HEADER AD

HEADER AD

MAAFISA USTAWI, WATENDAJI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA KUWALINDA WATOTO

 



Na Patricia Kilemeta, Dar es Salaam

KAMISHNA wa Ustawi wa Jamii wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee kutoka makundi maalum, Dk. Nandela Mhando ametoa rai kwa Maofisa Ustawi wa ngazi zote kushirikiana na umoja wa Wamiliki wa Vituo vya kulea Watoto wadogo na wa shule ya Awali (UVIWADA) kuhakikisha wanatoa elimu ya kuwalinda watoto dhidi ya madhara yanayoweza kuwatokea.

Dk.Mhando ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wakati wa zoezi la ugawaji wa vyeti kwa wahitimu mafunzo ya malezi na makuzi ya watoto wa vituo vya kulea watoto wadogo na wa shule ya awali (UVIWADA) pamoja na walezi wao.

Hatua hiyo imekuja wakati Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi, Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ambayo ilizinduliwa Desemba 2021 inayolinda watoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane ambayo inashirikisha Asasi za kiraia Katika Malezi jumuishi ya watoto kwenye nyanja mbalimbali za elimu, afya, lishe, Malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama. 

Dk Mhando  amewataka Maofisa hao kushirikiana na Watendaji wa kata na mtaa kwa kupita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kutoa elimu ya Malezi kwa jamii Ili kila mmoja aweze kuwajibika kuwalinda na kuwasimamia watoto ipasavyo.


"Watoto wanastahiri kulindwa na jamii mzima, sio mzazi au mlezi peke yake, ni jukumu la kila mmoja kuona umuhimu wa kulinda mtoto katika mazingira yake, hivyo basi tukishirikiana na watendaji wa Kata au mtaa tutaweza kufanikiwa atika Hilo," amesema Dk.Mhando. 

Ameongeza kuwa, wanaotekeleza vitendo vya ukatili wanaishi kwenye jamii, hivyo basi wanapaswa kufuatwa ili waweze kuelimishwa na kujua madhara ambayo yanaweza kuwapata watoto waliofanyiwa vitendo hivyo.

Amesema kuwa, watoto waliopitia kwenye ukatili wanaathirika kisaikolojia, hata ukuaji wake unarudi nyuma, kama jamii inapaswa kuwajibika na wale watakaobainika kuwafanyia ukatili watachukuliwa htua kali za kisheria.

" Kuna kesi nyingi za kutelekezwa watoto, ubakaji, ulawiti na unyanyasaji wa namna moja au nyingine kwa watoto, kesi hizo zimejitokeza kwa sababu wazazi au walezi wameshindwa kuwajibika kwa watoto wao" amesema.

Amesema hali hiyo imesababisha  watoto kuathirika kiakili, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali Ili kutoa elimu ya malezi jumuishi kwa jamii zetu ili kila mmoja aweze kujua wajibu wake" amesema Mhando.

Amesema kuwa, kutokana na hali hiyo, Maofisa Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau wengine wanapaswa kutoa elimu kwa jamii ya kupinga vitendo vya ukatili Ili watoto waweze kulelewa katika hali ya usalama.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vituo vya Kulea Watoto wadogo na wa shule ya Awali (UVIWADA) Mkoa wa Dar Es Salaam, Shukuru Mwakasege amesema kuwa, vituo vya kulea watoto vinawapokea watoto kuanzia umri wa miaka mitatu hadi mitano, lakini baadhi ya watoto  wanaofikishwa kwenye vituo hivyo  wanakua tayari wameshafanyiwa  vitendo vya ukatili wa namna moja au nyingine.

" Vituo vyetu vinachukua watoto kuanzia umri wa miaka mitatu hadi mitano, lakini baadhi yao wanakuja wakiwa tayari wameshafanyiwa vitendo vya ukatili ikiwamo kibakwa, kulawitiwa au kuteswa, jambo ambalo linaathiri ukuaji wao," amesema Mwakasege.

Ameongeza kuwa, wamiliki wa vituo hivyo wakigundua kuna mtoto kafanyiwa ukatili wamekuwa wakiwashirikishs wazazi lakini hawatoi ushirikiano wowote badala yake wanasema suala hilo limemalizwa kifamilia.

Amesema kuwa, kwakuwa vituo hivyo havina watalaam wa saikolojia, wanaendelea kukaa na Watoto hao  bila ya kuwapa msaada wowote.

Ameiomba Serikali kutoa elimu kwa jamii ili waweze kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto kwa sababu wanaotekeleza vitendo hivyo wanaishi katika jamii.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wamesema kuwa, kutowajibika Katika malezi ya mtoto kwa wazazi na walezi kunachangia kuendelea kujitokeza Kwa vitendo vya ukatili.

" Baadhi ua wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wanashindwa kuwajibika kwenye Malezi, jambo ambalo limechangia kuendelea kujitokeza Kwa matukio ya ukatili Kwa watoto, hivyo basi seeikali inapaswa kutoa elimu kwa jamii na pia kutengeneza Sheria Kali ambazo zitawawajibisha watu wote watakaobainika kufanya ukatili Kwa watoto," amesema Omary Khamis (56) mkazi wa Dar ss Salaam.

Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na Serikali Mwaka 2017 zinaonyesha  kuwa kesi zilizofunguliwa  za ukatili kwa watoto zilikua 13,457 na  Mwaka 2018 kesi zilikua 14,419 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.2 na Mwaka 2019 kesi  zilizoandikishwa zilikua 15, 980 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 10.8.

No comments