HEADER AD

HEADER AD

DC MASWA ARIDHISHWA NA UJENZI WA MIRADI YA MAUWASA

Na Samwel Mwanga, Maswa

MKUU wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Aswege Kaminyoge ameridhika na maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya Maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(MAUWASA).

Amesema hayo Mei,04,2023 wakati akitembelea miradi hiyo akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya huku akiagiza ikamilike kwa wakati.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Ujenzi wa tenki la kuhifadhi Maji lita Milioni mbili katika Kijiji cha Hinduki na ulazaji wa mabomba ya maji katika tenki la Nyalikungu lililopo mjini Maswa.

     Sehemu za bomba zilizounganishwa za kuingiza Maji katika Tenki la kuhifadhi Lita Milioni Moja lililopo kwenye kilima Cha Nyalikungu

Miradi mingine ni pamoja na mradi wa Maji ya bomba katika kijiji cha Mwashegeshi na mradi wa maji wa bomba wa dharura katika mji wa Malampaka.

Kaminyoge amesema kuwa miradi yote waliyotembelea iko katika hatua nzuri kutokana na usimamizi mzuri wa Mamlaka hiyo.

Amesema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias(kushoto,)akisoma taarifa  kwa Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(kukua) ya Ujenzi wa tenki katika mji wa Malampaka

"Hii miradi ikikamilika itaondoa changamoto ya upatikanaji wa Maji safi na salama katika maeneo hayo sambamba na kuboresha huduma ya maji hasa katika mji wa Maswa,"amesema.

Amesema kuwa fedha za kutekeleza miradi inayoletwa na serikali katika Mamlaka hiyo zimekuwa hazikai kwenye akaunti kwa muda mrefu kwani zimekuwa zikitumika mara moja kwenye miradi iliyokusudiwa.

"Jambo jingine nipongeze uongozi wa MAUWASA kwa kutekeleza miradi hii na fedha inapoingia kwenye akaunti zinaanza kutumika mara moja kwenye miradi iliyokusudiwa hazikai muda mrefu kwenye akaunti na miradi inatekelezwa na tunaiona,"amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA,Mhandisi Nandi Mathias amesema miradi yote itakapokamilika itagharimu zaidi ya Sh Bilioni mbili itaisaidia Mamlaka hiyo kuongeza mtandao wa usambazaji wa Maji safi na salama kwenye maeneo wanayoyahudumia.

    Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias(kushoto) akisoma taarifa ya Mradi wa kutandaza mabomba katika tenki la Nyalikungu mjini  Maswa Kwa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Maswa.

Aidha Mhandisi Nandi ameishukuru serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ya Maji.



No comments