HEADER AD

HEADER AD

TMDA YAPATA HATI SAFI YA UKAGUZI WA CAG

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

MWENYEKITI wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba-TMDA, (MAB), Eric Shitindi, ameipongeza TMDA kwa kupata Hati safi kwenye  ukaguzi wa hesabu za mwaka wa Fedha 2021/2022  na kuielekeza Mamlaka kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG ili kuendelea kupata hati safi.

Mwenyekiti wa MAB, Eric Shitindi akipokea Hati Safi ya ukaguzi wa CAG kwa hesabu za mwaka wa fedha 2021/22 kutoka kwa Mwenyekiti wa kamati ya Ukaguzi na Vihatarishi, CPA Zaina Thabiti.

Shitindi ametoa pongezi hizo mara baada ya kukabidhiwa Hati safi ya ukaguzi toka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi na Usimamizi wa Vihatarishi ya MAB, CPA Zaina Thabiti mara baada ya kukabidhiwa na Mkurugenzi mkuu wa TMDA,  Adam Fimbo, wakati wa kikao cha kawaida cha Bodi kupitia taarifa mbalimbali za utendaji kazi wa Taasisi kinachofanyika kwa siku mbili tarehe 4 na 5 Mei, 2023 mkoani Mtwara.

“Sisi kama bodi tunapata faraja na fahari kusimamia taasisi ambayo inatambua na kutekeleza mifumo thabiti ya kiutendaji ikiwa ni pamoja na kusimamia ipasavyo rasilimali zilizopo kwa maslahi mapana na nchi” amesema Shitindi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, wakati akikabidhi Hati safi hiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi amsema;

“Mafanikio haya yote yanatokana na utekelezaji wa maelekezo na ushauri unaotolewa na Bodi unayoiongoza kwa lengo la kuepuka hoja mbalimbali za kiukaguzi”.

“Nikiwa kama Mtendaji Mkuu wa kila siku pamoja na timu nzima ya Menejimenti,nikiri kuwa tunayo furaha na tunajivunia mafanikio haya ambayo yamekuwa ni rekodi nzuri kwa Taasisi na hata kwa Wizara mama”. Amesema Fimbo.

Aidha, TMDA, tangu kuanzishwa kwake, imeweka rekodi ya kupata Hati safi kwa miaka takriban 15 mfululizo ambapo maelekezo na ushauri unaotolewa na CAG katika kila kaguzi yamekuwa yakizingatiwa.

Mwenyekiti wa MAB, Eric Shitindi Akikabidhiana Hati safi na Mwenyekiti wa kamati ya Ukaguzi na Vihatarishi, CPA Zaina Thabiti. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ni Taasisi iliyo chini ya wizara ya Afya yenye jukumu la kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii.



No comments