WAANDISHI WA HABARI WAWASHUKIA MA- RPC UCHELEWESHAJI WA TAARIFA
>>Watamani Wakuu wa Polisi wilaya (OCD) wawe wasemaji.
>>Wasema baadhi ya ripoti zinakinzana na uhalisia wa tukio
>>Baadhi ya Matukio Ma-RPC wadaiwa kukacha kuyatolea taarifa
>>Wasema miaka ya nyuma hata usipomkuta RPC ofisini Waandishi wa Habari walikuta taarifa kwa Makatibu Muhtasi (PS).
>>Waiomba Serikali kushusha mamlaka ya usemaji kwa wakuu wa Idara katika Halmashauri na Ma- OCD ili kuharakisha upatikanaji wa taarifa.
Na Dinna Maningo, Musoma
UCHELEWESHAJI wa taarifa kutoka kwa baadhi ya vongozi wa Serikali ambao ni wasemaji na watoa taarifa katika Wilaya, Mkoa, Halmashauri na Taasisi za Serikali umetajwa kukwamisha utendaji kazi kwa Waandishi wa Habari mkoani Mara katika kuhakikisha wananchi wanapata habari kwa wakati.
Imeelezwa kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa taarifa unaosababishwa na baadhi ya viongozi na Watendaji wa Serikali hususani Wakurugenzi wa Halmashauri, Makamanda wa Jeshi la Polisi na Waganga wakuu.
Makamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mara ni miongoni mwa wasemaji wanaolalamikiwa kwa kuchelewa kutoa taarifa kwa wakati na zingine kutotolewa jambo linalosababisha wananchi kutopata haki ya kupata habari kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 18.
Hayo yameelezwa hivi karibuni Mei, 12, 2023 na Waandishi wa Habari mkoani Mara wakati wa maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika kimkoa mjini Musoma katika ukumbi wa John Rudin Mwembeni Complex.
Katika maadhimisho hayo Waandishi wa Habari na wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi walijadili masuala mbalimbali ya kihabari ambapo Waandishi wa habari walilalamika mbele ya Katibu Tawala wa wilaya ya Musoma Justine Manko aliyekuwa mgeni rasmi juu ya ushirikiano hafifu na ucheleweshaji wa taarifa katika baadhi ya taasisi za Serikali.
Mwandishi wa Habari mmiliki wa chombo cha habari mtandaoni Serengeti Media Centre na Antoma online Tv, Anthony Mayunga amefunguka na kueleza namna ucheleweshaji wa taarifa unavyowakwamisha Waandishi wa habari.
Anthony Mayunga Mwandishi wa Habari mmiliki wa chombo cha habari mtandaoni Serengeti Media Centre na Antoma online TV.
"Ma- OCD wawe wasemaji kwasababu wanakuwa wapo karibu wilayani tofauti na Ma- RPC wanakuwa wapo mkoani kuja kupata taarifa kutoka kwake kama msemaji inachukua muda sana na wakati mwingine tukio linaweza kutokea lakini yeye anakuwa hajapata taarifa.
"Tukio linaweza kutokea OCD yupo pale, Mwandishi wa habari yupo pale lakini OCD hawezi kulisemea kama kiongozi wa Polisi wilaya mpaka taarifa iende kwa RPC yeye ndiye akalisemee ambaye hakuwepo eneo la tukio.
Mayunga amesema hali hiyo inachelewesha Waandishi wa habari kuripoti taarifa kwa wakati na kwamba wakati mwingine taarifa utolewa tofauti na ile iliyoshuhudiwa kwenye tukio.
"Tukio limetokea Mwandishi umeona lakini unaweza shangaa taarifa inatolewa tofauti na ulivyoona wewe Mwandishi. RPC anakuwa hayupo eneo la tukio anapelekewa taarifa anaweza kutoa taarifa tofauti na ile Mwandishi uliyoona.
"Mwandishi wa Habari akija kuandika kile alichokiona inaleta shida kwakuwa tayari RPC kasema yake na ndiye msemaji, inasababisha migongano ya kitaarifa kati ya Mwandishi wa habari na RPC" amesema Mayunga.
Mayunga Ameiomba Serikali kushusha mamlaka ya usemaji kwa viongozi wa chini ili kuharakisha upatikanaji wa taarifa ambapo ameomba wakuu wa Polisi wilaya wawe wasemaji kutoa taarifa kwa Waandishi wa Habari hususani taarifa za matukio.
