HEADER AD

HEADER AD

DIWANI ATAKA MWALIMU APIMWE AKILI

Na Samwel Mwanga,Maswa

DIWANI wa Kata ya Zanzui katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Jeremiah Shigala (CCM) ataka aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sola wilayani humo,Edward Lutabu apimwe akili.

Diwani huyo amesema hivyo kutokana na majibu ya mwalimu huyo anayoyatoa kufuatia sakata linalomsibu la tuhuma za kudaiwa kufanya matumizi ya Tsh. 10,780,128  za shule hiyo bila kufuata kanuni za manunuzi ya Serikali.

Fedha hizo zimetokana na fidia toka Wakala wa barabara nchini (TANROAD) baada ya sehemu ya eneo la shule hiyo kupitiwa na Barabara ya mchepuko ya lami ya Mjini Maswa.

      Madiwani wa Halmashauri ya Maswa wakiwa kwenye Kikao.

Akizungumza katika kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani katika halmashauri hiyo amesema kuwa suala hilo limekuwa la muda mrefu na sasa ni mara ya pili kuzungumzwa kwenye kikao hicho na diwani wa Kata ya Sola,Masanja Mpiga.

Amesema majibu ya Mwalimu huyo yanachonganisha kati ya Madiwani na Watendaji wa halmashauri hiyo hivyo ni vizuri akapimwe akili Ili ijulikane kama kichwa chake kama kipo vizuri.

"Hili sakata la Mwalimu sasa ni mara ya pili linazungumzwa katika kikao cha baraza la madiwani na hata majibu ya mwalimu ukiyaangalia yanachonganisha sisi madiwani na Wataalam wa halmashauri yetu ni vizuri akapimwe akili,"alisema.

Amesema kuwa ni vizuri suala hilo la madai dhidi ya mwalimu likafika mwisho kuliko hali ilivyo sasa ambalo limezua sintofahamu na kusababisha Mwalimu huyo kuvuliwa madaraka na kusimamishwa kazi 
 
Awali Diwani wa Kata ya Sola,Masanja Mpiga akiuliza swali la papo kwa papo amesema kuwa katika fedha hizo Mwalimu huyo amenunua mashine ya kurudufu karatasi tu na fedha nyingine hazijajulikana zimefanya shughuli gani.

Amendelea kueleza kuwa pamoja na hatua za awali zilizochukuliwa dhidi ya mwalimu huyo lakini bado amekuwa akiwatuhumu walimu wenzake kuwa ni washirikina na sasa ameandika barua kwa Rais Samia Suluhu akimuomba uhamisho wa kutoka shule hiyo.

"Huyu Mwalimu katika hizo fedha amenunua kitu kimoja tu nacho ni photocopy mashine tu na amepaka rangi madarasa la rangi tofauti na madarasa mengine kinyume cha utaratibu hivyo nataka kujua ni hatua gani zaidi zitachukuliwa, dhidi yake"amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Simon Berege amesema kuwa hatua za kiserikali zile za kisheria na zile za mamlaka yake ya kinidhamu zimeanza kuchukuliwa dhidi ya mwalimu huyo kutokana na tuhuma zinamkabili na hata yeye anapenda suala hilo limalizike mapema.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Berege akijibu moja ya hoja kwenye Kikao Cha baraza la Madiwani.

Akizungumzia madai dhidi yake Mwalimu Lutabu amesema kuwa afya yake ya akili iko vizuri na ndiyo maana alipewa cheo cha Mwalimu mkuu na bado ni mwalimu mzuri wa somo la hisabati kwa darasa la saba.

"Mie niko vizuri sana kiakili ndiyo maana waliona ninafaa wakaniteua kuwa Mwalimu mkuu na hata somo ninalolimudu ni hesabu darasa la saba ambao ni walimu wachache wenye uwezo kichwani yaani akili wanaofundisha,"amesema.

Amesema kuwa tuhuma dhidi yake zilizotolewa na diwani,Masanja dhidi yake ni za uongo licha ya kuwa ni diwani wa Kata iliyopo shule ya msingi Sola lakini hana taarifa sahihi kwani fedha hiyo imetumika kama walivyokubaliana kwenye vikao mbalimbali ikiwemo Kamati ya shule na kikao cha walimu wa shule hiyo.

            Mwl. Edward Lutabu

Amesema kuwa suala hilo la fedha hizo kwa sasa linachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)huku tayari mamlaka yake ya nidhamu yaani Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC)imekwisha kumuandikia barua ya kusimamishwa kazi kutokana na tuhuma hizo ambazo amedai si za kweli.

"Suala la madai ya fedha hizo kuwa zimetumika bila kufuata utaratibu hazina ukweli wowote kuna chuki binafsi ndiyo maana unaona wameungana wote kunishambulia,maana TAKUKURU wanachunguza,TSC nao wamechukua hatua bila kujiridhisha kuwa nimepatikana na hatia na diwani naye anakimbilia kwenye baraza la madiwani,"

"Mie niko tayari kwenda mahakamani kujibu hizo tuhuma nasubiri wamalize uchunguzi wao maana mahakama ndicho chombo pekee cha kutoa haki hapo ndipo tuhuma dhidi yangu nazodaiwa za wizi na ubadhirifu zinaweza kuthibitishwa na si vinginevyo wanavyotumia nguvu kubwa,"amesema.

Kuhusu kumuandikia barua Rais Dkt Samia Suluhu amesema ni kweli na hiyo inatokana na kutokuwa na imani na viongozi wa wilaya na mkoa ambao amedai nao wamekuwa ni sehemu ya kumnyanyasa badala ya kumsaidia na kusisitiza kuwa msaada zaidi amebakiza kwa Rais,Samia.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Paul Maige(mwenye kipaza sauti)akiongoza Kikao Cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

No comments