HEADER AD

HEADER AD

JICHO LA TANZANIA ORGANIZATION NA MKAKATI UTOAJI ELIMU RASILIMALI ZILIZOSAHAULIKA


>Lasema matunda pori ni rasilimali yenye fursa lakini yamesahaulika kibiashara 

>>Yabaini uwepo wa matunda pori yanayooza bure licha ya kuwa ni fursa ya biashara 

>>Lajipanga kutoa elimu kwa wananchi ili wafanye biashara ya matunda pori wajiinue kiuchumi

Na Dinna Maningo,  DIMA Online

JICHO la Tanzania Organization (JTO) ni Shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu jijini Dodoma, lililounganisha watu kutoka katika mikoa mbalimbali ndani ya Tanzania Bara na Zanzibar bila kujali Itikadi za kidini, kabila na vyama vya kisiasa kwa lengo la kuweka nguvu pamoja katika kufanikisha masuala ya kijamii.

Shirika hilo pamoja na majukumu mengine limedhamilia kutoa elimu ya umuhimu wa wananchi kuzitumia fursa za rasilimali zilizosahaulika ili kujipatia kipato na ajira.

Akizungumza na DIMA Online, Mwenyekiti wa Jicho la Tanzania Organization Sospeter Ndabagoye amesema kuwa, kuna rasilimali nyingi nchini hususani maeneo ya vijijini zilizosahaulika katika jamii hazina thamani lakini zina fursa kubwa kwa wananchi katika kujipatia kipato.

      
Amesema shirika hilo limedhamilia kutoa elimu kwa wananchi hususani wa vijijini kutumia fursa ya matunda pori ili kujipatia fedha na kujikomboa kiuchumi kwani matunda hayo yanapatikana kwa urahisi katika jamii ambayo mtu halazimiki kuwa na mtaji mkubwa wa fedha.

"Kuna Rasilimali zilizosahaulika katika jamii zetu hazina thamani mfano; matunda pori yapo ndani ya jamii zetu yanadondoka na hakuna mtu anayeyajali.

"Baadhi ya matunda hayo yanaliwa na binadamu  na mengine ni dawa kama tiba, yana virutubisho vingi vya kutosha kwa ajili ya afya. Mfano Tabora kuna matunda yanaitwa Ntalali, Ntonga na Sambia.

          Matunda pori Ntalali wengine huiata Sungwi

" Hayo ni matunda yanayoliwa yanapatikana porini mahali ambapo wananchi wa kawaida wapo lakini matunda yanaharibika bure hakuna wa kuyavuna yanadondoka chini na kuoza hayaonekani kuwa na thamani" amesema Sospeter.

Ameongeza kuwa matunda hayo wananchi wakijulishwa namna ya kuyaongezea thamani na namna ya kuyafungasha vizuri yakaenda kuuzwa sokoni yanaweza kuwa na faida nzuri na kumwingizia kipato.

Mwenyekiti huyo amewaomba wananchi kuona umuhimu wa kutumia fursa ya biashara itokanayo na matunda ya asili ya porini ili kujiingiizia kipato.

        Matunda pori yanayofahamika kwa jina la Nkenene kwa kabila la Wakurya 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti hyo wa Jicho la Tanzania Organization amesema kuwa, kumekuwepo wimbi la umasikini linaloikabili jamii, athari za matumizi ya teknolojia ya habari, dawa za kulevya, ukuaji wa mtandao wa kusambaza imani na dini potofu.

Pia uharibifu wa mazingira, magonjwa ya mlipuko, changamoto za afya ya akili, elimu duni kwa jamii kuhusu uraia na utawala bora, ukosekanaji wa ajira na hali duni za kimaisha katika jamii.

Amesema hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo katika jamii sambamba na jamii zinazo hamahama za wafugaji, waokota matunda pori,wala mizizi na wavuvi.

"Ili kuwepo na maendeleo endelevu, tumeanzisha Shirika la Jicho la Tanzania  katika kuleta mabadiliko ya changamoto hizo, kwa kuwaunganisha vijana, akina mama na makundi yote ya kijamii kuwapatia elimu ili kujitambua na kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye mazingira yao.

"Pia, kutumia tehama katika kujiingizia kipato njia inayoweza kuwasaidia watanzania wengi kujiajiri pamoja na kushirikiana na serikali kupinga matumizi mabaya ya madaraka, rushwa, unyanyasaji wa kiraia, matumizi mabaya ya rasilimali za taifa pamoja na ukwamishaji jitihada za serikali katika kuleta maendeleo endelevu" amesema Sospeter .

>> Jicho la Tanzania Organization ni Taasisi mahususi iliyo sajiliwa kwa namba 00NGO/R/4753 kwaajili ya watanzania wazalendo walioko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye nia ya dhati na thabiti ya Kutoa elimu ya Uraia,Utawala bora,Utunzaji wa Mazingira.

Pia ukatili wa kijinsia, afya,ujasiriamali, tehama, maadili na uzalendo kwa jamii na kutambua nafasi na mchango wa kila mmoja katika kujiletea maendeleo .











No comments