HEADER AD

HEADER AD

MADIWANI WALALAMIKA WAKULIMA 5,000 KUHUDUMIWA NA MAAFISA UGANI WAWILI

Na Daniel Limbe,Biharamulo

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera,wameiangukia serikali kwa kuitaka kusaidia upungufu wa watumishi wa Umma, huku ikielezwa kuwa wakulima zaidi ya 5000 wa Kata ya Nyamigogo wakihudumiwa na maafisa ugani wawili pekee.

Hatua hiyo inatajwa kuwa kikwazo cha kufikia malengo ya uzalishaji wa mazao kwa tija badala yake wakulima wanaendelea kupata chakula cha kujikimu na kushindwa kukabiliana na lindi la umaskini wa kipato.

Diwani viti maalumu, Beatrice Ayuko, amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kata ya Nyamigogo kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambapo ameiomba serikali kusaidia kupunguza uhaba wa watumishi wa sekta ya kilimo.

Diwani viti maalumu, Beatrice Ayuko

"Inasikitisha sana kuona wakulima zaidi ya 5,000 waliopo kwenye kata ya Nyamigogo wakihudumiwa na maofisa ugani wawili tu waliopo kwenye kata nzima hali hii tunaamini haiwezi kuwasadia wakulima wetu kuondokana na kilimo cha mazoea"amesema Ayuko.

Mbali na hilo, Diwani wa kata ya Lusahunga,Amos Madebwa,ameitaka serikali kuongeza nguvu za upelekaji wa fedha kwenye kata zao ili kurahisisha ukamishwaji wa miradi ya maendeleo iliyokwama muda mrefu.

"Pamoja na nguvu za wananchi wetu kuchangia maendeleo... tunaiomba serikali isaidie kutoa fedha kwaajili ya miradi ambayo imekwama ikiwemo ujenzi wa shule za msingi,sekondari,zahanati,vituo vya afya na ujenzi wa matundu ya vyoo kwaajili ya wanafunzi wetu" amesema Malembwa.

Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Mihayo Miganyalo, amesema kwa kuwa serikali kuu inaendelea kutoa ajira za utumishi wa umma, ipo haja kwa halmashauri kuweka mgawanyo mzuri wa watumishi kwenye kata na vijiji kulingana na uhitaji uliopo.

   Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Mihayo Miganyalo

Kadhalika amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kushirikiana na madiwani wanapokwenda kutembelea miradi ya maendeleo badala ya viongozi hao kupewa taarifa pekee.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Dk. Sospeter Mashamba, amekiri kuwepo kwa miradi mingi ambayo haijakamilika kutokana na upungufu wa fedha huku akiwataka madiwani kuwahamasisha wananchi kuchangia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati kwa kuwa serikali pekee haiwezi kutatua changamoto zote.


      Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Biharamulo,Dk.Sospeter Mashamba,akitoa ufafanuzi kwenye kikao cha uwasilishaji wa taarifa za maendeleo ya kata.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Biharamulo wakiendelea na kikao cha Baraza lao.

                      

No comments