wachapa kazi ambao watauvusha mkoa wetu kuutoa ulipo na kuusogeza mbele hivyo kama kuna wezembe ni lazima mkafanye mabadiliko ya haraka kabla hamjabainika" Amesema Fatma.
Amesema anahitaji kuona mkoa huo unatoka katika nafasi ya sasa kiuchumi na kupanda juu huku akitegemea watumishi hao kufanya ubunifu wa haraka katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha amesema atahakikisha anaanza na miradi sugu iliyoonekana kukwama kwa muda mrefu ikiwemo ujenzi wa stendi kuu na soko ambapo pia amewakumbusha watumishi hao wajibu wao ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili maendeleo ya mkoa huo yaonekane kwa haraka.
Hata hivyo Taasisi mbalimbali za serikali zimewasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo huku mkuu huyo akiwasihi kuwa wamoja ili maendeleo ya mkoa huo yaweze kwenda kwa haraka.
Post a Comment