HEADER AD

HEADER AD

WALIMU NYANTAKARA SEC WADAIWA KUFANYA BIASHARA YA KUWAUZA WANAFUNZI WA KIKE KWA WANAUME

>>> Walimu wengine wadaiwa kujihusisha na vitendo vya ngono na wanafunzi

>>>Wapo wanaochukua fedha kwa wanaume wanaofanya mapenzi na Wanafunzi ili wasiwape adhabu

>>>Madiwani waiomba Serikali kuwajibisha walimu kunusuru wanafunzi

Na Daniel Limbe,Biharamulo

BAADHI ya Walimu katika shule ya Sekondari Nyantakara wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera wanadaiwa kufanya biashara haramu ya kuwauza wanafunzi wa kike kwa wanaume ili kujipatia fedha huku wengine wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya ngono na wanafunzi.

Kukithiri kwa vitendo vya biashara haramu ya kuwauza wanafunzi wa kike kwa wanaume imemsababisha Diwani wa viti maalumu, Ziyuni Hussein kumwaga machozi mbele ya madiwani wenzake kutokana na hatua dhaifu zinazochukuliwa na mamlaka husika.

Ni kutokana na kutoridhishwa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali kwa watuhumiwa wa vitendo hivyo kwa lengo la kunusuru maisha ya wanafunzi ambao wapo hatarini kushindwa kutimiza ndoto zao kupata elimu bora.

   Diwani viti maalumu Biharamulo,Ziyun Hussen,akichangia hoja kwa uchungu kabla ya kumwaga machozi.

"Inasikitisha sana kuona wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari Nyantakara wanaendelea kuuzwa kwa wanaume na mwalimu tena wa kike aliyepewa dhamana ya kuwalinda na kuwafundisha maadili mema watoto wetu"

"Wanafunzi wanazidi kutoa mimba na baadhi ya walimu wanathubutu kuchukua fedha kwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanafunzi hao ili kuwasaidia watoto hao wasipewe adhabu ya kulejeshwa majumbani mwao kutokana na adhabu zinazotolewa na walimu wa shule hiyo" amesema Ziyuni.

Awali vitendo hivyo viliibuliwa mwaka jana 2022 na kamati maalumu ya madiwani wa viti maalumu wa halmashauri hiyo ambapo walitembelea baadhi ya shule za sekondari na kubaini changoto mbalimbali ikiwemo mwalimu wa kike (jina limehifadhiwa) kujipatia fedha kinyume cha sheria kwa kuwauza mabinti kwa wanaume kwenye shule ya sekondari Nyantakara.

Baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwenye vikao vya baraza la madiwani tangu mwaka jana kwa lengo la kuchukua hatua za haraka kuwanusuru watoto hao ambao wapo hatarini kupata mimba za umri mdogo na kukatishwa masomo,bado hatua stahiki hazijachukuliwa kutokana na mkanganyiko wa mamlaka za kinidhamu.

Baadhi ya madiwani wakiwa kwenye kikao chao

Kutokana na hali hiyo,baadhi ya madiwani hao wamegeuka mbogo kutaka walimu wote waliotajwa kwenye ripoti ya madiwani hao kusimamishwa kazi haraka wakati taratibu zingine za kisheria zikiendelea.

Akitoa ushauri kwa baraza hilo kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,Ofisa Utumishi Mathias Likenejo,amesema baraza hilo halina mamlaka kisheria ya kuwawajibisha walimu ispokuwa Tume ya utumishi wa walimu ambao ndiyo wenye jukumu hilo baada ya kupewa taarifa za mamlaka ya halmashauri.

Kauli hiyo imeonekana kupokelewa kwa hisia tofauti ambapo Diwani wa kata ya kata Nyantakara,Sospeter Rugula,amesema pasipo hatua za makusudi kuchukuliwa haraka ipo hatari kubwa ya madhara kuongezeka kwa jamii huku akizitaka mamlaka zinazohusiana na nidhamu kwa walimu kusaidia suala hilo pasipo kulindana.

Diwani wa kata ya Nyantakara,Sospeter Rugula,akiendelea kuchambua hoja za baraza hilo.

Hata hivyo,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,amewataka madiwani hao kuvuta subra kusubiri ripoti ya baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo,ili baadaye kuwe na uamuzi wa busara kwa walimu waliotajwa kuhusika na masuala ya utovu wa nidhamu.

"Niwaombe sana wajumbe wa kikao hiki tuvute subra katika hili, kwa maana ripoti iliwataja walimu takribani sita kwahiyo haitakuwa busara kutaka awajibishwe mwalimu mmoja pekee aliyetajwa na wanafunzi kuwatafutia wanaume wakati na wengine wanatuhuma za kufanya ngono na wanafunzi wao" amesema Rushahu.

Kushoto ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,akiendelea kupokea changamoto za wajumbe wa baraza hilo,akiwa na Katibu wa kikao,Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Inacent Mkandara.  

No comments