"Tunaomba hizi mamlaka za chini zishushiwe nguvu yawepo mambo machache ambayo RPC atatakiwa kuyasemea haya mengine kama matukio wasemaji wawe Ma-OCD.
"Hii itawarahisishia kazi Waandishi wa Habari, tukio linatokea wakati mwingine unapiga simu RPC hapokei na yupo mkoani Mwandishi yupo wilayani, matokeo yake Mwandishi unashindwa kuandika habari wananchi wanaanza kukulalamikia kuwa hujaandika habari huwenda umehongwa pesa kutotoa habari kwasababu tu RPC hajabalansi stori" amesema.
Mayunga ameongeza kusema kuwa changamoto nyingine ni madaktari kuthibitisha tukio lakini bado Mwandishi wa habari kulazimika kumfuata RPC kulisemea tukio hilo.
" Mfano ajali inatokea au mtu kafa kafikishwa hospitali daktari kathibitisha lakini huku kwingine unaambiwa RPC ndiye athibitishe wakati anayepaswa kuthibitisha kifo ni Daktari hii inaleta shida na kusababisha ucheleweshaji wa taarifa" amesema Mayunga.
Mohamed Nyabange Mwandishi wa Redio Mazingira na Redio Abood amesema miaka ya nyuma ofisi ya RPC ilitoa taarifa kwa wakati lakini kwa sasa imekuwa tofauti huku akishauri taarifa zitolewe kwa wakati.
"Miaka ya nyuma ofisi za Ma- RPC zilikuwa na utaratibu mzuri hata usipomkuta RPC ulikuwa unakuta press release ( Taarifa kwa vyombo vya habari) kwa PS wake (Katibu Muhtasi) lakini kwa kipindi hiki imekuwa ni vigumu kupata taarifa za Polisi. Hali hii imesababisha wananchi kukosa taarifa za Polisi kwa wakati.
"Polisi watumie utaratibu wa press hata kama hayupo tukute kwa PS hii itatusaidia kuripoti habari kwa wakati ukizingatia wanahabari tunafukuzana na muda, ukichelewa kuipata ukapeleka kwenye chombo chako inakuwa imepoteza uzito". amesema Nyabange.
Karoli Jacob Mwandishi wa Habari wa Clouds Tv amesema uhuru wa vyombo vya habari bado ni changamoto kwakuwa baadhi ya viongozi wa Serikali hawaoneshi ushirikiano huku baadhi ya ripoti zikikinzana.
"Waandishi wa Habari tunakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yetu kama sheria na katiba inavyosema.
"Kuna changamoto kubwa Jeshi la Polisi , Afya katika utoaji wa ripoti za uchunguzi, ripoti za Madaktari baadhi zinapingana na uhalisia mfano kuna mtu aliuawa kwa kupigwa risasi na Askari Polisi.
"Ripoti ya Dkt. ikasema alianguka chini akavunjika mguu, habari ikakinzana sekta ya afya na polisi, RPC akafika hospitali akathibitisha mtu yule alipigwa risasi"amesema.
Karoli amesema licha ya Serikali ya awamu ya sita kuwa na dhamira nzuri na ya kusaidia Waandishi wa habari kufanikisha kazi zao za kihabari bado kuna urasimu wa utoaji taarifa kwa baadhi ya viongozi wa Serikali.
"Serikali ya awamu ya sita ina dhamira nzuri ya kusaidia Waandishi wa habari na imeweka mazingira mazuri ya vyombo vya habari lakini baadhi ya viongozi wa Serikali wamekuwa wakitushika miguu na kutukwamisha.
" Tunaomba viongozi waliopo chini wasaidiwe kujua umuhimu wa Waandishi wa habari katika kuhabarisha umma ambalo ni takwa la kisheria na kikatiba" amesema.
Karoli ameongeza " Ukienda kwa Wakurugenzi wa Halmashauri baadhi yao hawana ushirikiano atakutuma kwa mkuu wa idara ukienda nao wanakuruka wanasema wao siyo wasemaji matokeo yake stori inakosa upande wa pili.
Katibu Tawala wa wilaya ya Musoma aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Justine Manko alipokea changamoto hizo na kuahidi kuzifikisha katika taasisi za Serikali ili zifanyiwe utekelezaji.
Katibu Tawala wa wilaya ya Musoma Justine Manko aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya habari yaliyofanyika kimkoa mjini Musoma
Post a Comment